Pages


Home » » WANANCHI WA MJI MDOGO WA MBALIZI, MBEYA VIJIJINI WAPATIWA MAJI KWA NJIA YA RELI, KUTOKANA NA UHABA WA MAJI.

WANANCHI WA MJI MDOGO WA MBALIZI, MBEYA VIJIJINI WAPATIWA MAJI KWA NJIA YA RELI, KUTOKANA NA UHABA WA MAJI.

Kamanga na Matukio | 04:40 | 0 comments

Wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi, wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya wakigombania foleni ya kuteka maji, yaliyobebwa kwenye Behewa la treni inayomilikiwa na Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) siku ya jana majira ya asubuhi kutokana na uhaba wa maji unaokabiri mji huo.

Wananchi waliofika eneo TAZARA huku wengine wakiwa wamepanga  foleni kwa ajili ya kupata maji ambapo Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) liliteka maji hayo kwa ajili ya wafanyakazi wake waliopo mji mdogo wa Mbalizi, wilaya ya Mbeya vijijini Mkoani Mbeya.
 Wananchi waliofika eneo TAZARA huku wengine wakiwa wamepanga  foleni kwa ajili ya kupata maji ambapo Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) liliteka maji hayo kwa ajili ya wafanyakazi wake waliopo mji mdogo wa Mbalizi, wilaya ya Mbeya vijijini Mkoani Mbeya.
*****
 Siku ya tatu toka hali ya utulivu kurejea mkoani Mbeya, hali imekuwa tete zaidi katika mji mdogo wa Mbalizi uliopo wilaya ya Mbeya Vijijini ambapo wananchi wanamtaka Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro kuchukua maamuzi mazito ya kuwarejeshea mradi wao wa maji ulioporwa na Vigogo wa Serikali.

Vikosi kadhaa vya kutuliza Ghasia (FFU) vilionekana jana katika viunga mbalimbali vya mji huo kwa ajili ya kuwatawanya wananchi baada ya Serikali kupata taarifa yakuwepo maandalizi ya maandamano ya kudai haki yao hiyo ambayo walisema Mkuu wa wilaya hiyo Evance Balama alishindwa kuitolea ufafanuzi katika mkutano uliofanyika Kijijini hapo hivi karibuni.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Mbalizi leo, wananchi ambao waliomba hifadhi ya majina yao walisema kuwa wanamuomba Mkuu wa mkoa wa Mbeya kuingilia kati shida ya maji inayoukabili mji huo ili kuwanusuru na hali mbaya ya ukosefu wa maji ambayo kwa sasa hununua lita 20 kwa Shilingi 1500 maji ambayo yanatoka Jijini Mbeya.

Wakati FFU wakiwa wanazunguka katika mji huo kuhakikisha hazitokei vurugu, wananchi kadhaa walionekana wakigombania matone ya maji yaliyokuwa yamepelekwa eneo la Tazara na Shirika la Tanzania na Zambia.

Kwa mujibu wa baadhi ya maafisa wa Tazara ambao walihojiwa na mtandao huu wamesema kuwa maji hayo ambayo yalikuwa ndani ya behewa moja la gari moshi(Treni) yalikuwa maalum kwa ajili ya familia za wafanyakazi wa Tazara wanaoishi katika Mji huo lakini wananchi baada ya kuona hivyo wakajikusanya na kuanza kuchota maji hayo.

Hali hiyo ilianza majira ya saa kumi jioni Novemba 13 mpaka jana majira ya saa Nne asubuhi ambapo maji yalikuwa yamekwisha lakini imeelezwa kuwa baada ya kuona hivyo Serikali imeamua kuwaangukia Tazara ili waendelee kuwapelekea maji wananchi hao ili kuinusuru Serikali kuingia katika vurugu na wananchi hao.

Novemba 9, mwaka huu wananchi hao walimtaka Rais Jakaya Kikwete kumfuta kazi haraka ama kumwondoa wilayani humo Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Juliana Malange kutokana na kushindwa kudhibiti genge la waporaji wa miradi ya wananchi.

 Hayo waliyasema katika mkutano wa hadhara uliokuwa umeitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo Evance Balama kwa nia ya kutatua kero ya maji ambayo wanatozwa  kwa amri Shilingi Elfu kumi na Mamlaka ya maji iliyopelekwa kinyemela na Serikali kijijini hapo huku kikao hicho kikishindwa kutoa majibu kwa wananchi.

Wananchi hao walimweleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa tatizo hilo limesababishwa na Mkurugenzi huyo ambaye amekiweka Kijiji hicho kama shamba la Bibi la kuchumia fedha bila kushirikiana na wananchi huku akitumia wapambe wake kupora miradi ya wananchi na kujimilikisha ukiwemo mradi huo.

Baadhi ya mabango hayo yaliandikwa ‘’Tumechoka na bili hewa, ,Hivi maji ni ya Minja na Mkurugenzi, Minja + Gadafi= na uuaji, Wazee wetu walichimba mitaro, Minja tupe maji yetu’’

Wananchi hao zaidi ya Elfu ishirini waliokusanyika katika viwanja vya mahubiri kutoa kero zao walimuuliza Mkuu huyo maswali zaidi ya ishirini ambayo yote hayakupatiwa majibu badala yake Mkuu huyo wa wilaya aliomba radhi kwa yale yote waliyotendewa wananchi kabla na baada ya kuhamishiwa yeye katika wilaya hiyo.

Naye Elia Kabholile alisema kuwa alishangaa kuona Mkurugenzi ameambatana na Mkuu wa wilaya wakati alikuwa ameitwa na wananchi akawapuuza kutokanana hulka yake ya kuwa na kiburi.

Baada ya hapo Mkuu wa wilaya alimwita Mkurugenzi wake Juliana Malange ili ajibu yale yanayomuhusu na shutuma alizokuwa akitupiwa ana kwa ana na wananchi hali iliyozua mtafaruku baada ya Mkurugenzi huyo kukataa kujibu shutuma zake akiwa juu ya jukwaa la meza.

Kutokana na hali hiyo huku wananchi wakimtaka apande katika meza iliyokuwa ikitumiwa na viongozi wenzake kujibu hoja na kuhoji ndipo akaanza kubembelezwa na viongozi wenzake huku akizomewa na wananchi wakisema kuwa amekuwa shalobalo hivyo aondoke.

Hali hiyo ilileta mzozo mkubwa, huku Mkuu wa wilaya hiyo akiamua kuchukua makarabrasha yake na kuondoka bila mkutano kufungwa huku wananchi wakiendelea kumzomea Mkurugenzi na kutaka kumpiga mawe Meneja wa maji Andason Minja waliyemwita ‘’Ninja’’ aliyekuwa amefishwa katika gari STK 7534 huku msafara huo ukiokolewa na Polisi waliokuwa wakiongozwa na Kamanda wa polisi wa wilaya hiyo Silvester Ibrahim.

Kutokana na ubabe huo wa baadhi ya watendaji wa Serikali ya wilaya hiyo kupora mradi wa maji, hivi karibuni wananchi wa Kijiji hicho walifunga ofisi za mamlaka hiyo ambayo mpaka sasa haijafunguliwa mpaka hapo mradi utakaporejeshwa mikononi mwa Serikali ya Kijiji.

Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger