Habari na Ezekiel Kamanga,Mbozi.
Wananchi
wa Kitongoji cha Njiapanda,Kijiji cha Msamba,Kata ya Nyimbili,Wilaya ya
Mbozi Mkoani Mbeya,walisusa kuzika maiti kwa takribani siku mbili na
nusu kwa kile kilichodaiwa kuwa mfiwa alikuwa hahudhurii misiba wenzie
kijijini hapo.
Hayo
yalibainishwa na mwandishi wa habari hii baada ya kufika kijijini
hapo,ambapo imedaiwa Bwana Samson Mwazembe(35),ambaye alifiwa na mwanae
aitwaye Hassan Samson(7) mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi
Chizumbi wilayani humo,aliyefariki siku ya Ijumaa Septemba 7 mwaka huu
majira ya saa 10 alfajiri.
Mtoto
huyo anadaiwa kufariki baada ya kuugua ugonjwa wa kuharisha kwa muda wa
siku tatu lakini hakufanikiwa kupelekwa hospitali kwa ajili ya
matibabu.
Baada
ya kifo hicho,kutokana na kasumba ya Bwana Mwazembe kutohudhuria katika
misiba kijiji hapo,aliamua kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi
cha wilaya hiyo ili kuomba msaada wa kusaidiwa kuzika mwanae,lakini
polisi walikataa na kumtaka arudi kijijini ili azungumze na wananchi.
Kufuatia
juhudi zake kugonga ukuta,aliamua kujifungia ndani ya nyumba yake na
ndipo mkewe aitwaye Bi.Daina Kananda(25),aliamua kwenda kumuona
Mwenyekiti wa kitongoji Bwana Eston Silomba ambapo alikwenda kwa
Mwenyekiti wa Kijiji Bwana Ikson Halihoka Sikaponda(48) kwa pamoja
walimtaka mfiwa azike mwenyewe kutokana na tabia yake ya kutohudhuria
misibani.
Aidha,baada
ya agizo hilo Bwana Mwazembe wakati akielekea tena katika Kituo cha
Polisi alikutana na kaka njia aitwaye Bwana Adam Mwazembe(55),na
alimwambia warudi kijijini na kuchukua jukumu la kuomba msamaha kwa
uongozi wa kijiji ili wamsamehe mdogo wake huyo,viongozi walikataa ombi
hilo na kumtaka mfiwa alipe jumla ya shilingi 460,000 ikiwa shilingi
400,000 kwa ajili ya kuchimba kaburi na shilingi 60,000 ya jeneza la
kumhifadhia marehemu.
Hata
hivyo mfiwa alikataa kulipa akidai kuwa hana fedha zozote ndipo maiti
ikabaki bila kuzikwa na asubuhi ya Jumamosi Septemba 8 mwaka huu,Bwana
Mwazembe alifanikiwa kupata shilingi 110,000 nakuomba uongozi upokee
fedha hizo lakini bado walikataa na kumweleza kuwa akachimbe kaburi
mwenyewe na kukabidhiwa vifaa vya kuchimbia lakini alishindwa na kubaki
akiangua kilio.
Septemba
9,mwaka huu siku ya Jumapili ndugu wa Bwana Mwazembe kwa pamoja
walimueleza auze mifugo wakiwemo mbuzi,nguruwe vilevile mazao(mahindi)
baada ya kuuza jumla ya shilingi 400,000 zilipatikana lakini wananchi
waliendelea kuwa na msimamo wakitaka zitimie shilingi 460,000,ndipo
Mwandishi wa habari hii alipowasihi wananchi wakubali kupokea pesa hizo
walikubali na kufanya mazishi majira ya saa 8 mchana.
Uchunguzi
umebaini kuwa mfiwa anatuhumiwa kujihusisha na imani za kishirikina
kwani mkewe alishawahi kujifungua watoto wawili na baadae kufariki kwa
nyakati tofauti na yeye kuwazika pasipo kutoa taarifa kijijini na baadhi
ya viungo kuvichukua na kuvipeleka kusikojulikana.
Wakati
huohuo Bwana Mwazembe,amedai sababu za kutohudhuria katika misiba ni
kutokana na kusisikia utofauti awapo msibani na ndiyo sababu ambayo
hupelekea kutohudhuria.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa kijiji Bwana Sikaponda amesema kuwa hilo ni
fundisho kwa mfiwa huyo na kwamba asirudie tena kitendo hicho na kwamba
kijiji hakitatoa msamaha tena bali watamtaka kuondoka kijijini hapo
kutokana na kutokuwa na ushirikiano.
Katika pesa zilizotolewa na mfiwa Bwana Mwazembe,shilingi 50 ilitumika kununulia vifaa vya kuchimbia kaburi kijijini hapo.
(Picha zaidi za tukio hili fuatilia mtandao huu)
0 comments:
Post a Comment