Pages


Home » » Uongozi wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey Jijini Mbeya walalamikiwa kutosikiliza kero na kutolea ufafanuzi,

Uongozi wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey Jijini Mbeya walalamikiwa kutosikiliza kero na kutolea ufafanuzi,

Kamanga na Matukio | 02:22 | 0 comments
Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey Jijini Mbeya.
 Na Venance Matinya, Mbeya.
Wanafunzi wanaosoma Chuo cha Uuguzi cha Aggrey kilichopo Sido Mwanjelwa Jijini Mbeya wameulalamikia uongozi wa Chuo hicho kwa kutosikiliza kero zao pamoja na kutotoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti wanafunzi hao wanaosomea fani za madawa(Clinical Medicine), meno (Dental), Maabara(Laboratory) na uuguzi(nursing) walisema baadhi ya kero ambazo hazitolewi majibu ya kueleweka ni pamoja na kusajili baadhi ya wanafunzi wasiokuwa na sifa.
Walisema baadhi ya wanafunzi waliosajiliwa katika chuo hicho ni ambao wana alama moja ya D ya ufaulu katika somo la Baiolojia katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha nne  wa taifa hali inayozua wasiwasi juu ya uwezo wa Wauguzi watakatolewa Chuoni hapo bila kuzingatia ufaulu wa masomo mengine kama Kemia na Fizikia.
Waliongeza kuwa mbali na hilo pia Chuo hicho hakina usaji wa kueleweka ambapo wao wanaoneshwa namba mbili ambazo zinasomoka 116 na 117 ambazo zimetolewa na Msajili wa Vyuo(Nacte) hali ambayo  wanadai kuwa itawasumbua katika mitihani yao ya mwisho.
Wanafunzi hao wa Mwaka wa Pili wapatao 120 walienda mbali zaidi kwa kudai kuwa  hata wanapoenda kwenye mafunzo ya Vitendo(Field) hupewa kazi ambazo hawajawahi kuzisoma katika mtaala hivyo kubaki wababaishaji na watazamaji tu bila kujua namna ya kufanya ambapo pia walidai kuwa hata wakiwa kwenye mazoezi hayo hakuna Mwalimu anayepita kufuatilia mwenendo wake.
Walisema katika utaratibu wa kufanya mazoezi ya vitendo wanafunzi walipaswa kupewa fedha za kujikimu ambazo ni Shilingi 150,000/= kwa kila mtu lakini tangu waanze Chuo hicho hawajawahi kupewa fedha hizo ambapo wakidai kwenye uongozi wanashindwa kupewa majibu ya kueleweka.
Kutokana na madai hayo wanafunzi hao wamejaribu kufanya mgomo na maandamano takribani mara mbili ili kushinikiza uongozi kuwapatia majibu ya kueleweka lakini juhudi zao zimekuwa zikigonga ukuta kutokana na jeshi la Polisi kuwahi eneo la tukio na kutuliza jitihada zao na kuendelea kutoa ahadi kuwa watarekebisha.
Februari 28, Mwaka huu, wanachuo hao walijaribu kufanya maandamano kushinikiza uongozi wa Chuo hicho kutolea ufafanuzi madai yote ya wanachuo ambapo uongozi huo uliwaahidi kurekebisha matatizo yote yaliyojitokeza lakini hali hiyo haikufanyika hadi yalipotokea maandamano mengine yaliyozimwa na jeshi la polisi.
Katika maandamano ya hivi karibuni wanafunzi hao walikuja na hoja mpya ambayo walidai kuwa tangu wanafunzi wa mwaka wa kwanza waanze masomo hawajapelekwa kwenye mafunzo ya vitendo kwa zaidi ya mwaka mmoja wakati ilitakiwa kabla yakufunga mwaka wawe wamesoma.
Akijibu tuhuma hizo Meneja wa Chuo hicho Kamugisha alisema Suala la usajili kuwa namba mbili linatokana na Wizara kutoangalia vizuri mtiririko wa usajili ambapo walitoa namba ya mbele na baadaye kujikuta namba moja imerukwa ambayo ni 117 badala ya 116 hivyo kusababisha utata huo.
Alisema kutokana na hilo waliamua kulifuatilia ambapo Wizara  yenyewe ilibaini kufanya makosa ambapo waliamua kuiondoa namba 117 na kuitaka Aggrey kutumia namba 116 ambayo hawajaifuta katika baadhi ya matangazo yao na kuongeza kuwa katika kuwaridhisha wanafunzi waliamua kutuma wanafunzi Wizarani ambao walileta majibu kwa wenzao.
Kuhusu kusajili wanafunzi wasio na sifa bado Meneja huyo alisema tatizo liko  Wizarani ambao wamekuwa wakibadilisha mitaala kila mara ambapo mara ya kwanza walitoa sifa kuwa anayetakiwa kujiunga na masomo ya uuguzi ni lazima awe na ufaulu wa alama ya D katika Somo la Baiolojia.
Aliongeza kuwa  mtindo huo umekuwa ukileta sintofahamu kwa wanafunzi ambao hawajaambiwa utaratibu huo hivyo kusababisha kudai maelezo ambayo baada ya kuambiwa wamekuwa wakisahau na kujikuta wakiendelea kuibua matatizo mengine.
Alienda mbali zaidi kuwa chanzo cha migogoro hiyo ni kutokana na baadhi ya wakufunzi kutuhumiwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi hali iliyosababisha uongozi wa Chuo kuwafukuza kazi jambo ambalo lilileta mvurugano chuoni hapo.
Aliongeza kuwa baada ya kutokea hali hiyo uongozi wa chuo ulilazimika kuwarudisha Wakufunzi hao kuendelea kufundisha licha ya kuonesha utovu wa nidhamu kazini  ambapo uongozi wa chuo umeshindwa kuchukua hatua yoyote.
Hata hivyo kufuatia uwepo wa kashfa hizo chuoni hapo baadhi ya wananchi na wadau wa Elimu wameitupia lawama chuo hicho kwa madai kuwa wanazalisha wauguzi wasiokuwa na sifa huku wakitolea mfano kwa sakata la daktari aliyewahi kumfanyia upasuaji wa Kichwa badala ya mguu.
Waliiomba Serikali kuingilia kati utaratibu wa chuo hicho ikiwa ni pamoja na kukagua sifa za wanafunzi waliojiunga na chuo hicho na wakufunzi waliopo hapo kama wanastahili kuendelea na kazi au kusimamishwa.
Walisema wanachojaribu kukitengeneza ni hatari kwa taifa na vizazi vijavyo kutokana na hatua wanazoenda nazo ambapo wanafunzi wanashindwa kufanya mazoezi ya vitendo na wakienda kufanya mazoezi hayo hushindwa kuendana na mazoezi kwa kile wanachodai kutofundishwa darasani.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii umebaini kuwa wanafunzi hao wanalipa ada ya Shilingi Milioni 1 na Laki mbili (1,200,000/=) kwa mwaka kiwango ambacho ni kikubwa kulingana na hali ya uchumi wa Watanzania wengi ilivyo sasa.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Chuo hicho Neema Mwambusi alipopigiwa kuhusiana na tuhuma za chuo hicho aliishia kujibu kuwa matatizo hayo yapo lakini yanapaswa kumalizwa kiubinadamu bila ya kuhofia uchumi wa wazazi na  kizazi kinachozalishwa kutokana na elimu inayotolewa chuoni hapo.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger