Pages


Home » » SOKO LA SIDO MWANJELWA LAFUNGWA BAADA YA KIBANDA KIMOJA CHA MAMA NTILIE KUNUSURIKA KUTEKETEA KWA MOTO. MAMA NTILIE MBIONI KUFUNGULIWA MASHTAKA - MBEYA.

SOKO LA SIDO MWANJELWA LAFUNGWA BAADA YA KIBANDA KIMOJA CHA MAMA NTILIE KUNUSURIKA KUTEKETEA KWA MOTO. MAMA NTILIE MBIONI KUFUNGULIWA MASHTAKA - MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:39 | 0 comments
Sehemu ya Soko la Sido Mwanjelwa lililoteketea kwa moto Jijini Mbeya,mnamo Septemba 16 mwaka jana na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wa soko hilo.
*****
Na  Venance Matinya, Mbeya.
Halmashauri ya Jiji la Mbeya inatarajia kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara wa soko la Sido Mwanjelwa kutokana na kuhusishwa na vyanzo vya moto katika soko hilo mara kwa mara.
 
Baadhi ya wafanyabiashara hao ni wale wanaoshughulika na huduma za kupika na kuuza vyakula ndani ya soko hilo ambapo imedaiwa kuwepo na makubaliano kati ya viongozi na wafanyabiashara wa soko kutoruhusiwa kuwasha mkaa,sigala au moto na kutopika kitu chochote sokoni hapo.
 
Uongozi wa Jiji umesema watuhumiwa hao wamekiuka makubaliano na sheria ndogo ndogo zinazohusu soko hilo ambazo ni kifungu cha 12(1) cha mwaka 2011 ambacho kinakataza kujihusisha au kuwasha moto ndani ya soko hilo ili kuepuka majanga hayo.
 
Makamu Mwenyekiti wa soko la sido Bwana Wilson  Mwakisilwa alisema majanga hayo yamekuwa yakiliandama soko hilo tangu mwaka juzi ambapo wafanyabiashara wengi walipoteza mali zao na kusababisha waendelee kudaiwa kutoka katika taasisi za fedha.
 
Alisema hali hiyo inatosha na ndiyo sababu wameamua kuwafikisha mahakamani wale wote ambao wanakiuka makubaliano na kuendelea kusababisha hali ya hatari katika masoko na kusababisha wananchi kushindwa kufanya biashara zao kwa uhuru.
 
Mwakisilwa alisema wamefikia uamuzi huo baada ya juzi baadhi ya mama ntilie kuwasha moto na kusababisha kubanda kimoja kunusurika kuungua hali iliyosababisha taflani kubwa sokoni hapo na kuleta malumbano kati ya uongozi wa soko na wafanyabiashara.
 
“ Juzi jioni mama mmoja alikuwa akipika ndani ya kibanda na kusababisha moto kuwaka ingawa tulifanikiwa kuuzima lakini hawa akina mama  hawakuwa na lugha nzuri kwetu sisi na kusababisha tukose maelewano hali iliyotulazimu kwenda kwenye vyombo vya dola na hapa tumewakamata watu 9 waliohusika na hali hiyo” alisema Makamu Mwenyekiti huyo.
 
Aidha makamu mwenyekiti huyo aliwataja watu hao watakaofikishwa mahakamani kuwa ni Halima Benard, Lukia Kayuni, Maria Mwakamela,Elizabeth Sikwesi, Agnes Dominick, Rehema Musa, Beth Aron, Agatha Hussein na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Skauti.
 
Kwa upande wake baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo Michael Ashibaye na Lucia Silingwa waliwalalamikia mama ntilie kwa kutokuwa na uchungu wa mali wanazounguliwa hivyo kufikia hatua za kukaidi maagizo wanayokubaliana nayo.
 
Kamanda wa polisi wa wilaya ya Mbeya (OCD) Abraham Silvester alisema Uongozi wa Jiji wako tayari kuandaa hati ya mashtaka tayari kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao ambapo aliongeza kuwa watuhumiwa wote wanashikiriwa katika kituo cha kati cha polisi.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger