Pages


Home » » HABARI KAMILI KUHUSIANA NA AJALIILIYOTOKEA MKOANI MBEYA

HABARI KAMILI KUHUSIANA NA AJALIILIYOTOKEA MKOANI MBEYA

Kamanga na Matukio | 02:05 | 0 comments
BAADHI YA MAJERUHI WAKIFIKISHWA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA
Godfrey Kahango, Mbeya.
Jinamizi la ajali Mkoani Mbeya limeendelea kumaliza roho za watu, ambapo watu  sita wamepoteza maisha  na wengine 10 wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea eneo la Itewe kata ya Inyala wilaya ya Mbeya Vijijini.

Tukio hilo lilitokea jana saa 4:00 asubuhi ambapo ajali hiyo ilihusisha gari ya abiria  aina ya Hiace yenye namba za usajili T245 AMH iliyokuwa ikitokea Jijini Mbeya kwenda Chimala wilayani Mbarali na lori  aina ya FAW lenye namba za usajili T 276 ATQ  lenye  tela namba T 655 AUP lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda nchi jirani ya Congo lililokuwa likendeshwa na dereva aliyetambuliwa kwa jina la Geofrey Msoma.

Katika ajali hiyo watu watano walifariki papo hapo na mmoja alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ambako walikokimbizwa majeruhi wote.

Akithibitisha  kupokea miili ya marehemu waliofariki katika ajali hiyo  na majeruhi hao afisa  Muuguzi wa  kitengo cha huduma  ya haraka Jenny Kapeye,  katika hospitali hiyo ya Rufaa,alisema kuwa walipokea miili ya marehemu watano ambao walifariki katika eneo la tukio huku mmoja alifariki akiwa anapatiwa huduma hospitalini hapo.

Aliwataja watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Steven Kimario, (Mchaga) Shalfa Abdalah, Simon Mwakalikwa (66), Andrea Simbeye (47), Mariam Mwanginde  na mwanaume mwingine ambaye hakufahamika jina lake mara moja ambapo miili hiyo imefadhiwa katika hospitali hiyo ya Rufaa.

Pia aliwataja majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kuwa ni 10 ambapo kati yao saba walitibiwa na kuruhusiwa huku watatu ambao ni Elia Malowe (18), Charles Gumani (53), Doto Tagala (44) wakiwa wamelazwa wodi namba moja.

Aidha, uchunguzi wa awali kwa dereva wa lori hilo ulibaini kwamba alikuwa akiendesha gari huku akiwa amelewa pombe  aina ya konyagi ambayo ilikutwa ndani ya gari hilo huku dereva huyo akitaka kupigana na wananchi waliofika katika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada wa awali kabla ya kufika kwa askari wa usalama wa barabarani.

Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya, Diwani Athumani amethibishwa kutokea kwa ajali hiyo ambapo alisema kuwa  dereva  wa lori anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger