Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
MWALIMU
mkuu pamoja na uongozi wa Serikali ya Kitongoji cha Iyunga kata ya
Ilembo wanatuhumiwa na wananchi wao kutafuna fedha za michango ya
wananchi pamoja na zilizotolewa na serikali.
Watumishi hao wa umma
wanatuhumiwa kufuja fedha ambazo zilichangwa na wananchi kwa ajili ya
kusakafia vyumba vya madarasa ambazo ni shilingi Milioni 1,640,000/=.
Fedha zilizotolewa na
Serikali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu zinazodhaniwa kutafunwa
na viongozi hao ni shilingi Milioni tisa(9,000,000/=).
Mwalimu anayetajwa
kuhusika na skendo hiyo ni Mwalimu Ibrahimu Amosi ambaye alikuwa Mwalimu
mkuu katika Shule ya msingi Hazina ya kijijini hapo ambapo kufuatia
tuhuma hiyo Mwalimu huyo alihamishiwa katika shule ya Msingi Mbagala ya
kata ya Ilembo.
Kwa upande wa viongozi wa
Kitongoji wanaotuhumiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya shule ya
Hazina Allan Mbwiga,Mwenyekiti wa kitongoji Bonifasi Uledi, Stefano
Oswadi na Christina Richard ambao pamoja na ubadhilifu huo pia
hawajasoma mapato na matumizi kwa kipindi cha mwaka mzima.
Kutokana na ubadhilifu
huo Wananchi wamekatishwa tamaa na kuendelea kuchangia ujenzi wa shule
hali iliyopelekea wanafunzi kurundikana katika madarasa yaliyojaa vumbi
huku walimu wakikosa nyumba za kuishi.
Aidha wanafunzi hao wako
hatarini kupata magonjwa mbali mbali kutokana na vyumba hivyo kujaa
vumbi ambapo chumba kimoja kina wanafunzi zaidi ya 70 pia walimu ambao
hulazimika kutembea zaidi ya kilomita 4 kuifuata shule hiyo.
Hata hivyo Kufuatia
tuhuma hizo Katibu tawala msaidizi wa Wilaya ya Mbeya Geophrey Anania
alikiri kupokea tuhuma hizo na kuongeza kuwa tayari ametuma tume
kuchunguza tuhuma hizo.
Alisema tume hiyo
ikimaliza kazi hiyo atatoa taarifa kama kweli wamehusika na hatua
zitakazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa watakaohusika na tuhuma hizo
ambapo alisema muda wa tume hiyo ni mfupi kutokana na hali ya vyumba vya
madarasa ilivyo.
0 comments:
Post a Comment