Pages


WALIOGOMA KUHESABIWA WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI - MBEYA

Kamanga na Matukio | 05:52 | 0 comments
 Pichani wananchi waliokataa kuhesabiwa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Bwana Guram Hussein Kifu. katikati ni Kiongozi wa Mgomo Bwana Ally Mwangoto, kutoka dini ya Kiislamu wanaojiita wenye msimamo mkali wakiwa chini ya ulinzi katika mahabusu ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Ruiwa,Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya,wakisubiri kupelekwa Polisi wilayani humo.
Picha na Habari na Ezekiel Kamanga,Mbarali.
Licha ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka waislamu  nchini kushiriki zoezi la Sensa  ya watu makazi, hali hiyo imeonekana kuwa tatizo kwa kijiji cha Ruiwa Kata ya Ruiwa Wilayani Mbarali  ambapo watu wasita wanaosadikiwa kuwa ni waislamu  wenye msimamo mkali kugoma kuhesabiwa  kwa madai  kuwa serikali imepuuza  madai yao.

Imeelezwa kuwa waislamu hao walishaeleza serikali kuwa hawako tayari kuhesabiswa lakini bado serikali imeshindwa kutekeleza matakwa yao na hivyo kukataa kuhesabiwa.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusiana na madai hayo , Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruiwa Bw. Jordan Masweve alisema kuwa kwa kata zoezi la sense toka limeanza imekuwa ni tatizo kubwa sana kutokana na watu hao kuonyesha msimamo wao wa kutotaka kuhesabiwa.

“Wao wanadai kuwa hawapo tayari kuhesabiwa hata iweje msimamo wao ni mmoja hata wafanywe nini lakini suala ni kutokubali kuhesabiwa tu kwa madai serikali imeepuza madai yao toka mwanzo ya kutotaka kuhesabiwa”alisema.

Bw. Masweve alisema tukio hilo limetokea  Agosti 27 mwaka huu majira ya saa 8.30 mchana  katika kijiji cha Ruiwa wakati makarani wa sense  walipofika katika makazi wa wananchi hao  wakiongozwa na Mtendaji wa kijiji  kwa lengo la kuwataka wakubali kuhesabiwa lakini waligoma.

Alisema  hata hivyo zilifanyika jitiha za kuwasihi kushiriki zoezi hilo  lakini hawakutaka kukubali  ndipo mgambo wa kijiji walipowakamata na kuwapeleka kwenye ofisi ya Kata.

Bw. Masweve aliwataja waislamu waliokamatwa kuwa ni Ally Mwangoto,Subeti Juma, Abinala, Pembe ,Ally Suleiman pamoja na Nawab Suleiman licha ya kufikishwa katika ofisi ya kata bado waliendelea kuwa na msimamo wao  kuwa hawako tayari kuhesabiwa na kudai kuwa vyovyote itakavyokuwea wapo tayari  hata kuchinjwa au kufungwa jela lakini si kuhesabiwa.

Hata hivyo alisema kuwa waislamu hao walidai kuwa hata Mkuu wa Wilaya akifika hapo hawako tayari kuhesabiwa msimamo wao ni mmoja tu .

“Bado tupo nao hapa ofisini tukisubiri Mkuu wa Wilaya ya Mbarali ,na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbarali ili waje kuwachukua  watu hawa”alisema.

Aidha aliongeza kuwa kabla ya zoezi hilo kuanza  kulikuwa na mikutano ya  hadhara ambayo ulikuwa unaendeshwa na  viongozi wa kiislamu kutoka Jijini Mbeya  walikuwa wakihamasisha waislamu wenzao kuwa ambao hawatakuwa tayari kushiriki zoezi hilo kukimbilia misikitini ambako watawapelekea chakula mpaka zoezi hilo litakapokuwa limekamilika.

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa njiani kuelekea kijiji cha Ruiwa  Mkuu wa Wilaya Mbarali Bw. Gulamu Hussen Kiffu alisema amepata taarifa za tukio hilo lakini bado hajafika huko lakini yupo njiani kuelekea huko ili aweze kujua undani wa tukio hilo.

“Kwasasa nipo kwenye gari naelekea Ruiwa kwa ajili ya tukio hilo mara baada ya kufika na kuangalia tukio lilivyo nitatoa taarifa kamili na hatua zipi ambazo tutakuwa tumechukua”alisema.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Bw.Athuman Diwani alisema bado hajapata taarifa hizo na kudai kuwa taarifa zote za matokeo atatotoa mara baada ya zoezi la sense kumalizika.

UKOSEFU WA WAWEKEZAJI NDIO CHANZO CHA UCHANGISHWAJI WA USHURU MKUBWA - MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:51 | 0 comments
Habari na Eseter Macha, Mbeya...
 Imefahamika kuwa ukosefu wa wawekezaji Mkoani Mbeya unachangiwa na ushuru mkubwa unaotozwa na halmashauri ya jiji hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara wakubwa kuwekeza katika mikoa mingine na hivyo kutopanda kwa mapato halmashauri.

Hayo yamesemwa na hivi karibuni na Mbunge wa viti maalum kupitia chama cha mapinduzi(CCM) Mkoani Mbeya Dk Mary  Mwanjelwa hivi karibuni  katika kikao maalum cha maadili cha baraza la madiwani  (RCC) Kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa.

Alisema kuwa kuwa kuna haja kubwa ya halmashauri kujipanga kikamilifu na kuhakikisha kodi za wawekezaji wakubwa zinapunguzwa ili kuongeza kasi ya kuwa na wawekezaji hususan katika sekta mbalimbali kama yalivyo majiji mengine na si wawekezaji kukimbia mkoa.
 
“Mapato ya ushuru yanachangia wawekezaji kukimbia mkoa na kuwekeza katika mikoa mingine jamani sasa ni wakati sasa mkurugenzi kaa na timu yako muhakikishe swala hili linapatiwa ufumbuzi ili tuweze kurejesha imani kwa wawekezaji warudi kuwekeza mbeya  ukilinganisha mkoa huu unauwezo wa kulisha nchi nzima katika kilimo”Alisema.

