Pages


Home » » WANANCHI KUKATA TAMAA YA KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO NI CHANZO CHA KUDORORA KWA UJENZI WA HOSTELI SHULE ZA SEKONDARI.

WANANCHI KUKATA TAMAA YA KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO NI CHANZO CHA KUDORORA KWA UJENZI WA HOSTELI SHULE ZA SEKONDARI.

Kamanga na Matukio | 06:04 | 0 comments
Na Esther Macha, Mbeya
Imeelezwa kuwa sababu za kudorora kwa ujenzi wa hosteli za wanafunzi katika shule za sekondari  Mkoani Mbeya, ni wananchi kukata tamaa ya kuchangia shughuli za maendeleo kutokana na kutosomewa taarifa za mapato na matumizi.


Hayo yalisemwa na Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bw.Modestus Dickson Kilufi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri wa Mkoa(RCC) kilichofanyika jijini mbeya.


Bw. Kilufi alitoa kauli hiyo baada ya taarifa ya elimu ya mkoa wa Mbeya iliyowasilishwa ndani ya kikao hicho  na Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda, kuonyesha kuwa shule ya sekondari ya Madibira yenye kidato cha tano na sita iko hatarini kufungwa kutokana  kukosa hosteli, hali inayosababisha wanafunzi kulala madarasani.


Alisema kuwa suala la wananchi kususia kujitoa katika kuchangia maendeleo hususani ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanafunzi  Mkoani hapo unatokana na utendaji na usimamizi mbovu wa viongozi wanaohusika kwa kutowasomea mapato na matumizi huku kukiwa hakuna jambo lolote linaloendelea baada ya kutoa michango yao.


Akitolea Mfano wa Shule ya Sekondari ya Rujewa Mbunge huyo alisema kuwa wananchi walijitoa kimasomaso kuchangia ujenzi wa madarasa ya kidato cha tano na sita muda mrefu lakini  tangu wachangie michango hiyo hadi hakuna linaloendelea hadi sasa  jambo ambalo alidai kuwa linachangia wananchi hao kukata tama ya kuchangia.


“Naomba ieleweke wazi kwamba wananchi siyo kusema kuwa hawataki kuchangia  maendeleo ya ujenzi wa Hostel, tatizo lililopo ni kwamba wananchi wamekuwa wakichanga michango yao lakini wamekuwa hawasomewi mapato na matumizi huku kukiwa hakuna ujenzi wowote unaokuwa ukiendelea” alisema na kuongeza.


“Wananchi wapo tayari kuchangia maendeleo hayo lakini sumu iliyopo  ni hiyo ya kutosomewa mapato ya matumizi ya michango yao, na kwamba hata kama wananchi hao ni wajinga kiasi gani kwa hilo hawata kuwa tayari kuendelea kujitoa kwa nguvu zao huku wasijue fedha zao zinakwenda wapi”alisema Mbunge huyo.


Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bi.Hilda Ngoye alihoji uhalali wa kufunguliwa kwa shule hiyo ya Madibira wilayani Mbarali, wakati sera ya taifa ya elimu inaelekeza kuwa shule yenye kidato cha tano na sita ili  ifunguliwe kigezo cha kwanza ni kuwepo kwa hosteli kwa wanafunzi wote.


Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw.Abbas Kandoro alionyesha kushtushwa na hoja hiyo na kuhoji kazi za kamati za maendeleo ya kata, pamoja na kuagiza wakuu wote wa wilaya Mkoani  hapo kufuatilia na kuhakikisha taarifa za mapato na matumizi zinasomwa katika kila kijiji na yeye (Kandoro), kupewa nakala za taarifa hizo.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger