Na Ezekiel Kamanga, Mbeya..
RAISI
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
ametekeleza ahadi ya kuwawekea umeme wakazi wa kijiji cha Ilembo Wilaya
ya Mbeya Mkoani hapa.
Ahadi hiyo iliahidiwa na
Raisi katika kampeni ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 baada ya kupita
kijijini hapo na kukuta nguzo za umeme zikiwa zimesimikwa na kutelekezwa
bila kuendelezwa kwa muda wa miaka 8.
Umeme huo uliowashwa
mwezi uliopita umeonekana kuwafurahisha wakazi hao ambao bila kificho
walimpongeza raisi kwa kutekeleza ahadi hiyo ya umeme na kufanya kijiji
hicho kusahaulika kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi
wa habari kijijini hapo Mwenyekiti wa kijiji hicho Abeli Amon mbali na
kutoa pongezi kwa raisi kutokana na kutekeleza ahadi hiyo pia ametoa
wito kwa Shirika la Umeme Tanesco kusambaza nguzo nyingi kutokana na
mwitikio wa wananchi kuhitaji nishati hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema
kutokana na uwepo wa nishati hiyo shughuli za kiuchumi zimeongezeka kwa
kasi kubwa kutokana na wananchi kutumia nishati hiyo kuzalisha na
kufanya shughuli za kimaendeleo.
Alisema shirika la Umeme
Tanesco ni vema likapeleka miundombinu ya umeme katika kila kaya
kijijini hapo kutokana na utayari wa wananchi ambao walikuwa na hamu
kubwa ya kuona umeme ukiwaka kijijini hapo.
Alisema miaka nane ni
mingi sana tangu Tanesco wasimike nguzo lakini walishindwa kuendeleza
hadi hapo alipofika raisi na kusikia kilio chao na hatimaye
kuwatekelezea ahadi hiyo na kuwatimizia ahadi ya umeme.
Nao baadhi ya wananchi
walioongea na gazeti hili,wameiomba Wizara ya Afya kupitia Halmashauri
ya Wilaya ya Mbeya kuingiza umeme katika kituo cha afya cha Ilembo ili
usaidie katika kurahisisha huduma.
" Wizara husika ni vema
ikaingiza umeme katika kituo cha afya ili kusaidia katika huduma za
upasuaji na wakati wa kujifungua kwa akina mama" alisema Shizya Halinga
mkazi wa kijiji hicho.
Naye Benard Shusa alisema
uwepo wa umeme utasaidia uhifadhi wa mazingira kwa wananchi kuacha
kukata miti ovyo kwa ajili ya nishati na badala yake watatumia umeme kwa
kazi mbali mbali.
Aliongeza kuwa wananchi
walikuwa wakiharibu mazingira kutokana na kukata miti ambayo walikuwa
wakitumia kuchoma mkaa na shughuli zingine kama za kupikia ambapo sasa
wanaweza kununua majiko ya umeme ili kurahisisha huduma hiyo.
0 comments:
Post a Comment