Alisema kuwa watendaji katika halmashauri ni wajibu wenu kuhamasisha wawekezaji kuwekeza mbeya ili kuweza kuwasaidia wakulimja wetu kupata soko la uhakika katika mazao ya chakula na biashara,shughuli za uvuvi ili kuweza kujiongeza kipato na kujikwamua kiuchumi na kuutangaza mkoa wa mbeya.

“Jamani mungu amejalia mkoa wa mbeya kwua na rasilimali nyingi za kutosha hususan katika swala zima la uwekezaji katioka kilimo ili kuwawezesha wananchi kupata fursa ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mzao ya chakula na biashara na kupata soko la uhakika”Alisema.

Bi.Mwanjelwa pia alitoa wito kwa madiwani kutoa elimu kwa jamii kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi agost 26 mwaka huu ili kuwarahisishia wasimamizi kupata takwimu sahihi zitaazosaidia serikali kujua idadi halisi ya watanzania.

VUGU VUGU LA UCHAGUZI NDANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

Kamanga na Matukio | 05:50 | 0 comments
 Na Esther Macha,Mbeya
Wakati vugu vugu la uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)likiendelea kushika kasi Rais wa Chama wakandarasi Wenyeji Tanzania(TLCO)Bw.Kura Mayuma amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Mkoa wa Chama hicho Mkoani Mbeya.

Alisema kuwa lengo ni kushawishi  serikali kukataa  sheria na kanuni kandamizi kwa wananchi ambazo zimetungwa na Bunge n a mabaraza ya madiwani Mkoani hapa.

Bw. Mayuma alisema hayo  jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo  katika Ofisi za chama cha mapinduzi zilizopo eneo la Sokomatola.

Alisema kuwa lengo la kugombea nafasi hiyo ni kutaka kurudisha hadhi ya chama hicho  Mkoani hapa ambacho tayari kimeppoteza mvuto kwa wanachama wake ili mwaka 2014 wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa uwe rahisi kupata viongozi wenye sifa.

“Pia katika uchaguzi huu kutawezesha kupata viongozi wenye sifa  kwa uchaguzi wa mwaka 2015 kwani tayari tutakuwa tumepata viongozi wenye sifa  ya kuongoza na hapa nimewingia kwa makusudi ili kuweza kukinusuru chama cha mapinduzi “alisema.

Alisema watu wanachaguliwa  katika chama watekeleze matakwa ya wananchi  badala yake wanashindwa kufanya yale waliyoagizwa  na hivyo kuanza kutokea vurugu  za wamachanga ambayo chanzo chake ni watendaji wa chini na hivyo CCM kuonekana kushindwa kuwajibika kwa wananchi.

Bw. Mayuma alisema hiyo inatokana na watendaji wa serikali kushindwa kuwajibika ,sera ya chama cha mapinduzi ni nzuri ila watendaji wake ndo wamekuwa tatizo kubwa.

Kwa Upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoani mbeya Bw. Maganga Sengelema alisema kwa sasa chama hicho kinajipanga vizuri ili kuweza kupata viongozi ambao watakitetea chama  tawala katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014.

UPUNGU WA VIFAA VYA MAABARA KATIKA HOSPITALI YA MKOA WA MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:49 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Upungufu wa  vifaa katika  kitengo cha Maabara katika hospitali ya Mkoa wa Mbeya umetajwa kuwa changamoto kubwa  ambayo inapelekea wagonjwa kuwa katika wakati mgumu  wa kupata vipimo muhimu .

Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa Huduma za Maabara  katika hspitali ya Mkoa wa Mbeya Dkt.Ezekiel Tuya  wakati alipozungumza  na gazeti hili kuhusu matatizo ambayo yanakwamisha shughuli za maabara hosptalini hapo.

Alisema ukusefu huo wa vifaa unasababisha kuendelea kudorola kwa huduma , na tatizp kubwa  lingine ni upungufu wa wataalamu katika taaluma ya afya  hasa vitengo vya maabara  katika hospitali hiyo ambapo hali hiyo inasababisha  wanafdunzi kuyakimbia masomo ya sayansi  ambayo ndiyo msingi wa afya.

“Hili ni tatizop kwani mara nyingi wanafunzi wanaotaka kuja kufanya mazoezi wanashindwa kutokana na kutokuwa na kutokuwa na wataalamu wa hivyo ni jambo ambalo ni muhimu ambali serikali inatakiwa kulifanyia kazi , na hata huu ukosefu wa vifaa nao unatutesa sana hasa ukizingatia kipindi hiki ambacho tuna wagonjwa wengi ambao wanahitaji vipimo ili waweze kuazishiwa matibabu ya dawa”alisema.

Alisema tatizo linguine  ukosefu wa vifaa wa vifaa na vitendanishi  katika maabara vifaa ambavyo hurahisisha utendaji wa kazi  kwa watumishi wa maabara.

Hata hivyo Dkt. Tuya ameiomba serikali  kushughulikia ukosefu wa  wataalamu wa maabara nchini  ili kunusuru maisha ya watanzania wanafariki dunia kwa kukosa huduma ya vipimo kwa wakati .

UCHAMBUZI. IMANI POTOFU KWENYE MATUMIZI YA SARAFU KWENYE POMBE ZA KIENYEJI

Kamanga na Matukio | 05:48 | 0 comments
Na Ester Macha.
Katika kuhakikisha kuwa kila mwananchi anaweza kuendesha maisha yake ya na familia wananchi wamekuwa wakijitahidi kubuni mbinu mbadala za biashara ili waweze kujikwamua kiuchumi ili waweze kuondokana  na hali duni ya kimaisha .

Kundi ambalo limekuwa likijikita zaidi katika harakati za kuendesha maisha wanawake waliopo vijijini na mijini ambao asilimia kubwa wamekuwa walezi wa familia zao.

Lakini ni ukweli usiopingika kuwa kundi hili la wanawake linahitajitaji msaada wa hali na mali kwa kubuni mbinu zingine ambazo zitaweza kuwasaidia kuliko hili wanalotumia ambalo ni  hatari kwa afya za binadamu.

Hivi karibuni kumeibuka imani potofu kwa wapikaji pombe za kienyeji kutumbukiza sarafu katika mapipa ya pombe  na kuchemsha  kwa pamoja kwa imani kuwa pombe inakuwa kali sana  na hivyo kununuliwa kwa wingi kwa wateja wao.

Kuna umuhimu kwa mamlaka husika kuliona hili kwani linaweza kuleta athari kwa wanywaji bila wapikaji pombe kufahamu hili hivyo  ni vema likafanyiwa utafiti wa kina ili kunusuru afya za wanywaji wa pombe  za
kienyeji.

Biashara hii kwa asilimia kubwa inafanywa na wanawake  na kwamba hali hii inatokana na baadhi ya wanawake kuwa na hali duni ya kimaisha na hivyo kulazimika kubuni mbinu ambayo itawawezesha kuishi maisha yao kila siku.

Lakini  pia ikumbukwe kuwa mbinu ya utumiaji  sarafu katika pombe imewalazimu wanawake walio wengi kutumia njia hiyo kutokana na pombe kutokuwa na uchungu na hivyo kushindwa kununuliwa na wateja ambao wanaamini kuwa ni msaada kwao baada ya kununua kinywaji hicho.

Nionavyo katika utumiaji wa sarafu hizi katika pombe si mzuri kiafya kwani hawa watumiaji wanatumia pasipo kuelewa kuwa kwa binadamu inaleta athari gani hivyo ni muhimu wizara ya afya kuliona hili na  kulifanyia kazi au  kutoa elimu kwa wapikaji wa pombe .

Sawa  sote tunafahamu  ugumu wa maisha  uliopo kwa wananchi lakini kwa mbinu hii ya utumiaji wa sarafu si mzuri hivyo  ni vema wakatafuta njia nyingine ambayo itawawezesha katika upikaji wa pombe hizo kuliko kutumia sarafu ambazo haijulikani zimetengenezwa kwa madini gani.

Njia hiyo kiafya si nzuri nashauri benki kuu ya tanzania kanda ya mbeya kutembelea maeneo ya vijijini na mijini kwa wanawake ambao wanajihusisha na upikaji wa pombe ili kuweza kuwapatia elimu juu ya matumizi ya sarafu katika upikaji wa pombe.

Elimu ikitolewa na kufahamu madhara yake wapikaji wa pombe watakuwa na woga na kubuni biashara nyingine ambayo haitaweza kuathiri afya za wananchi ambao ni nguvu kazi ya taifa inayotegemewa.

Kwa haraka jambo hili linaweza kuwa rahisi lakini lina madhara makubwa hata kama haiwezi kudhuru sasa lakini ni hali ambayo inaweza kutokea baadaye  tena kwa kwa kiwango kikubwa  hivyo ni muhimu likafanyiwa kazi haraka ili kunusuru afya za wanywaji .

Sababu tumezoea serikali huwa inafanyia kazi jambo mpaka pale waone kumetokea athari ikwa jamii lakini hivi hivi jambo hili litachukuliwa kirahisi tu na kuachwa kama lilivyo bila kufanyiwa kazi huku wapikaji wa pombe wakiendelea na shughuli zao ikama kawaida.

Ifike wakati  hata kwa wapikaji wa pombe za kienyeji wafahamu kuwa sarafu si nzuri kwa matumizi ya kinywaji chochote kile ambacho ni matumizi kwa binadamu .

Hata hivyo meneja msaidizi sarafu benki kuu ya tanzania kanda ya mbeya Bw.vincent mtan amewashauri  wapikaji wa pombe za kienyeji  wenye imani potofu ya kutumbukiza sarafu katika mapipa  na kuchemsha kwa pamoja  kwa imani ya kukolea kwa pombe ni uharibifu na makosa kisheria na kwamba jitihada zinaendelea kufanyika kuboresha sarafu.

Alisema kuwa  ili sarafu zisiweze kuchuja rangi  licha ya kuchemshwa kwa muda mrefu katika mapipa ya  pombe huku akisisitiza kuwa sarafu zote kuanzia senti tano  hadi sh.200 bado zipo katika mzunguko na zinatumika kihalali .

Sawa nakubaliana na ushauri wa benki kuu kuwa wananchi waachane na mila potofu lakini hapo naona bado haitoshi ila kitu kikubwa ambacho kinatakiwa kwa wahusika wakuu wa benki kuu na kuwapatia elimu kila kijiji na kata  ili elimu iweze kutolewa kwa kila mwananchi ili waweze kufahamu madhara ya utumiaji wa sarafu.

Lakini pia ikumbukwe kuwa  imani hiyo potofu kwa wananchi juu ya matumizi ya sarafu  katika upikaji wa pombe  unatokana na ugumu wa maisha uliopo katika jamii na hivyo katika kujitahidi kujinasua kimaisha wananchi wameona mbinu bora  ambayo itaweza kumudu maisha yao ni kutumia sarafu katika pombe ili iweze kuwa kali na hatimaye kupata wateja kwa wingi.

Nionavyo watendaji  wa kata na wenyeviti wa mitaa waanze zoezi hili mapema kwa kupita katika nyumba ambazo wananchi wake wanapika pombe za kienyeji kuchunguza kwa undani zaidi ili kubaini matumizi hayo ya sarafu katika pombe za kienyeji.

Hii itaweza kusaidia kwa kiasi fulani na kubaini wananchi ambao wanatumia sarafu hizo lakini ili zoezi hilo liweze kwenda vizuri hakuna budi wakaenda nalo taratibu .

Pia elimu hiyo itumike hata kwa wale ambao hawajihusishi na upikaji wa pombe kwa kuitisha mikutano ya hadhara katika vilabu vya pombe za kienyeji maana huko ndiko wanywaji wengi walipo,

Jukumu hili pia linapaswa kuanzia ngazi ya vijiji na kata na mjini kwani ni hali ambayo itaanza kuleta athari kubwa kwa jamii hivyo ni vema mamlaka zinazohusika kuzingatia  na kulifanyia kazi mapema ili kunusuru afya za watumiaji wa pombe za kienyeji.

Lakini ni vizuri pia serikali nayo mikajitahidi kukaa na wananchi wake kuhimiza kufanya miradi mingine ya kimaendeleo ambayo itakuwa haina madhara kwa wananchi na ambayo itakuwa na tija kwa wananchi kuwawezesha kumudu maisha yao ya kila siku.

Kwani yote hii inatokana na viongozi husika wa mitaa na kata kutokuwa wabunifu wa wa miradi kwa wananchi wake kwa kuanzisha miradi mbali mbali ambayo haina madhara kwa binadamu.

MAKALA JUU YA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Kamanga na Matukio | 05:47 | 0 comments
Makala na Ester Macha.
UDANGANYIFU  wa vitambulisho vya Taifa  wenye lengo la utambuzi wa watu Nchini umeingia dosari baada ya watendaji wa mitaa na  kata katika maeneo yao kugeuza zoezi hilo kuwa mradi wao binafsi na kusahau dhamana waliyopewa na serikali ya  kuwatumikia wananchi.

Kutokana na Unyeti wa zoezi hili kuna umuhimu wahusika wakuu waweze kuchukuliwa hatua mapema kwani Jiji Dar Es Salaam  ndo limeanza ndo wamekuwa wa kwanza kuanza mchakato huo sasa endapo mamlaka ya

vitambulisho ikifanya mzaha kuna hatari maeneo mengine yakashindwa kufikia malengo  vizuri kama ilivyotarajiwa zoezi hili.

Tunafahamu kuwa zoezi kama hili ni nyeti kwa Taifa lakini kinachokuja kushangaza ni kuona baadhi ya watendaji ambao si waaminifu wanataka kufanya mchezo kuhusu suala la vitambulisho ambalo ni muhimu ambalo linatakiwa kupewa kipaumbale.


Ni dhahili kuwa katika maeneo mengine ya Jijini Dar Es Salaam hayataweza kufanikisha zoezi hili  na wananchi walio wengi hawataweza kupata vitambulisho vya Taifa kutokana na urasimu uliopo na rushwa

iliyokithiri miongoni mwa watendaji ambao si waaminifu .

Nionavyo katika zoezi hili kumekuwa na changamoto  mapema kabla ya hata zoezi hilo halijakamilika mapema  hivyo kuna wajibu kwa serikali kufanya kila linalowezekana  kutoa elimu kwa wananchi kupitia

wenyeviti wake wa serikali kuhusu vitambulisho vya Taifa kuwa vinatolewa bure.

Hata hivyo katika zoezi hilo watendaji watatu wa mitaa walikamatwa kuhusiana na kuchukua rushwa kwa wananchi kati y ash.1000 mpaka 3000 kwa lengo la kuwaandikia barua ambazo zinaonyesha kuwa ni wakazi wa maeneo yao.


Pia maeneo ambayo yamekubwa na adha hiyo ni Yombo Vituko,Mwabe Pande na Bunju ambapo wananchi wake walidaiwa fedha na watendaji wa mitaa ili waweze kukamilishiwa zoezi la kupata vitambulisho hivyo.


Nionavyo serikali isipokuwa makini kuna hatari vijana na wazee waliopo Mijini na Vijijini kukosa vitambulisho vya Taifa hasa vijijini ambako watadanganywa sana na watendaji hawa ambao huko vijijini hujifanya miungu watu na kuwanyanyasa wananchi.


Katika hili Mamlaka inayohusika na vitambulisho lazima iwe makini na zoezi hili hasa vijijini kwani vitambulisho hivi vinaonekana kuwa dili kubwa  kwa watendaji wa mitaa hata wa kata kwani hawa jambo lao

ni moja.

Ili kukomesha tabia hii ninachofikiri ni kwa Halmashauri zinazohusika na utoaji wa ajira kusitisha ajira zao kwani kama hili limefanyika Dar Es Salaam je kwa mikoani itakuwaje ambako ndo kuna watu wengi ambao

hata hawaelewi chochote kile ,kufanyike utaratibu mzuri ambao utaweza kupelekea kila mmoja aweze kupata kitambulisho cha Taifa.

Ushauri wangu kuhusu  zoezi hili kwa Mamlaka ya  ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)kufanya kazi hii kwa undani zaidi kwani inawezakana kuwa kukawa na maeneo mengine  ambako kuna tatizo la upatikanaji wa

vitambulisho ,hivyo ni muhimu wakajaribu kupitia maeneo mtaa kwa mtaa ili kuweza kubaini tatizo na kulifanyia ufumbuzi  ili Mikoa na wilaya ambazo zinatarajia kufanya zoezi hili isitokee dosari.

Katika hili tayari baadhi ya wananchi wameanza kukatishwa tamaa kutokana na mchezo mchafu uliongia wa kutoa rushwa kwa viongozi wa mitaa il waweze kupatiwa huduma hiyo.


Lakini pia ikumbukwe kuwa wakati mpango wa uchangishaji fedha hizo kwa wananchi awali Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) inasisitiza kuwa uandikishaji huo ni bure na kuwa mwananchi yeyote hapaswi kutozwa fedha au gharama nyingine zozote lakini watendaji hawa wamekuwa wakienda tofauti na matakwa  na NIDA.


Dhuluma hii imekuwa ikifanyika kwa watu ambao hawana vitambulisho,kama vile kadi ya mpigakura, cheti cha kuzaliwa, ubatizo au hati ya kusafiria na ndipo maofisa waandikishaji huwaelekeza kwenda kwa watendaji wa mitaa na kata ili waweze kupata uthibitisho kuwa ni raia.


Nionavyo serikali isipokuwa makini kuna hatari zoezi hili lisiweze kukamilika vizuri kama ilivyotarajiwa endapo wahusika wanaohusika  na utozaji wa fedha hawatachukuliwa  hatua na pia kuwepo  na ufuataliaji

makini katika vituo vyote.

Lakini hivi karibuni Msemaji wa Nida,Bi. Rose Mdami alisema kuwa mwananchi yeyote hapaswi kutoa fedha yoyote ili kufanikisha mkakati wa kuandikishwa, hivyo akawaonya maofisa waandikishaji na wale wa serikali za mitaa kuacha tabia hiyo mara moja.


Mimi nadhani onyo hilo pekee halitoshi kinachotakiwa  kwa mamlaka ya vitambulisho ni kuwachukulia hatua kali wale wote waliohusika na utozaji wa fedha wakati zoezi hilo lilipoanza mapema mwezi wa saba mwaka huu.


Mamlaka ya vitambulisho Taifa ikumbuke kuwa zoezi hilo ni nyeti ambalo linatakiwa lifanywe  kwa umakini na hao wahusika waliokamatwa wachukuliwe hatua isiishie kukamatwa na polisi tu, zoezi hili bado linatakiwa kufanyika katika mikoa mingine sasa endapo wahusika wakikamatwa  na kuwekwa ndani na kutolewa  na kuishia mitaani bila ya kuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu kuna hatari mikoa mingine ambako zoezi  hili linatarajiwa kuendeshwa  kutofanikiwa hasa maeneo ya vijijini.


Nionavyo  hawa watendaji wa mitaa na kata wanaweza kuitia serikali katika matatizo kwani kwa mtindo huu  uraia unaweza kutolewa kiolela kwa wageni na watanzania kubaki wakiwa hawana uraia katika serikali 
lazima iwe macho na watendaji wake,kwasababu wamezoea kila mpango unaoletwa na serikali kwao wanaona ni sehemu ya kujipatia fedha.

Ifike wakati watendaji waweke kipaumbele kazi waliyopewa  na serikali badala ya kuweka maslahi mbele  kuliko dhamana waliyopewa na serikali ya kuwatumikia wananchi.

WADAU WA ELIMU WAIOMBA SERIKALI KUWEKA MJADALA WA KITAIFA JUU YA SHERIA YA ELIMU NA 25 YA MWAKA 1978

Kamanga na Matukio | 05:46 | 0 comments
Habari na Ester Macha, Ileje.
Wadau wa elimu  wilayani Ileje mkoanii Mbeya wameiomba serikali kuwepo na mjadala wa kitaifa juu ya sheria ya elimu namba 25 ya mwaka 1978  ambayo inadaiwa kutoweka wazi suala la wanafunzi kupeana ujauzito wakiwa shuleni.

Imeelezwa kuwa sheria ya sasa
  iliyopo imekuwa ikitoa adhabu kwa watoto  wa kiume pekee  hivyo wamependeza kuwa kuwa sheria  ambayo wataiuomba kurekebishwa  inapaswa kuwawajibisha wote wawili badala ilivyo hivi sasa,mwanafunzi wa kiume pekee anashitakiwa.

Tatizo la mimba mashuleni
 limeendelea kupamba moto na hivyo kulazimika wadau wa elimu kwa  ushirikiano wa wananchi kuomba  serikali kufanyia  marekebisho sheria ya elimu namba 25 ya mwaka 1978 ili iendane na  wakati uliopo hivi sasa.

Akizungumza wakati wa kikao na wadau wa elimu wilayani hapo Hivi karibuni Mratibu wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na watoto na akinamama (KIMAWAMBE)Bw. Mohamed Cheto alisema kuwa
  wakuu  wakuu wa shule mbalimbali wilayani Ileje  wameenda  mbalii zaidi na kuhimiza mabadiliko hayo ya sheria ya elimu.

Alisema kuwa kuanzia sasa
 shirika hilo litahakikisha lifanya jitihada za kuhakikisha kuwa tatizo la mimba mashuleni linakuwa ni  historia,kwani ni jambo ambalo limekuwa ni kero kwa muda mrefuna kusababisha watoto wa kike walio wengi kukatisha masomo kwa tatizo la mimba.

Bw.Cheto alisema  watafanya suala la
 elimu kuwa  miongoni mwa wahusika kwa lengo la  kutokomeza  dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii hasa wanafunzi wa kike kuwa suluhisho la kumaliza mimba mashuleni na wala sio  kuwashitaki wanafunzi wote mahakamani badala yake ni kukaa meza moja na wahusika  ili kuyamaliza kwa mafunzo na elimu ya saikolojia.

“Hakuna jambo ambalo haliwezekani ila kikubwa ni kujipanga tu kwa kutoa mafunzo  ya elimu ya Saikolojia kwa wahusika wote wawili ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wazazi wa familia zote”alisema.

Hata hivyo wananchi kwa ujumla walisema kuwa kuna haja sheria hiyo  ikafanyiwa marekebisho ili adhabu hiyo iweze kutolewa kwa wote.

KWANINI WAANDISHI WA HABARI WANAWAKE HAWAJIKITI KATIKA UANDISHI WA HABARI WA JINSIA YAO?

Kamanga na Matukio | 05:45 | 0 comments
Habari na Ester Macha,Mbeya.
Kutokana na waandishi wa habari wanawake nchini kutojikita zaidi katika uandishi wa habari za wanawake imeelezwa kuwa hali hiyo  imesababisha  habari zinazohusu wanawake kutoripotiwa kwa undani zaidi na badala yake waandishi wa habari wanaume ndio wamekuwa wakiandika habari hizo.

Waandishi wa habari wanawake ndo wanatakiwa kuwa nguzo muhimu katika kuandika habari za afya hususani wanawake waliopo vijijini,wengi wanafahamu matatizo ya wanawake hivyo itakuwa rahisi kuripoti habari hizo kwa upana .

Mwito huo umetolewa  jana na Mkufunzi wa wa mafunzo ya habari za afya Dkt.Ahmed Twaha  wakati akitoa mada kwa waandishi wa habari wanaohudhulia mafunzo hayo ya siku nne ambayo yanaendeshwa na umoja wa  clabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC).

“Nyinyi kama waandishi wa habari wanawake  mnatakiwa kuwa wa kwanza  kuandika habari za afya kutokana na kuwa na uelewa zaidi kuhusu masuala ya wanawake kwa maradhi mbali mbali ambayo wanaugua,kwa uelewa wenu mtaweza kuandika kitu ambacho ni kizuri”alisema.

Alisema mara nyingi waandishi wa habari wanaume ndio wamekuwa wakiandika zaidi habari za afya tofauti na wanawake wenyewe ambao wana uelewa zaidi ,kuna umuhimu wanawake kuanza rasmi kujikita zaidi na uandishi wa habari hizi za afya.

Aidha Dkt.Twaha alisema kuwa wakati wa kuandika habari za afya ni muhimu kuandika  kwa takwimu sahihi  ili jamii iweze kupata taarifa ambayo imefanyiwa utafiti wa kina na kuelewa nini kinazungumzwa.

Hata Mkufunzi huyo alisema pia kuna umuhimu kuangalia changamoto zinazowakabili  wanawake waliopo vijijini kuhusiana na huduma za afya,na kwamba asilimia kubwa ya wanawake na watoto ndio wanaotibiwa katika hospitali kuliko wanaume.

Kwa upande wao waandishi habari wanawake wanaohudhulia mafunzo ya habari za afya walisema kuwa wanashindwa kuandika habari hizo  kutokana na kutokuwa na vitendea kazi pamoja na uwezeshaji wa kifedha kutokana na habari nyingi kuwa vijijini .

Mafunzo hayo yanaendeshwa na umoja wa clabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC)na yanajumuisha waandishi 18 kutoka Mkoa wa Mbeya.

APPLE LINE BINGWA WA MCHEZO WA VISHALE (DARTS) MKOA WA MBEYA

Kamanga na Matukio | 03:28 | 0 comments
Wachezaji wa Apple line wakifurahia kubeba vikombe vyote vya ushidi wa  Darts mkoa wa mbeya baada ya kuigalagaza timu ya Polisi mkoa wa mbeya huku wakitoka bila kuaga baada ya kushindwa vibaya katika mchezo huo


Mwenyekiti wa klabu ya darts ya Apple line Weston Asisya akiwashukuru wachezaji wenzake kwakupata ushindi huo mkubwa pia timu hiyo imewaomba wakazi wa Mbeya kushiriki katika sensa ya watu na makazi inayoanza jumapili
ya tarehe 26 mwezi huu

Mwenyekiti wa klabu ya Apple line akimkabidhi kikombe cha ushindi wa mkoa mkurugenzi wa Apple line Bwana Chaula ambaye pia ni mfadhiri wa timu

Mchezaji bora wa Darts mkoa wa mbeya Raymond Mushi akiwa ameshikilia kombe lake la uchezaji bora



Mshindi wa pili katika uchezaji bora bwana Lazaro akiwa ameshika kikombe chake cha ushindi
wachezaji wa Apple line akiendelea kupongezana kwa kucheza darts


Hivi ndiyo vikombe walivyoshinda Apple line.Kwa hisani ya Mbeya Yetu








MATUKIO YA MKUTANO WA HADHARA ULIOJADILI MAUAJI YANAYOHUSISHWA NA IMANI ZA KISHIRIKINA - MBEYA

Kamanga na Matukio | 03:22 | 0 comments
Diwani wa Kata ya Myunga,Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya mheshimiwa Godfrey Siame kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA)(kushoto),alipokuwa akimuonesha mpiga picha wetu moja ya kati ya makaburi saba yanayodaiwa kuwa waliozikwa waliuawa kwa imani za kishirikiana kisha kutolewa viungo vyao kama vile meno,sehemu za siri na Moyo pembezoni mwa Mto Momba.Hata hivyo zaidi ya watu watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo hawajakamatwa licha ya kufahamika.
Wananchi wa Kijiji cha Myunga,Kata ya Myunga Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya wakisikiliza kwa makini mkutano wa hadhara uliokuwa unajadili mauaji ya kutisha yanayohusishwa na imani za kishirikina,ambapo baadhi waliouawa walinyofolewa viungo vyao kama vile meno,sehemu za siri na moyo.
Mwenyekiti wa Kijij cha Myunga Bwana Satieli Sikanyika akielezea kero ya wa mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina.
 Diwani wa Kata ya Tunduma mheshimiwa Frank Mwakajoka(kushoto) akimkabidhi pesa zenye thamani zaidi ya shilingi 200,000 Diwani wa Kata ya Myunga mheshimiwa Godfrey Siame zilizochangwa na wananchi katika mkutano kwa ajili ya kusaidia familia za watu 13 waliokamatwa katika Kata ya Myunga Agosti 11 mwaka huu wakituhumiwa kuharibu mali za mfanyabiashara Bwana Benard Simundwe ambaye pia anatuhumiwa kujihusisha na mauaji katika Kijiji cha Myunga.
Diwani Mwakajoka(kushoto) na Diwani Siame(kulia) wakihesabu fedha zilizochangwa na wananchi katika harambee iliyofanyika papo hapo katika mkutano.
 Mzee Sadock Simwanza ambaye alishindwa kujizuia kutoa machozi kutokana na matukio ya mauaji yanayofanyika katika kijiji cha Myunga.
Wananchi wenye hasira kali walishindwa kujizuia na kuamua kulipiza kisasi,kutokana na mauaji yaliyokithiri na Polisi kutochukua hatua zozote licha ya kuwasilishwa kwa vielelezo zikiwemo silaha mbili,simu za mkononi,nguo za baadhi ya marehemu ambazo Polisi walizichukua na kuwaachia huru watuhumiwa,ambapo baadhi ya Majambazi wawili waliuawa na wananchi,ambao walitumwa kwa ajili ya kumuua Diwani wa Kata ya Myunga Siame.
 (Picha na Ezekiel Kamanga, Myunga,Momba).

KAMA WEWE NI MTANZANIA NA MPENDA HAKI SHARE HIZI PICHA KUPINGA UONEVU NA UNYANYASAJI WA HAKI ZA BINADAMU

Kamanga na Matukio | 01:24 | 0 comments

WANAMKE AJIFUNGUA KICHANGA NA KUKIZIKA

Kamanga na Matukio | 05:00 | 0 comments
Mwanamke mmoja Bi. Tabu Elias mkazi wa Kitongoji Nambalwe Shina la Mwilonga,Kata ya Magamba,Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya,amejifungua mtoto wa kike na kumzika muda mfupi baada ya kujifungua.

Tukio hilo limetokea Agosti 22 mwaka huu kijijini hapo majira ya saa 11:30 jioni,ambapo mwanakme huyo alimzika mtoto huyo chumbani katika nyumba anayoishi.

Bi Tabu ametenda ukatili huo wakati mumewe Bwana Gilbert Nzowa,alipokuwa kazini na ndipo aliporejea majira ya saa 12 jioni alimkuta mkewe akiwa hana ujauzito na kumuuliza mkewe kulikoni,ndipo alipomueleza kuwa amejifungua mtoto wa kike na kumzika.

Taarifa hiyo ilimkasirisha Bwana Gilbert na kuchukua jukumu la kutoa taarifa kwa Katibu wa Shina Bwana Juma Chakupewa Chapotea Mwabulambo ambapo aliongozana hadi eneo la tukio ambapo mwanamke huyo alikiri kutenda kosa hilo.

Aidha Katibu huyo aliamuru Bi Tabu kufukua shimo ambalo alimzika mtoto huyo na kulitekeleza agizo hilo ambapo baada ya kumaliza kufukua alikutwa mtoto huyo akiwa amevalishwa nguo mpya na tayari akiwa ameshafariki.

Baada ya kupatikana mtoto huyo,alipoulizwa kwanini ametenda kitendo hicho,mwanamke huyo alidai tumbo lake lilikuwa likimuuma kwa muda mrefu na hata alipojifungua hakufahamu kama kajifungua mtoto hai na ndipo alipoamua kumzika mumewe akiwa hayupo.

Bwana Mwabulambo alimchukua mwanamke huyo mpaka Ofisi ya Kitongoji na kisha kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kitongoji hicho Bwana Mapinduzi Kailote.

Kwa upande wake Bwana Kailote alisema suala hilo ni gumu kwake kwa hiyo haitakuwa rahisi kutolea maamuzi,ndipo walipoolekea katika Ofisi za Kijiji cha Magamba ili kupata taaribu za kutoa taarifa Kituo cha Polisi Galula.

Hata hivyo hivi karibuni inadaiwa kuwa Bi Tabu Elias alionekana kama mwenye matatizo ya akili.

MATUMIZI YA ARV MKOANI MBEYA YAMEKUWA YA HALI YA JUU.

Kamanga na Matukio | 03:32 | 0 comments
Na Bosco Nyambege ,Mbeya.
Mwitikio wa watu katika matumizi ya huduma ya ARV Mkoani Mbeya umebainika kuwa ni mkubwa.

Hayo ni kwamujibu wa kaimu mratibu wa kitengo cha UKIMWI mkoa wa Mbeya Dkt.Francis Philly alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jumatano hii.

Philly  amesema kuwa mwitikio wa wagonjwa wanaotumia dawa za ARV kuwa ni mkubwa kwani takwimu zinaonesha kuwa kuanzia June 2004 hadi June 2012 wagonjwa waliojiandikisha katika huduma ni 106598 ambapo watu wazima ni 92085 na watoto ni 12889.

Ameongeza kuwa kati ya hao walioanzishiwa dozi ya ARV ni 52903 ambapo watu wazima ni 40701 na watoto ni 12202 na watu 13163 hawajulikani kama wamekatisha dozi ama wameacha na katika hospitali ya mkoa wa mbeya watu 7675 wameandikashwa na 3539 wameanzishiwa tiba ya ARV na watu 1766 hawajulikani walipo na hali hii inaonesha wazi kuwa watu hawafuati maelekezo ya wataalamu wa afya .

Kwa takwimu hiyo inaonyesha kuwa zaidi ya 50%ya watu wote ambao wameandikishwa katika huduma CTC wameanzishiwa dawa.

Kwa upande wake Afisa muuguzi wa kitengo cha CTC katika Hospitali ya mkoa wa Mbeya Mariam Mhanjo amesema kuwa katika sekta hiyo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa vitendea kazi, upungufu wa wahudumu katika sekta hiyo,miundombinu mibovu hususani vijijini  pamoja na masilahi kuwa duni.

Hivyo Mhanjo ameiomba serikali kuweza kuwasaidia kutatua changamoto hizo   ili kuweza kufanya kazi katika mazingira mazuri na yanayorizisha.

AUAWA KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI - CHUNYA

Kamanga na Matukio | 03:31 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Mkazi wa Kijiji cha Mpona,Kata ya Matundasi,Wilayani Chunya Mkoani Mbeya Joseph  Mwazembe(36) ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya ujambazi.

Tukio hilo limetokea Agost 21 mwaka huu majira ya saa 2 usiku katika Kijiji cha Mkatang’ombe,Kata ya Totowe wilayani humo ambapo ilielezwa marehemu alikuwa na wenzake wawili walivamia Grocery ya Hassan Michael (36) mfanyabiashara wa Kijiji cha Mpona.

Aidha mara baada ya kuvamia walipora simu za mkononi 15 ambazo thamani yake haikuweza kufahamika mara moja na katika eneo la tukio kulikutwa risasi 5 za SMG na SR  na ganda moja  la risasi na panga alilokutwa nalo marehemu.

"Watu wawili ambao walidaiwa kuwa na marehemu walitoroka kwa kutumia pikipiki"alisema mmoja wa shuhuda ambaye hakutaka kutaja jina lake .

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa Diwani Athuman  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kutojichukulia sheria mikononi na kutoa ushirikino kwa jeshi la polisi kuwafichua waharifu wawili waliokimbia  na kuhusika katika tukio hilo.

Hata hivyo ameongeza kuwa kufuatia tukio hilo jeshi la polisi limeweka mikakati ili kuhakikisha  mtandao huo wa uharifu unapatikana ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Mwanafunzi afikwa na mauti baada ya kunywa sumu, Ajali ya Barabara yaua Mkoani Mbeya

Kamanga na Matukio | 05:44 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Watu wawili wamefariki dunia Mkoani Mbeya katika matukio mawili likiwemo la mwanafunzi kunywa sumu inayosadikika kuwa ni sumu ya panya,baada ya kufokewa na Bibi yake kwa kosa la kuchelewa kurudi nyumbani.

Tukio hilo limetokea Agosti 18 mwaka huu majira ya saa mbili usiku Shukrani Ndembo(18) mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Isange na Mkazi wa Kitongoji cha Ndamba,Kijiji cha Isange,Wilayani Rungwe amejikuta akipoteza uhai wake baada ya kunya sumu hiyo.

