Na Gabriel Mbwille
Katika maisha yaliyo ya kawaida
tunafahamu kuwa kifo kinapotokea huwa kimepangwa na Mwenyezi Mungu, lakini pia
kwa wakati mwingine kifo husababishwa bila ridhaa ya mwenyezi Mungu, na ndio
maana kunakuwa na vyombo vya kisheria dhidi ya watu waliosababisha vifo katika
tawala mbalimbali zikiwemo za kimila, kidemokrasi na hata zile za kidikteta.
Katika vifo ambavyo kila mmoja
anaamini kuwa kimepangwa na Mwenyezi ni pamoja na kifo cha mtu kinachotokana na
maradhi mbalimbali ama ajali, lakini inapotokea mtu akafariki dunia kwa kupigwa
ama kuchinjwa na mtu mwingine jamii huamini kuwa kifo hicho si mpango wa Mungu
na ndio maana watu ama mtu anayehusika na kifo hicho hukamatwa na kufikishwa
kwenye vyombo vya dola ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.
Hata hivyo kutokana na utaratibu
huo bado jamii imekuwa ikijiuliza maswali mengi kuhusu hatua na maamuzi
yanayotolewa na vyombo vya dola dhidi ya watu wanaohusika kwa namna moja ama
nyingine na matukio ya mauaji hapa nchini hasa zaidi wakiwemo vigogo wa nchi na askari polisi wanaonekana kulindwa
zaidi kuliko raia wa kawaida.
Duniani kote, mara nyingi wahusika wa mauaji ya kisiasa ndio hubahatika
kufutiwa adhabu na kurejea uraiani. Adhabu ya kosa la kuua kwa kukusudia ni
kunyongwa hadi kufa. Mkuu wa nchi ndiye hutia saini kuidhinisha mtu
aliyehukumiwa kifo anyongwe, japo kutokana na kampeni ya asasi zinazopigania
kufutwa adhabu ya kifo, hukumu ya kifo imekuwa ikibatilishwa na kuwa kifungo
cha maisha jela.
Ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977
ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2005 inamruhusu Rais kutoa msamaha.
Ibara hiyo inatamka “Bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara
hii, Rais anaweza kutenda lolote ikiwamo kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa
mtu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu.”
Kama adhabu ya kuua kwa kukusudia
inasameheka, kwa nini Rais asiwasamehe mamia ya ‘wauaji’ walioko magerezani kwa
maana wameadhibiwa vya kutosha? Kama adhabu ya kuua kwa kukusudia inasameheka,
kwa nini Rais asiwasamehe wenye vifungo virefu vya makosa tena siyo ya kuua kama Nguza Viking na mtoto wake Papii Nguza?
Ushahidi uliotolewa wakati wa kesi hiyo ulionesha wazi Koplo Mswa na
konstebo Matiku walimuua Jenerali Kombe kwa kumpiga risasi baada ya kudhani
kwamba alikuwa mtuhumiwa sugu wa uhalifu.
Polisi hao walimkimbiza Jenerali Kombe aliyekuwa na mkewe. Alipoona hatari
Jenerali Kombe alinyanyua juu mikono kujisalimisha, lakini bado wauaji
wakamimina risasi kifuani na kumuua.
Mauaji hayo yalifanyika katikati ya uvumi kwamba Jenerali Kombe alikuwa
akikisaidia chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi ambacho mwenyekiti wake alikuwa
Augustine Lyatonga Mrema.
Hicho ndiyo kipindi ambacho Mrema alikuwa akilipua mabomu akifichua mipango,
mikakati na njama za serikali kuua upinzani.
Mazingira haya ndiyo yaliwafanya watu wahisi kwamba mauaji ya Jenerali Kombe
yalikuwa ya kisiasa. Ilihisiwa kwamba polisi hao hawawezi kusota jela miaka
mingi kwa vile walitumwa. Miaka 16 tangu Jenerali Kombe auawe mazingira
yanathibitisha hisia za watu – mauaji ya kisiasa!
Kwa nini wanaonufaika ni wanasiasa tu? Mwaka 1969 na 1983 wanasiasa na
wanajeshi waliokamatwa kwa tuhuma za kutaka kuipindua serikali ya Mwalimu
Nyerere wote waliachiwa huru baada ya mifumo ya kisiasa waliyopigania
kubadilika.
Waliokamatwa kwa tuhuma za uhaini mwaka 1969 ni pamoja na Bibi Titi
Mohammed, Waziri wa Kazi, Michael Kamaliza. Walihukumiwa kifungo cha maisha
jela lakini wakasamehewa mwaka 1972.
Mwaka 1983 vijana kadhaa wakiwemo kepteni Eugene Maganga, Suleiman Kamando,
Zakaria Hanspop, Vitalis Mapunda, Mbogolo, Kajaji Badru, Hatty MacGhee na
Christopher Kadego walikamatwa na wakatiwa hatiani mwaka 1985 kwa kula njama
kutaka kumpindua Nyerere.
Watuhumiwa hao walipewa kifungo cha maisha jela lakini baada ya kuanzishwa
mfumo wa vyama vingi mwaka 1991 waliachiwa huru mwaka 1995.
Juhudi za serikali kubatilisha adhabu ya kifo zilionekana kwa aliyekuwa mkuu
wa mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri. Mkuu wa mkoa huyo alichukua
bastola yake akaelekeza kwa dereva wa daladala, Hassan Mbonde akafyatua na
kumuua katika njiapanda ya Kawe na Bagamoyo.
Kortini wakasema Ditopile (sasa marehemu) ameua bila kukusudia kosa ambalo
mtuhumiwa anaweza kusamehewa au kupewa kifungo cha miaka kadhaa. Halafu akapewa
dhamana.
Koplo Mswa na Konstebo Matiku wako huru baada ya Mr Clean kutumia madaraka
aliyopewa kwa mujibu wa Katiba. Vema.
Lakini huenda ukajiuliza maswali mengi sana
je wafungwa wengine wa maisha wanapaswa kutimiza vigezo gani ili wafikiriwe
kusamehewa? Wawe maarufu? Wawe na ndugu wanaojua sheria? Wawe viongozi kama vile Ditopile? Wawe polisi? Ndiyo wawe polisi maana
hata polisi 13 waliofanya njama na kuua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa
madini kutoka Mahenge na dereva teksi mmoja mwaka 2006 waliachiwa huru eti kwa
kukosa ushahidi. Kikatiba si watu wote sawa mbele ya sheria?
Machi 2009 Deus Mallya alifunguliwa kesi ya kusababisha ajali iliyoua mjini Dodoma na akafungwa jela
miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia.
Kwanza ni kwa kuendesha gari kwa uzembe,
pili ni kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, na tatu
kuendesha gari bila leseni. Mallya hakupewa dhamana.
Mahakama ya Wilaya ya Singida, ilimhukumu dereva wa basi la kampuni ya
Adventure ya jijini Mwanza, Robert Willison (37), kifungo cha miaka 153 na miezi
sita jela baada ya kupatikana na makosa 49 tofauti likiwamo la kusababisha vifo
vya watu tisa mwaka 2008.
Robert alisomewa mashitaka matatu: la kwanza lilikuwa na makosa tisa ya
kusababisha vifo vya watu tisa; la pili makosa 36 ya kusababisha watu 36 kujeruhiwa
na shitaka la tatu lilikuwa na kosa moja la kuendesha basi bila leseni kutoka
mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam.
Lakini mahakama hiyohiyo ilimwachia huru dereva wa basi la kampuni ya
Mohamed Trans ya jijini Mwanza, Kharabu Jordan (43) ambaye alikabiliwa na
shitaka la kusababisha ajali iliyoteketeza abiria 25 kwa moto na kujeruhi
wengine kadhaa.
Mahakama ilidai ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka dhidi ya Jordan
ulikuwa dhaifu.
Katika kesi nyingine ya kigogo wa Serikali Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
ya Kinondoni-Kivukoni, Kwey Rusema alimtia hatiani aliyekuwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Andrew Chenge na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa
faini ya Sh. 700,000.
Makosa yaliyosababisha Chenge, ambaye awali alishitakiwa kwa mauaji na
baadaye kubadilishiwa mashitaka yakawa, atiwe hatiani ni kuendesha gari kwa
uzembe, kusababisha ajali iliyowaua Beatrice Constantine na Victoria George,
kuharibu mali
na kuendesha gari lisilo na bima. Hakimu alithibitisha kuwa Chenge alighushi
bima.
Tofauti na Mallya au dereva wa Mohamed Trans, Chenge ambaye ni Mbunge wa
Bariadi Magharibi na mwenyekiti wa nidhamu wa CCM, alipewa fursa ya kulipa
faini ya Sh. 700,000 hivyo akakwepa kifungo cha miaka mitatu jela.
Kushiriki katika uhalifu au kushiriki kupanga njama za kufanya uhalifu,
polisi wanasema ni kosa la jinai na mhusika anaweza kutiwa jela.
Lakini Jaji aliyesikiliza kesi ya kuuawa wafanyabiashara watatu wa Mahenge,
mkoani Morogoro, na dereva teksi mmoja mwaka 2006, alisema katika hukumu yake
kwamba aliyeua hajulikani, akawaachia polisi wote walioshiriki.
Katika tukio hilo,
wapo polisi walikiri kubeba vijana wale na kuwapeleka msitu wa Pande
walikouliwa, wapo walioshuhudia bunduki ikifyatuliwa, wapo waliochukua maiti
kupeleka Muhimbili – jaji hakuona ushiriki wao isipokuwa alitaka aliyeua.
Utetezi mkubwa wa wataalamu wa sheria ni kwamba watu wengi hawazijui sheria.
Je, hiyo ndiyo sababu ya kuwakomoa walalahoi kwa adhabu kali kwa kosa ambalo
mjuzi wa sheria anaachiwa huru?
Ukweli tatizo si wananchi kutojua sheria zilizopo, bali ni kukosekana
uadilifu, ujuzi makini, utashi wa majaji na mahakimu na kukithiri kwa rushwa
kunakosababisha mahakimu na majaji kutumia vifungu batili au kutoa tafsiri
iliyopinda ili kuwaridhisha mafisadi.
Hata mashtaka huandaliwa katika namna ya kukandamiza walalahoi na kuwaokoa
wakubwa.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Ukiwaona Ramadhani Ditopile Mzuzuri, baada
ya gari lake kugongwa na basi la abiria (DCM)
alishuka, akatoa bastola na kumtwanga risasi dereva na kumuua.
Polisi wa serikali wakafika kusoma hali, wakafikiria jinsi ya kumwokoa,
wakapima na kuandika ripoti.
Ripoti ikasomeka Ditopile aligongwa, akashuka kwenye gari lake kwa
bahati mbaya, akachukua bastola kwa bahati mbaya, akamgongea dirisha dereva wa
DCM kwa bahati mbaya, akamlenga na kumuua kwa bahati mbaya.
Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) aliposoma akafungua kesi ya kuua bila
kukusudia, na akapewa dhamana.
September 02, 2012 majira ya saa 10 za jioni mwandishi wa habari mwandamizi
wa kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa Daudi Mwangosi aliuawa kikatili na
chakushangaza ni jinsi, jeshi la polisi mkoani Iringa kutaka kuuficha ukweli
kuhusu kifo hicho na kutoa taarifa za awali kuwa, marehemu Mwangosi alifariki
dunia baada ya kupigwa na kitu kizito ambacho kilirushwa na kutoka kwa wafuasi
na viongozi wa Chadema.
Hata hivyo wakati akitoa jibu hilo
hakuwa na ufahamu kuwa wakati akiongea Watanzania wote walikuwa wamekwisha
fahamu kilichotendeka maeneo hayo ya Nyololo wilayani Mafinga kwa kupitia njia
ya mitandao ya kijamii baada ya moja ya wanahabari kupiga picha na kuziweka
kwenye mitandao hiyo.
Kutokana na maeneo hayo ya kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa kuhusu
taarifa za kwamba marehemu aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kutoka kwa
wafuasi wa CHADEMA je kamanda alikuwa na lengo gani hapo?Kila mtu anaweza
kujiuliza anavyoweza lakini ninachoweza kusema kuwa huenda Taifa likaingia
kwenye mvutano mkubwa na vyombo vya usalama kutokana na vyombo hivyo kutoa
kauli zake zenye utata mara kwa mara.
Pia tunaweza kujiuliza maswali mengi je ni kwanini basi mtuhumiwa wa mauaji
ya Mwangosi hakuweza kuchukuliwa hatua za haraka, na kwanini hatua ilichukuliwa
baada ya wananhabari hapa nchini kufanya maandamano ya kulaani vikali mauaji
hayo.Pia kunamasawali ambayo nadhani kila mtu huenda akawa anajiuliza kuhusu
kifo hicho na haki je itaweza kutendeka kwasababu siku ya ambayo mtuhumiwa
anafikishwa mahakamani alipelekwa huku akiwa kwenye gari la kifahari, la Land Cruiser,
polisi kuzuia kabisa, mtuhumiwa huyo, asipigwe picha na paparazi.
Vile vile, kitendo cha Kamuhanda kutoshtakiwa na kuendelea na kazi, wakati
inafahamika wazi kuwa yeye, ndiye aliyesimamia hiyo operesheni ya mauaji ya
Mwangosi unafikiri inaleta picha gani kwa watanzia ambao hivi wanaouelewa
mkubwa wa waya yanayoendelea hapa nchini?
Hata hivyo kutokana na tukio hilo waandishi mbalimbali mkoani Iringa
wamekuwa wakiwinda na baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa ni askari na kutishiwa
kuuawa hali iliyowalazimu baadhi yao kuamua kuandika ushahidi wao kwa maandishi
na kuuweka pia katika sauti ushahidi utakao saidia mahakama kutenda haki wakati
wa kutoa hukumu ya kesi hiyo.
Pamoja na hayo bado kuna wasiwasi mkubwa wa haki kutendeka baada ya hivi
karibuni KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi
kwa ajili ya kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari, marehemu Daudi Mwangosi,
kutukana na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwa mkoani Iringa kuibiwa Ipad
iliyokuwa na nyaraka muhimu za uchunguzi wa tukio hilo.
Baadhi ya wajumbe hao waliibiwa fedha na vifaa vya kazi vyenye thamani ya
mamilioni ya fedha kwenye hoteli waliyofikia, muda mfupi baada ya kuwasili
mjini hapa.
Wajumbe walioibiwa katika tukio hilo
ni pamoja na Theophil Makunga ambaye ameibiwa ipad, kamera na fedha taslimu
zaidi ya sh milioni moja.
Mwingine ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji Stephen Ihema ambaye naye
ameibiwa zaidi ya sh milioni moja na mjumbe mwingine ameibiwa sh 150,000.
Pamoja na hayo kamati hiyo ilionekana kuwa na hofu kubwa kutokana na
mazingira ya wizi na jinsi walivyoibiwa katika hoteli hiyo ya Ruaha
International.
Inaelezwa kwamba baada ya kuwasili na kupumzika kidogo katika vyumba vyao,
walipanga kwenda kupata chakula cha jioni.
Wakiwa nje wakisuburi chakula, mtu mmoja ambaye hajanaswa na polisi, kwa
kutumia funguo maalumu alifungua kwenye vyumba vya wajumbe hao na kuiba fedha
na vifaa hivyo.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanahoji kuwa ni kwa vipi mwizi huyo aliweza
kufungua vyumba hivyo tu na kuacha vingine.
Hoja ya msingi inayoweka njia panda wajumbe wa kamati hiyo ni juu ya
usalama, kwamba mwizi huyo ameweza kuingia kwenye vyumba vyao bila kukamatwa,
ni kwa vipi wanaweza kuwa na uhakika wa usalama wao?
Mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo aliliambia gazeti moja la kila siku kuwa
ni mara ya kwanza kwa wizi wa aina hiyo kutokea hotelini hapo.
“Nina muda mrefu hapa hotelini, sijaona wizi wa aina hii. Nadhani mwizi huyo
aliwafuatilia sana
wajumbe na alijipanga,” alisema mfanyakazi huyo.
Hata hivyo hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo na polisi wanaendelea na uchunguzi.
Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Mwakilishi wa Baraza la Habari
Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya
Mngulu.
Wajumbe hao wamepewa hadidu rejea yenye maswali sita ambayo ni kujua chanzo
cha kifo cha Mwangosi, iwapo kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa na
kama kweli kuna orodha ya waandishi watatu wa
kushughulikiwa mkoani Iringa.
Swali lingine ni kama nguvu zilizotumika zilistahili, kama
kuna utaratibu wa vyama vya siasa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa polisi na
kujua uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa ukoje.
Katika hatua nyinyine, hofu ya kutaka kumtorosha askari, Pasificus Cleophace
Simon, anayetuhumiwa kwa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha
Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Mbinu za kutaka kumtorosha askari huyo, namba G2573, zinadaiwa kufanywa na
baadhi ya askari wenzake wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa kushirikiana
na baadhi ya maofisa wa Polisi wanaodai kutoridhishwa na hatua ya kupandishwa
kizimbani kwa askari huyo pekee.
Mkakati wa askari waliozuia kwa kuwasukuma waandishi wa habari wasimpige
picha mtuhumiwa, huku akijifunika kitambaa usoni inatajwa kuwa moja ya mbinu
iliyopangwa ili mtuhumiwa asijulikane machoni kwa watu.
Siku moja baada ya askari huyo kupandishwa kizimbani, kulikuwa na mazungumzo
ya baadhi ya askari wa FFU waliokuwa katika ukumbi wa baa moja uliopo ndani ya
jengo la Iringa Net jirani na Benki ya Posta wakielezea mpango huo.
Askari hao wanne, waliokuwa wamevalia kiraia, katika mazungumzo yao walitoboa siri kubwa
ya kumnusuru askari mwenzao kwa kumtorosha nje ya nchi, vinginevyo kesi hiyo
itamuelemea.
Walisema kuwa wamejaribu kwa kila njia kufikiria jinsi ya kumnasua mwenzao,
mwisho wakakubaliana afikishwe mahakamani ili asomewe mashitaka yake kama kawaida, huku wakifanya mpango wa kumkimbiza nje ya
nchi halafu baada ya kufanikisha wataiambia mahakama mtuhumiwa ametoroka.
Wakati hayo yakizungumzwa ndani ya baa hiyo, mmoja wao alisema Mkuu wa Jeshi
la Polisi (IGP), Said Mwema, asingekubali askari huyo afikishwe mahakamani na
kuendelea kusota mahabusu, kwani wangekuwa tayari kulipuana ili kuhakikisha
mkuu huyo wa Jeshi la Polisi na viongozi wengine wa Polisi, wanakuwa miongoni
mwa watuhumiwa.
“IGP Mwema alitumia busara kufanya hivyo vinginevyo kule ndani
kusingekalika. Ungekuwa ni uonezi mkubwa kama mwenzetu atiwe gerezani wakati
alikuwa akitii amri yao
wenyewe.
“Inabidi ifanyike haraka iwezekanavyo ili hata Kamanda Kamuhanda aondoke
maana wananchi wameshapata hasira, usione wamekaa kimya ipo siku lolote
linaweza kutokea,” alisema mmoja wao.
Tuliongea na Mwema siku mbili ikaonekana Kamuhanda hawezi kukwepa kesi hiyo.
Hivyo tumepanga kumkimbizia nje ya nchi,” alisema mmoja wa askari polisi mkoani
humo.
“Hii kesi ina watu wengi na isingekuwa hii mbinu inayotaka kutumika
kumtorosha mtuhumiwa, Kamuhanda na wengine wasingepona kwa sababu yule kijana
hatakubali kutumikia jela peke yake wakati haukuwa uamuzi wake.
“Tulipanga kwamba wakati mtuhumiwa anafikishwa mahakamani askari
watakaomsindikiza wahakikishe wanamlinda kwa kila njia ili asipigwe picha
akajulikana sana,
kwani akijulikana hata huko atakakopelekwa anaweza kukamatwa tena. Si uliona
jinsi askari walivyofanya mahakamani kuzuia asipigwe picha?” kilisema chanzo
chetu cha habari.
Ilielezwa kuwa tayari mtuhumiwa huyo ametengenezewa cheti kingine cha
kuzaliwa chenye jina la Kacian Alphonce Mapila, huku akielezwa kuwa ni Mhehe
tofauti na kabila lake (Mhaya).
Kwa maelezo hayo kila mtu anaweza kuwa na fikra tofauti kuhusu ukweli wa
kesi hiyo na kuona namna ambavyo jeshi limekuwa likitumia kila njia kulindana
ili kukwepa aibu ya chombo hicho muhimu cha kusimamia usalama wa raia na mali
zake baada ya wao kuwa chanzo cha kupoteza maisha ya raia na uhalibifu wa mali
za mwananchi.
Kwa kesi hiyo huenda watu wakawa na mawazo hasi kwa wanahabari kuwa wanataka
kulikandamiza jeshi la polisi kwa kuwa mwenzao kauwa lakini vipi kuhusu vifo
vingine vya raia vinavyotokana na kupigwa na polisi, Mbeya mwanafunzi wa shule
ya sekondari Iyunga aliuawa mikononi mwa polisi, kwenye vurugu za Mwanjelwa
tumeona watu zaidi ya 6 wakijeruhiwa kwa kupigwa risasi na polisi, vurugu za
Tunduma raia mmoja aliuawa naye ambapo baadaye ilitoelewa taarifa kuwa alikuwa
akijaribu kuiba benki jambo ambalo si kweli na hivi karibuni mwanachama wa
CHADEMA aliuawa mkoani Morogoro.
Kutokana na hayo je haki itaweza kutendeka kweli?Vipi kuhusu maamuzi
yanayotolewa na viongozi, wanahabari na raia usalama wao uko wapi kunapotekea
mikutano ya kisiasa, na kwanini viongozi wa kuu wa wameshindwa kuzungumzia hilo?
Kwa maoni 0714-558777.
0 comments:
Post a Comment