WAKATI baadhi ya Taasisi na mashirika binafsi
yanayojihusisha na kulea na kuhudumia watoto wenye ulemavu na kujikita zaidi
mijini na kusahau vijijini wamepewa wito wa kutembelea maeneo yote.
Mashirika hayo ambayo yamewasahau watoto walioko
vijijini wametakiwa kuwatembelea walemavu hao ambao hawajui sehemu ambayo
wanaweza kupata misaada ikiwemo mafuta ya kupaka kwa ajili ya kutunza ngozi zao
pamoja na miwani na kofia.
Mwito huo umetolewa baada ya kukutwa kwa watoto wenye
ulemavu wa ngozi ambao wanasoma katika shule za msingi huku wakiwa
wamechanganywa na watoto wengine ambao hawana matatizo.
Watoto hao wenye ulemavu wa ngozi(Albino)
wanaosoma katika shule ya Msingi Motomoto iliyoko katika Kata ya Ruiwa Wilaya
ya Mbarali Mkoani hapa walisema wamesahaulika katika kupatiwa misaada ambapo
wanaofaidi wako mijini tu.
Watoto hao waliokutwa nawaandishi wa habari
shuleni hapo huku wakiwa wamechanganywa na wanafunzi wengine katika darasa moja
huku wakiwa hawawezi kuendana na wenzao ambapo wamebainika kushindwa kusoma
wala kuandika kutokana nakukosa vifaa.
Aidha watoto hao walisema wanaiomba Serikali na
mamlaka inayohusika kuwahamisha na kuwatenganisha na wanafunzi wengine ili iwe
rahisi kwa wao kupewa misaada ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifunzia na mafuta
ya kupaka.
Walisema wamesahaulika kwa kiasi kikubwa kutokana
na kuchanganywa katika darasa moja ambapo inakuwa si rahisi kwa mwalimu
kuwaangalia kwa ukaribu na kujua kama kuna mahitaji mengine tofauti na watu
wengine ambao hawana uhitaji wa dawa na vifaa.
Baadhi ya watoto hao ambao wako darasa la kwanza
na darasa la tatu walikutwa wakitumia daftari za kawaida ili hali wanamatatizo
ya kuona mbali bila kuwa na vifaa kama miwani na kofia za kusaidia kuzuia na
kupunguza mwanga.
Mmoja wa walimu katika shule hiyo ambaye hakutaka
jina lake liandikwe kwa sababu ya kutokuwa msemaji wa tukio hilo alisema
tangu watoto hao waanze shule hiyo hawajawahi kupatiwa msaada wa aina yoyote.
Alisema hata namna ya ufundishaji wa watoto hao
unakuwa mgumu kutokana na kuchanganywa na watoto wengine katika darasa moja
ambapo Mwalimu inambidi kufundisha kwa ujumla bila kujali mahitaji ya mtu mmoja
mmoja.
Aidha aliwashukuru wazazi na walezi ambao
wamekuwa wakijitolea kuwahudumia watoto hao kwa kuwapeleka na kuwarudisha
shuleni ambapo pia aliwaomba wasamaria wema kujitolea kuwahamisha watoto hao
ili wakasome kwenye shule maalumu kutokana na hali mbaya ya hewa Wilayani
Mbarali.
Alisema hali ya hewa ya Mbarali ni joto ambalo
linawaathiri watoto hao hivyo amewaomba wasamaria wema kujitolea kwa
kuwahamisha na kuwatafutia shule maalumu ambazo zinamahitaji yote yanayotakiwa
kwa ajili ya walemavu wa ngozi ambao asilimia kubwa pia wanasumbuliwa na macho.
Picha na kamanga
|
0 comments:
Post a Comment