Sakata hilo lilianzia pale Bibi wa marehemu alipomtuma binti huyo dukani kununua mahitaji na kisha kuchelewa kurudi nyumbani na baada ya kuulizwa marehemu aliamua kuchukua sumu na kuinywa,ambapo hali yake ilikuwa mbaya na juhudi za kumkimbiza hospitalini zilifanyika lakini ziligonga ukuta baada ya marehemu kufikwa na mauti muda mfupi.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Lutengano Mwakyoma, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kisha kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha wilaya hiyo,ambapo walifika na kuthibitisha tukio hilo.

Hilo ni tukio la pili kutokea kwa wanafunzi wa shule mwaka huu,ambapo mwanzoni mwa mwaka mwanafunzi mwingine alifariki dunia baada ya kugundua kuwa ana ujauzito.
  
Aidha,mnamo majira ya saa 10 jioni Agosti 20 mwaka huu,katika Kijiji cha Ihanda,Wilayani Mbozi barabara ya Mbeya/Tunduma gari nambari T 466 BGF aina ya Toyota Coaster linalosafirisha abiria kutoka Mbeya mpaka Tunduma lilimgonga mtembea kwa miguu Moto Asha Mzumbwe(8) na kusababisha kifo papo hapo.

Hata hivyo chanzo cha ajali ya gari hilo lililokuwa likiendeshwa na dereva Bwana Michael Kasebele(56),mkazi wa Kalobe Jijini Mbeya,kimetajwa kuwa ni kuwa ni mwendokasi wa kupindukia.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Diwani Athuman amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na ametoa wito kwa wazazi kuchukua tahadhari ya kutowaacha watoto wao kurandaranda barabarani.

Tukio hilo nila kwanza tokea kuwekwa kwa matuta katika eneo la Ihanda,baada ya magari mengi kusababisha vifo vya mara kwa mara kwa wananchi wa eneo hilo,ambapo walifikia hatua ya kulichoma  moto gari ya abiria aina ya Coaster kutokana na mwendokasi.

MKURUGENZI AKIRI BARAZA KUFANYA MAKOSA YA KUWAKATA SHILINGI 200/= WAKULIMA - MBOZI

Kamanga na Matukio | 05:43 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Wananchi wa Tarafa  ya Itaka inayojumuisha kata ya Bala, Halungu, Itaka na Nambizo, wilayani Mbozi wamekataa kukatwa shilingi 200 toka kwenye mauzo yao ya kahawa kwa ajili ya kuchangia hisa ya uanzishwaji wa benki ya wananchi wa wilaya humo.

Katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika wilayani hapo uliazimia kila mkulima kukatwa shilingi 200 toka katika mauzo yao ya kahawa ambapo madiwani hao baadhi yao walionekena kutofautiana na kauli ya Charles Chenza, ambaye ni mwaandaji wa rasimu ya uanzishwaji wa benki ya wananchi wilaya ya Mbozi ambapo alisema kuwa kila mkulima wa zao hilo atakatwa kiasi hicho cha fedha ili kuchangia hisa ya benki hiyo.

Kufuatia kauli hiyo ya Chenza, wananchi tarafa hiyo waliamua kuitisha mkutano wa ndani agosti 18 mwaka huu katika kata ya Halungu ukihusisha madiwani toka kata zote za tarafa hiyo, na vikundi 24 vinavyohusika na ununuzi wa kahawa ambapo kwa pamoja walipinga kauli hiyo.

Wananchi hao walisema walifikia uamuzi huo wa kupinga kwa madai yakuwa hawakuwashirikishwa  katika kikao chochote na kukubaliana na maamuzi hayo kwani suala la ununuzi wa  hisa ni hiari ya mtu na kwamba walisema kuwa wao hawapingi kuanzishwa kwa benki hiyo.

Eribariki Msukwa, mkazi wa Nambizo, alisema kuwa wananchi wa wilaya hiyo wamekuwa wakionewa mara kwa mara kwa kukatwa fedha zao za mazao hususani zao la kahawa na fedha hizo kutokuwa na maelezo ya kutosha huku serikali ikishindwa kuwasaidia.

Alisema kuwa baada ya kikao hicho waliazimia kuunda kamati itakayokwenda kumuona mkuu wa wilaya hiyo Dr. Michael Kadeghe, mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas Kandoro na hatimaye kwenda Bodi ya Kahawa(TCB) Moshi ili kupinga kwa ukatwaji wa fedha hizo.

Aidha, walisema kuwa endapo itashindikana kupata msaada toka kwa viongozi hao wanaokusudia kuwafuata basi wataamua kwenda moja kwa moja mahakamani ili kudai haki yao.

Hata hivyo madiwani wa kata hizo kwa pamoja walionekana kupingana na kauli iliyotolewa na mwandaaji wa rasimu ya uanzishwaji wa benki hiyo,Charles Chenza ndani ya kikao hicho ambapo hata baada ya hapo madiwani hao waliweza kukaa na wanachi wao ili kuwapa taarifa na ambapo waliamua kwa pamoja kupinga suala hilo.

Madiwani hao ni pamoja na  Wiston Songa,toka kata ya Bara, Alan Mgula toka kata ya Itaka, Samson Simkoko toka kata ya Halungu,Bernad Mweniyonde wa kata ya Nambizo, na Salome Kibweja diwani viti maalum.

 Katika kamati hiyo walioteuliwa ni Eribariki Msukwa toka kata ya Nambizo, Cairo Msyete wa kata ya Bara, Taji Mwashambwa wa kata ya Itaka na Lewadi Sikaponda wa kata ya Halungu.
Wakati huohuo baada ya kumkosa Mkuu wa wilaya ya Mbozi,walimuona Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Bwana Levson Chileo amekiri kufanyika makosa hayo na hivyo amewataka wakulima hao kwenda Moshi Mkoani Kilimanjaro,kuiona bodi ya kahawa nchini TCB ILI kuzuia ukatwaji wa pesa hizo.
Wajumbe waliofanikiwa kuondoka ni pamoja na Bwana Eribariki Msukwa na Leward Sikaponda.
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger