Na Bosco Nyambege,Mbeya
Serikali
imeshauriwa kuwa na mikakati maalumu ya kuwaandaa Vijana katika misingi
ya kuyapenda masomo ya Sayansi kwa lengo la kuwa walimu watakaobobea
katika ufundishaji wa masomo hayo yatakayowasaidia wanafunzi kujitegemea
na siyo kutegemea ajira.
Wito
huo umetolewa na baadhi ya wakuu wa shule za sekondari mkoani Mbeya
wakati wa mahojiano maalum kuhusiana na uhaba wa walimu wa sayansi
mashuleni na kitu ambacho kinapelekea kukosa walimu wa masomo hayo.
Kwa
upande wake mwalimu mkuu wa Shule ya sekondari Regco iliyopo Jijini
Mbeya,Joshua Mwakitalima amesema kuwa ili kujenga kizazi ambacho
kitaweza kujitegemea na kupambana na maisha ni vema Serikali ikajikita
zaidi katika kuzalisha walimu vijana ambao pia watafundishwa mbinu za
kuwawezesha wanafunzi pindi watakapohitimu wajue jinsi ya kujitegemea.
Ameongeza
kuwa katika masomo yafundishwayo mashuleni, ni masomo ya Sayansi pekee
ndiyo yanaweza kumjengea msingi wa kujitegemea mwanafunzi pindi
amalizapo masomo yake bila kutegemea ajira.
Aidha
ameongeza kuwa hivi sasa Serikali ni kama inaelekea kuua masomo ya
sayansi kwa sababu wahitimu wengi ni masomo ya Art na kufanya idadi
kubwa ya walimu mashuleni kuwa wa masomo hayo tofauti na walimu wa
Sayansi.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Juma Iddi ambaye ndiye mwajiri
mkuu wa Halmashauri ya Jiji alipohojiwa kuhusu tatizo hilo alikiri
kuwepo na kuongeza kuwa hilo ni janga la kitaifa.
Iddi
amesema upungufu wa walimu wa sayansi limechangiwa sana na ongezeko la
shule nyingi za kata hivyo serikali imeshindwa kuendana na kasi hiyo
katika kuleta walimu wa sayansi ambao hata vyuoni ni wachache.
Ameongeza
kuwa Jiji la Mbeya linahitaji jumla ya walimu 412 kwa shule zote lakini
badala yake kuna walimu 215 hivyo kuwa na upungufu wa walimu 197 ambapo
amesema ni upungufu mkubwa na tatizo hilo linatakiwa lipewe kipaumbele.
Aliongeza
kuwa tatizo lingine linalosababisha upungufu wa walimu wa sayansi ni
kuwahamisha baadhi ya walimu wenye digrii kuwapeleka katika shule
zingine ili hali wenye diploma ni wachache na hawajitoshelezi.
Ametanabaisha
kuwa Halmashauri ya Jiji ina mpango wa kuongeza walimu wa sayansi
katika Mwaka wa fedha wa Mwaka 2012-2013 ambapo katika bajeti yao
wanatarajia kupata walimu 86 ambao pia hawataziba pengo la upungufu huo
kwa kuwa bado kuna shule zinaongezeka.
0 comments:
Post a Comment