Pages


Home » » WATU WATATU WAFARIKI DUNIA.

WATU WATATU WAFARIKI DUNIA.

Kamanga na Matukio | 05:17 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Watu watatu wamefariki dunia katika matukio matatu tofauti Mkoani Mbeya,likiwemo la fundi seremala Furaha Msongole kudondoka juu ya paa la nyumba Mtaa wa Mwenge,Kata ya Vwawa Wilaya ya Mbozi.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 5 asubuhi Julai 17 mwaka huu,fundi huyo ambaye alidondoka wakati akipaua nyumba ya Mtumishi wa Halmashuri ya wilaya hiyo Bwana Moses Kibona.

Aidha,jitihada za kujaribu kuokoa uhai wake ziligonga mwamba baada ya kufikishwa katika Hospitali ya wilaya hiyo na kugundulika kuwa ameshafariki dunia.

Naye Mwenyekiti wa mtaa huo Bwana Michael Mwaipwisi,amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa tuio hilo.

Tukio la pili limetokea Mji mdogo wa Tunduma,Wilaya mpya ya Momba ambapo mtu au watu wasiofahamika walimpiga hadi kumuua Izzu Simkoko(25),mkazi wa Chapwa,Kitongoji cha Igawa Tunduma.

Mnamo Julai 17 mwaka huu majira ya saa 2:30 usiku mtu huyo anayesadikika kuwa ni mgonjwa wa akili alipopita eneo la Muungano Mwaka Tunduma,aliwakuta akina mama wakipika chakula na kupiga kelele za mwizi,kisha wakazi wa eneo hilo kuanza kumpiga mpaka kumsababishia kifo.

Mwili wake umehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha mji huo huku Polisi wakiendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo la kikatili.

Tukio la mwisho limetokea wilayani humo humo katika Kitongoji cha Luwemba,Kijiji cha Ikonya,Kata ya Bara lililohusisha ukuta wa nyumba kuanguka na kusababisha kifo cha mtoto wa kiume Hekima Sikitu Balanga(3) na kuwajeruhi wazazi wake.

Wazazi wa mtoto huyo aliyefariki ni Bwana Sikitu Balanga(35) na mkewe Roina Jeremiah ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mbozi Mission baada ya kujeruhiwa.

Hata hivyo Diwani wa Kata ya Bara Mheshimiwa Wiston Songa,amewataka wananchi kuamini hiyo ni ajali ya kawaida kutokana na uvumi kuenea kijijini hapo ya kudai kuwa tukio hilo limesababishwa na imani za kishirikina.

Wakati huo huo mazishi ya mtoto Hekima yamefanyika katika kijiji hicho,Mola azilaze roho za marehemu wote watatu mahali pema peponi.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger