Marehemu John Mwankenja aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiwira(CCM) na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe..
Watu wanne wamefikishwa katika
mahakama kuu kanda ya Mbeya wakituhumiwa
kumuua kwa maksudi John Mwankenja aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiwira(CCM) na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe..
Mwendesha mashtaka wa Serikali
Basilius Namkambe aliaambia Mahakama hiyo Mbele ya Jaji Samweli Karua kuwa
watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Mei 15,2011 katika Kijiji cha Mpandapanda
kata ya Kiwira Wilayani Rungwe kinyume na kifungu cha 196(16) kilichofanyiwa
marekebisho Mwaka 2002.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa
ni Hakimu Mwakalinga ambaye ndiye mtuhumiwa namba moja katika kesi hiyo akiwa
na Daudi Mwasipesya,Obote Mwanyimbili na Kelvin Maurus Myovela ambao
wanatuhumiwa kumuua John Mwankenja aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiwira(CCM) na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Awali baada ya kupandishwa
kizimbani watuhumiwa kujibu kesi inayowakabili yenye namba 31/2012 walimkataa
Wakili aliyejulikana kwa jina moja laMwakabubu aliyekuwa ameteuliwa kwa ajili
ya kuwatetea kwa madai kuwa hawana imani naye kutokana na mwenendo wa kesi
alizosimamia.
“Mtukufu Jaji kabla ya kesi
yetu haijaanza kusikilizwa tunaomba kubadilishiwa Wakili kwa sababu huyu Mwakabubu
hana uwezo na tumeona kesi ndogo tu anababaika na kesi yetu ni kubwa tunaona
wazi kabisa kuwa hataweza kututetea” alisema Mwakalinga Mshitakiwa namba moja.
Kufuatia ombi hilo Jaji Karua
alikubaliana nao ambapo alimteua Wakili mwingine ambaye ni Sambwee Shitambala
ambaye walimkubali kabla hajawaongezea wakili mwingine ili asaidiane na
Shitambala ambapo alimtaja Wakili Zakia Selemani.
Akisoma mashtaka yao Mwendesha
mashtaka wa Serikali Basilius Namkambe
aliiambia mahakama hiyo kuwa mnamo tarehe 19, Mei 2011 majira ya jioni
marehemu akiwa anatokea Mbeya mjini akirudinyumbani kwake Kiwira Wilayani
Rungwe alifika Nyumbani akiwa na gari lenye namba za usajili T 127ACZ Nissan
(Double cabin).
Namkambe aliongeza kuwa baada
ya kufika nyumbani kwake alipiga honi ya gari kwa ajili ya kuomba kufunguliwa
geti la mlango ambapo baada ya kusikia honi hiyo alitoka Mjomba wake ambaye
baada ya kumfungulia aliambiwa ashushe Kuku aliyokuwa amewabeba nyuma ya gari
yake.
Alisema kabla ya mjomba wa
Marehemu hajaanza kushusha kuku kwenye gari alitokea mshitakiwa namba moja
akiwa na siraha ambapo alimwamuru asifanye lolote ndipo akaanza kufyatua risasi
akimwelekezea marehemu kisha kumuuana kutoweka kusiko julikana.
Akijibu tuhuma hizo Wakili wa
Utetezi Shitambala na Zakia walikana washtakiwa hao kuhusika na matukio hayo
pamoja na baadhi ya vielelezo vilivyotolewa na upande wa mashtaka kuthibitisha
kuhusika kwa wateja wao.
Walisema mtuhumiwa wa kwanza
hakuwepo Wilayani Rungwe siku ya tukio ambapo walisema atakuwa na mashahidi
ambao watathibitisha kwamba hakuhusika ambao waliwataja kuwa ni pamoja na yeye mwenyewe,
Askari Magereza wawili wa gereza la Tukuyu Wilayani Rungwe waliotajwa kwa jina
moja moja la Hereda na Green.
Wengine ni Padeso Mwakipesile,
Aneth Siandene Kalinga na Jumanne Mwakisole huku washtakiwa namba mbili, tatu
na nne ambao hawatakuwa na mashahidi ambapo watasimama wao wenyewe kujitetea.
Namkambe aliiambai mahakama
hiyo kuwa upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi zaidi ya 15 ambao aliwataja
kuwa ni pamoja na Sofia Fungameza, Weston Gilbert,Magdalena Mgawe, Musa
Jackson, Issa Mwaipopo, Teresia Ludovick na Williamu Mtanga.
Wengine ni askari Polisi Mwenye
namba D2385 Sajent Michael wa Tukuyu, Inspekta Isaya Bwile wa Tukuyu, David
Paul kutoka makao makuu ya Polisi Dar Es Salaam, Twaha kutoka kitengo cha
Upelelezi makao makuu ya Polisi Dar Es Salaam, Haruna kutoka Polisi Tukuyu na
WP3433 Agnes wa polisi Tukuyu.
Namkambe aliwataja mashahidi
wengine katika kesi hiyo kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa upelezi (RCO) Mkoa
wa Mbeya aliyehamishiwa makao makuu SSP Anacletus Malindisa, John Mayunga na
Dk. D Z Matata kutoka ofisi ya Mkemia mkuu wa Serikali.
Jaji Karua aliahirisha kesi
hiyo hadi hapo itakapopangwa tena kwa ajili ya kuendelea na kuwasilikiza
mashahidi kutoka upande wa mashtaka baada ya kuambia mahakama kuwa upelelezi
umekamilika na mashahidi wote wako tayari.
0 comments:
Post a Comment