Habari na Ester Macha,Mbeya.
Kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari
wa kituo cha Channel Ten Mkoani Iringa Bw. Daudi Mwangosi Umoja wa
klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) umeitaka serikali kuwasimamisha
kazi askari waliohusika katika tukio la mauaji ya kutisha ya mwandishi huyo.
Umoja huo umesema kuwa askari walioshiriki katika
oparesheni hiyo ambayo ni haramu wamesema serikali iwasimamishe kazi mara
moja ili kupisha uchunguzi kufanyika.
Hayo yalisemwa jana Jijini Dar Es Salaam
na Rais wa Umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Bw.Keneth
Simbaya wakati alipokuwa akitoa tamko la mauaji dhidi ya mwandishi
wa habari aliyeuwawa akiwa mikononi mwa polisi katika kijiji cha Nyololo
Wilayani Mufindi.
“Hapa tunataka uchunguzi huu ukikamilika
tunaitaka serikali kuutangazia umma na kupisha sheria kwa wale
watakaobainika kuhusika kwa uzembe huo kwa namna moja au nyingine
wachukuliwe hatua dhidi ya mauaji haya ya mwandishi wa habari Bw. Daudi Mwangosi”alisema.
Hata hivyo Bw. Simbaya alisema wakati uchunguzi
ukiwa unaendelea serikali iridhie na kurasimisha malipo
kwa ajili ya Mjane wa mwandishi huyo na watoto walioachwa na marehemu ili
waweze kujikimu.
Aidha alisema licha ya kutoa tamko hilo
wanaendelea kulitazamia jeshi la polisi kama mdau mwenye
shaka namna wanavyotenda kazi na waandishi wa habari mikoani
na kwamba watataarifu umma kuhusu mwenendo wao hapo baadae.
“Lakini pia katika mkutano huu tumeridhia
kushirikiana na taasisi zingine za haki za binadamu ,uwakili na
Utetezi ili kubaini namna bora ya kuistaki serikali kama mwenendo wa
suala hili hautakuwa unaleta tija hivyo tunakarisha mashirika
ya haki za binadamu ,asasi zisizokuwa za kiserikali ili kuweza kufanikisha azma
hii”alisema Bw. Simbaya.
Akizungumzia kuhusu usalama kwa waandishi wa
habari Bw. Simbaya alisema katika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari
wanafanya kazi yao kwa usalama amelitaka jeshi la polisi kutoa utaratibu
ambao utawezesha wanahabari nchini kufanya kazi kwa usalama
bila hofu wala dharau,kutoa elimu kwa jeshi la polisi kuhusu
umuhimu wa wanahabari na jukumu lao katika Taifa.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa Vyama vya
waandishi wa habari Tanzania ambao wanahudhulio mkutano mkuu wa umoja wa
clabu za waandishi wa habari Tanzania
walisema tamko hilo
halijapewa uzito kutokana na tukio la mauaji lenyewe jinsi lilivyo inatakiwa
kupewa uzito wa kina.
“Hili Tamko lilitakiwa kupewa uzito sana
kwani sisi tuliokuwepo katika msiba huo kwa ujumla inasikitisha sana
hivyo tamko ni muhimu lipewe uzito zaidi kulingana na mauaji yenyewe
yanavyotisha hivyo tufuate maamuzi ya viongozi wa clabu waliotoa matamko
ya kususia habari za polisi mpaka pale watakapokuwa wameridhia kukaa meza
moja na wanahabari juu ya mauaji hayo”alisema mmoja wa viongozi wa clabu
za waandishi wa habari Tanzania Bw. Christopher Nyenyembe.
0 comments:
Post a Comment