Pages


Home » » SERIKALI YAOMBWA NA WAKULIMA NA WAFUGAJI KUFANYIA UCHUNGUZI MADINI YA KULAMBA NA MIFUGO.

SERIKALI YAOMBWA NA WAKULIMA NA WAFUGAJI KUFANYIA UCHUNGUZI MADINI YA KULAMBA NA MIFUGO.

Kamanga na Matukio | 03:18 | 0 comments
*Habari na Ester Macha,Mbeya.
Wakulima na Wafugaji wa Kijiji cha Itizi,wilaya ya Mbeya Vijijini wameiomba Serikali kufanya uchunguzi kuhusu aina ya madini yanayodaiwa kuchakachuliwa na hivyo kusababisha asilimia kubwa ya ng’ombe kutokuzaa kwa zaidi ya miaka miwili sasa licha ya mifugo hiyo kulamba madini,kupata joto na kupandishwa.

Wamesema kuwa wameshindwa kuendelea kujenga mitambo ya Biogesi kutokana na kuhofia mradi huo kumalizika mapema na kukosa ruzuku,inayotokana na mradi unaofadhiliwa na Programu ya uenezi wa mitambo ya biogesi ngazi ya Kaya Tanzania (TDBP) chini ya Camartec kwa wakulima wanaojenga.

Wakizungumza na gazeti hili wakazi wa kijiji cha Itizi Bw.Anyesile Mwasanga na Alex Elias walisema wamekuwa wakizingatia kanuni za ufugaji bora kama walivyofundishwa na kuendelea kusisitizwa na mtaalamu wao wa mifugo kwa kulisha vizuri na wengine kufikia hatua ya kukaa na dume la ng’ombe nyumbani kwa zaidi ya siku tatu kutegea kabla ya muda wa kupata joto na kupandisha lakini hakuna matokeo yeyeote ya kushika mimba.

Hata hivyo wamebainisha kuwa  wana hofu kubwa ya kufanyika hujuma ya uchakachuaji wa madini kama ya awali kwani jiwe la madini limekuwa likikatika ovyo wakati wa kulamba ng’ombe na kumeguka ovyo. 

‘Tunajuwa umuhimu wa kutunza na kufuga ng’ombe kwani wanatuletea faida kubwa ya maziwa,ndama na kupata fedha kwa ajili ya kujikimu kimaisha na tunazingatia maelekezo ya mtaalamu lakini jambo hili limetushtusha sana mfugaji kukaa na ng’ombe wawili tu kwa muda wa miaka sita hadi saba hawakamati mimba,"alisema.

Bw.Acley Sauzan,Adamu Malankali na Imanueli Anangisye walisema wamekuwa wakifuata ratiba ya kupata joto ndani ya siku 18 na wanapata joto kwa haraka na kumpandisha dume lakini ni zaidi ya miaka miwili hakuna matokeo yeyote ya kushika mimba jambo ambalo linawanyima raha na kuwakatisha tamaa ya kuendeela kufuga na hivyo wameiomba serikali na mamlaka zinazohusika kufuatilia suala hilo.

Kwa upande wake Ofisa ugani na msimamizi wa mradi Caritas Mbeya,Bw.Hansley Hansley alisema tatizo hilo kitaalamu linaweza kusababishwa na ukosefu wa madini ama kutozingatia ratiba ya kupandisha ng’ombe na kwamba upo umuhimu wa kukaa na wakulima kujaribu kuangalia chanzo cha tatizo sanjari na njia ya kuzuia na kutatua.

Mkurugenzi wa Caritas Mbeya  Bw,Edgar Mangasila ametoa mwito kwa wakulima kuchukuwa jukumu la kuwaita wataalamu mara kwa mara kuzungumzia masuala mbalimbali yanayowakabili mapema badala ya kusubiri kupatwa na tatizo.

"Waiteni wataalamu wa Halmashauri,caritas na wengine kuzungumzia masuala yenu mbalimbali na siyo kusubiri hadi mmepata tatizo kwani mtakuja kujikuta mmepata hasara kubwa,Ninyi ndiyo mabosi wa wataalamu na mashirika yanayowasaidia kwa hiyo waiteni siyo hadi waamue wenyewe kuja..haya mambo yanahitaji ushirikishwaji,"alisema.

Alisema wakulima wasitegemee ndama na maziwa pekee bali waangalie manufaa mengine yatokanayo na ng’ombe mathalani teknolojia mpya ya bayogesi kwa kujenga mitambo ya bayogesi sanjari na samadi ambayo inarutubisha ardhi na hivyo wakulima watajikuta wakisahau suala la Vocha za ruzuku na kuacha kufikiria maduka ya mbolea.

"Ukibaki na ndama na maziwa maumivu yake ni makali lakini ukiingia katika bayogesi itapunguza maumivu kwa sababu mama atapikia,watoto watasoma kwa ajili ya mwanga,utapata maziwa kidogo ya lishe na watoto, na kinyesi hicho hicho kitatumika kama dawa ya kuuwa wadudu  katika mboga mboga,"alisema.

Hata hivyo Mangasila amewaondoa hofu wakulima hao kuwa mradi wa bayogesi unaendelea kwa miaka mitatu na hivyo ametoa wito kwa wakulima kuchangamkia mradi huo mapema kwani kadri siku zinavyozidi kusonga mbele na gharama za ujenzi zinazdi kuongezeka.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger