Pages


WAKUNGA WA JADI WAZALISHA WANAWAKE WAJAWAZITO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU - CHUNYA,

Kamanga na Matukio | 05:35 | 0 comments
Na Ezekiel Kamanga, Chunya.
Wakunga wa jadi wawili wanaofanya shughuli ya kuwazalisha wanawake wajawazito katika Kata ya Totowe,Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wamewaokoa wanawake wengi,licha ya kukabiliwa  na Chnamoto mbalimbali katika ufanikishaji wa fani hiyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi.

Mmoja wa wakungunga anayefahamika kwa jina la Bi.Hilda Said Kawinga(80),amesema mpaka sasa amewazalisha wajawazito 55 mwaka huu na walipokelewa kwake siku mojakbalya yakujifungua na hakuna kifo chochote kilichowahi kutokea  na kuorodhesha katika Daftari  lake na ilimlazimu kufanya hivyo ili kuisaidia Serikali kupata takwimu endapo zitahitajika,

Amesema kuma kuwa changamoto aliyonayo ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya studio kama vile mkasi,vyombo vya kuhifadhia maji,kitanda na godoro ambapo amesema kwa wastani hupokea zawadi ya wajawazito 10 kwa mwezi na hakuna tozo kwa huduma hiyo mara baada ya kujifungua.

Kwa upande wake Mkunga mwingine Bi, Agripina Fredrtick Sikanyika (37) maarufu kama Mama Namwinji,amesema imemlazimu kuwaachia nyumba wagonjwa wanaofika kwa ajili ya kujisubiria kutokana na mfululizo wa wagonjwa hao wanaofika kwake kupata huduma hiyo huku akiacha nyumba nyingine kwa ajili ya kujifungulia.

Mkunga huyo amesema alianza huduma hiyo tangu mwaka 2000 na mwaka 2011 alizalisha wajawazito 114 na mwaka huu wajawazito 187 na kwamba kati ya hao watoto wawili walizaliwa wakiwa na ulemavu wa aina yake.

Mnamo Septemba 15 mwaka huu mwanamke mmoja alijifungua mtoto mwenye sikio moja, mguu mmoja, mdomo na pua vikiwa vimeungana ma mtoto huyo alifariki muda mfupi baada ya kujifungua.

Aidha Septemba 16 mwaka huu pia alizaliwa mtoto aliyekuwa na kichwa mithili ya ng'ombe  na kiwiliwili cha binadamu.

Mbali na matukio hayo mawili ya aina yake,mkunga amesema kuwa yeye hatozi tozo yoyote licha ya kazi ngumu ambayo amekuwa akiifanya usiku na mchana huku ukiwepo uhaba wa kitanda cha kujifungulia wajawazito kwani huwalaza chini na kukabiliwa na magonjwa hasa kipindi cha masika.

Aidha Bi Agripina amesema kuwa hufuata taratibi zote za kuwapokea wajawazito hao kwa kuzikagua kadi za kliniki  na kuzijaza pindi wakijifungua.

Mbali na hilo mkunga huyo pia hupokea wajawazito ambao wanatakiwa kufanyiwa oparesheni/upasuaji na kwake hujifungua salama bila upasuaji wowote na kubainisha kuwa mmoja wa wajawazito alifanyiwa upasuaji kama mara mbili hospitalini lakini alipopelekwa kwake alijifungua watoto wawili salama katika nyakati tofauti.

Hata hivyo Bi Agripina ametoa wito kwa serikali kuwasaidia wakunga kutokana na kufanya kazi hizo ngumu ambazo zingefanywa hospitalini na pia amesikitishwa na kitendo cha Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbuyuni kumtoza shilingi laki mbili kwa kile alichodai kuwa ni kifo cha mama mjamzito na stakabadhi ya malipo kutopewa.

ACHARANGWA MAPANGA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA, MWINGINE AUAWA KWA KUPIGWA NONDO.

Kamanga na Matukio | 05:34 | 0 comments
Na Ezekiel Kamanga,Mbeya
Ajuza mwenye umri wa miaka 80 aliyefahamika kwa jina la Bi. Janeth Nenje, amenusurika kifo baada ya kucharangwa na mapanga na mtu aliyefahamika kwa jina la Pato Lwiza Mkazi wa Kitongoji cha Chang'ombe,Kijiji cha Mbuyuni Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea kijijini hapo Septemba 19 mwaka huu majira ya saa mbili usiku ambapo mtuhumiwa alimfuata ajuza huyo nyumbani kwake na kuanza kumcharanga kwa mapanga na kisha kumjeruhi vibaya hali iliyopelekea kukimbizwa katika Kituo cha Afya kilichopo kijijini hapo.

Imedaiwa kuwa siku za hivi karibuni mtuhumiwa Bwana Lwiza alimtuhumu ajuza huyo kuwa ni mshirikina hali iliyomfanya kuingiwa na hasira na kumtendea ukatili huo sehemu mbalimbali za mwili wake.

Aidha Bi. Nenje hivi sasa amelazwa katika kituo hicho cha afya cha Mbuyuni na hali inaendelea vema.

Baada ya msako mkali wananchi walifanikiwa kumkamata Bwana Lwiza na kuanza kumsulubu kabla ya kuokolewa na Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Mwashiuya kwa kushirikiana na Mgambo wa Kijij hicho kabla ya kukabidhiwa mikononi mwa polisi wa Kituo cha Mkwajuni.

Katika tukio jingine Mwananchi mmoja Mkazi wa Kijiji cha Lulasi,Kata ya Mpombo Wilaya ya Rungwe Mkoani hapa ameuawa na mtu au watu wasiuofahamika kisha kutumbukizwa katika Kisima cha Maji safi kinachomilikiwa na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.

Tukio hilo limegunduliwa na wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wakiteka maji katika kisima hicho na kubaini harufu kali katika maji hayo yanayotumika katika matumizi ya nyumbani kama vile kunywa,kupikia na kufulia.

Hali ilizidi kuwa mbaya Septemba 22 mwaka huu majira ya saa 8 mchana baada ya wananchi kadhaa waliokuwa wakiteka maji hayo kuambua kukivunja kisima hicho kinachomilikiwa na Bwana Noah Mwambalaswa na kuukuta mwili wa marehemu ukiwqa kichwa chini miguu juu,hivyo taarifa kutolewa kwa viongozi wa kijiji hicho.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Jimmy Mwalupaso amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo Daktari wa Hospitali ya Wilaya hiyo alifika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi  mwili wa marehemu  na kubaini kuwa alipingwa na kitu kizito(nondo) kichwani hali iliyompelea marehemu kuvuja damu nyingi mpaka mauti yalipomfika.

Hata hivyo baada ya uchunguzi wa daktari mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika kijijini hapo Septemba 23 mwaka huu.

MAKALA

Kamanga na Matukio | 05:33 | 0 comments
Na Gabriel Mbwille
Katika maisha yaliyo ya kawaida tunafahamu kuwa kifo kinapotokea huwa kimepangwa na Mwenyezi Mungu, lakini pia kwa wakati mwingine kifo husababishwa bila ridhaa ya mwenyezi Mungu, na ndio maana kunakuwa na vyombo vya kisheria dhidi ya watu waliosababisha vifo katika tawala mbalimbali zikiwemo za kimila, kidemokrasi na hata zile za kidikteta.

Katika vifo ambavyo kila mmoja anaamini kuwa kimepangwa na Mwenyezi ni pamoja na kifo cha mtu kinachotokana na maradhi mbalimbali ama ajali, lakini inapotokea mtu akafariki dunia kwa kupigwa ama kuchinjwa na mtu mwingine jamii huamini kuwa kifo hicho si mpango wa Mungu na ndio maana watu ama mtu anayehusika na kifo hicho hukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.

Hata hivyo kutokana na utaratibu huo bado jamii imekuwa ikijiuliza maswali mengi kuhusu hatua na maamuzi yanayotolewa na vyombo vya dola dhidi ya watu wanaohusika kwa namna moja ama nyingine na matukio ya mauaji hapa nchini hasa zaidi wakiwemo vigogo wa  nchi na askari polisi wanaonekana kulindwa zaidi kuliko raia wa kawaida.

Duniani kote, mara nyingi wahusika wa mauaji ya kisiasa ndio hubahatika kufutiwa adhabu na kurejea uraiani. Adhabu ya kosa la kuua kwa kukusudia ni kunyongwa hadi kufa. Mkuu wa nchi ndiye hutia saini kuidhinisha mtu aliyehukumiwa kifo anyongwe, japo kutokana na kampeni ya asasi zinazopigania kufutwa adhabu ya kifo, hukumu ya kifo imekuwa ikibatilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela.

Ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2005 inamruhusu Rais kutoa msamaha.

Ibara hiyo inatamka “Bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii, Rais anaweza kutenda lolote ikiwamo kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu.”

Kama adhabu ya kuua kwa kukusudia inasameheka, kwa nini Rais asiwasamehe mamia ya ‘wauaji’ walioko magerezani kwa maana wameadhibiwa vya kutosha? Kama adhabu ya kuua kwa kukusudia inasameheka, kwa nini Rais asiwasamehe wenye vifungo virefu vya makosa tena siyo ya kuua kama Nguza Viking na mtoto wake Papii Nguza?

Ushahidi uliotolewa wakati wa kesi hiyo ulionesha wazi Koplo Mswa na konstebo Matiku walimuua Jenerali Kombe kwa kumpiga risasi baada ya kudhani kwamba alikuwa mtuhumiwa sugu wa uhalifu.

Polisi hao walimkimbiza Jenerali Kombe aliyekuwa na mkewe. Alipoona hatari Jenerali Kombe alinyanyua juu mikono kujisalimisha, lakini bado wauaji wakamimina risasi kifuani na kumuua.

Mauaji hayo yalifanyika katikati ya uvumi kwamba Jenerali Kombe alikuwa akikisaidia chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi ambacho mwenyekiti wake alikuwa Augustine Lyatonga Mrema.

Hicho ndiyo kipindi ambacho Mrema alikuwa akilipua mabomu akifichua mipango, mikakati na njama za serikali kuua upinzani.

Mazingira haya ndiyo yaliwafanya watu wahisi kwamba mauaji ya Jenerali Kombe yalikuwa ya kisiasa. Ilihisiwa kwamba polisi hao hawawezi kusota jela miaka mingi kwa vile walitumwa. Miaka 16 tangu Jenerali Kombe auawe mazingira yanathibitisha hisia za watu – mauaji ya kisiasa!

Kwa nini wanaonufaika ni wanasiasa tu? Mwaka 1969  na 1983 wanasiasa na wanajeshi waliokamatwa kwa tuhuma za kutaka kuipindua serikali ya Mwalimu Nyerere wote waliachiwa huru baada ya mifumo ya kisiasa waliyopigania kubadilika.

Waliokamatwa kwa tuhuma za uhaini mwaka 1969 ni pamoja na Bibi Titi Mohammed, Waziri wa Kazi, Michael Kamaliza. Walihukumiwa kifungo cha maisha jela lakini wakasamehewa mwaka 1972.

Mwaka 1983 vijana kadhaa wakiwemo kepteni Eugene Maganga, Suleiman Kamando, Zakaria Hanspop, Vitalis Mapunda, Mbogolo, Kajaji Badru, Hatty MacGhee na Christopher Kadego walikamatwa na wakatiwa hatiani mwaka 1985 kwa kula njama kutaka kumpindua Nyerere.

Watuhumiwa hao walipewa kifungo cha maisha jela lakini baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991 waliachiwa huru mwaka 1995.

Juhudi za serikali kubatilisha adhabu ya kifo zilionekana kwa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri. Mkuu wa mkoa huyo alichukua bastola yake akaelekeza kwa dereva wa daladala, Hassan Mbonde akafyatua na kumuua katika njiapanda ya Kawe na Bagamoyo.

Kortini wakasema Ditopile (sasa marehemu) ameua bila kukusudia kosa ambalo mtuhumiwa anaweza kusamehewa au kupewa kifungo cha miaka kadhaa. Halafu akapewa dhamana.

Koplo Mswa na Konstebo Matiku wako huru baada ya Mr Clean kutumia madaraka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba. Vema.

Lakini huenda ukajiuliza maswali mengi sana je wafungwa wengine wa maisha wanapaswa kutimiza vigezo gani ili wafikiriwe kusamehewa? Wawe maarufu? Wawe na ndugu wanaojua sheria? Wawe viongozi kama vile Ditopile? Wawe polisi? Ndiyo wawe polisi maana hata polisi 13 waliofanya njama na kuua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge na dereva teksi mmoja mwaka 2006 waliachiwa huru eti kwa kukosa ushahidi. Kikatiba si watu wote sawa mbele ya sheria?
Machi 2009 Deus Mallya alifunguliwa kesi ya kusababisha ajali iliyoua mjini Dodoma na akafungwa jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia.

Kwanza ni kwa kuendesha gari kwa uzembe, pili ni kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, na tatu kuendesha gari bila leseni. Mallya hakupewa dhamana.

Mahakama ya Wilaya ya Singida, ilimhukumu dereva wa basi la kampuni ya Adventure ya jijini Mwanza, Robert Willison (37), kifungo cha miaka 153 na miezi sita jela baada ya kupatikana na makosa 49 tofauti likiwamo la kusababisha vifo vya watu tisa mwaka 2008.

Robert alisomewa mashitaka matatu: la kwanza lilikuwa na makosa tisa ya kusababisha vifo vya watu tisa; la pili makosa 36 ya kusababisha watu 36 kujeruhiwa na shitaka la tatu lilikuwa na kosa moja la kuendesha basi bila leseni kutoka mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam.

Lakini mahakama hiyohiyo ilimwachia huru dereva wa basi la kampuni ya Mohamed Trans ya jijini Mwanza, Kharabu Jordan (43) ambaye alikabiliwa na shitaka la kusababisha ajali iliyoteketeza abiria 25 kwa moto na kujeruhi wengine kadhaa.

Mahakama ilidai ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka dhidi ya Jordan ulikuwa dhaifu.
Katika kesi nyingine ya kigogo wa Serikali Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kinondoni-Kivukoni, Kwey Rusema alimtia hatiani aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh. 700,000.

Makosa yaliyosababisha Chenge, ambaye awali alishitakiwa kwa mauaji na baadaye kubadilishiwa mashitaka yakawa, atiwe hatiani ni kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha ajali iliyowaua Beatrice Constantine na Victoria George, kuharibu mali na kuendesha gari lisilo na bima. Hakimu alithibitisha kuwa Chenge alighushi bima.

Tofauti na Mallya au dereva wa Mohamed Trans, Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi na mwenyekiti wa nidhamu wa CCM, alipewa fursa ya kulipa faini ya Sh. 700,000 hivyo akakwepa kifungo cha miaka mitatu jela.

Kushiriki katika uhalifu au kushiriki kupanga njama za kufanya uhalifu, polisi wanasema ni kosa la jinai na mhusika anaweza kutiwa jela.

Lakini Jaji aliyesikiliza kesi ya kuuawa wafanyabiashara watatu wa Mahenge, mkoani Morogoro, na dereva teksi mmoja mwaka 2006, alisema katika hukumu yake kwamba aliyeua hajulikani, akawaachia polisi wote walioshiriki.

Katika tukio hilo, wapo polisi walikiri kubeba vijana wale na kuwapeleka msitu wa Pande walikouliwa, wapo walioshuhudia bunduki ikifyatuliwa, wapo waliochukua maiti kupeleka Muhimbili – jaji hakuona ushiriki wao isipokuwa alitaka aliyeua.

Utetezi mkubwa wa wataalamu wa sheria ni kwamba watu wengi hawazijui sheria. Je, hiyo ndiyo sababu ya kuwakomoa walalahoi kwa adhabu kali kwa kosa ambalo mjuzi wa sheria anaachiwa huru?
Ukweli tatizo si wananchi kutojua sheria zilizopo, bali ni kukosekana uadilifu, ujuzi makini, utashi wa majaji na mahakimu na kukithiri kwa rushwa kunakosababisha mahakimu na majaji kutumia vifungu batili au kutoa tafsiri iliyopinda ili kuwaridhisha mafisadi.

Hata mashtaka huandaliwa katika namna ya kukandamiza walalahoi na kuwaokoa wakubwa.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Ukiwaona Ramadhani Ditopile Mzuzuri, baada ya gari lake kugongwa na basi la abiria (DCM) alishuka, akatoa bastola na kumtwanga risasi dereva na kumuua.

Polisi wa serikali wakafika kusoma hali, wakafikiria jinsi ya kumwokoa, wakapima na kuandika ripoti.
Ripoti ikasomeka Ditopile aligongwa, akashuka kwenye gari lake kwa bahati mbaya, akachukua bastola kwa bahati mbaya, akamgongea dirisha dereva wa DCM kwa bahati mbaya, akamlenga na kumuua kwa bahati mbaya.

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) aliposoma akafungua kesi ya kuua bila kukusudia, na akapewa dhamana. 

September 02, 2012 majira ya saa 10 za jioni mwandishi wa habari mwandamizi wa kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa Daudi Mwangosi aliuawa kikatili na chakushangaza ni jinsi, jeshi la polisi mkoani Iringa kutaka kuuficha ukweli kuhusu kifo hicho na kutoa taarifa za awali kuwa, marehemu Mwangosi alifariki dunia baada ya kupigwa na kitu kizito ambacho kilirushwa na kutoka kwa wafuasi na viongozi wa Chadema.

Hata hivyo wakati akitoa jibu hilo hakuwa na ufahamu kuwa wakati akiongea Watanzania wote walikuwa wamekwisha fahamu kilichotendeka maeneo hayo ya Nyololo wilayani Mafinga kwa kupitia njia ya mitandao ya kijamii baada ya moja ya wanahabari kupiga picha na kuziweka kwenye mitandao hiyo.

Kutokana na maeneo hayo ya kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa kuhusu taarifa za kwamba marehemu aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kutoka kwa wafuasi wa CHADEMA je kamanda alikuwa na lengo gani hapo?Kila mtu anaweza kujiuliza anavyoweza lakini ninachoweza kusema kuwa huenda Taifa likaingia kwenye mvutano mkubwa na vyombo vya usalama kutokana na vyombo hivyo kutoa kauli zake zenye utata mara kwa mara.

Pia tunaweza kujiuliza maswali mengi je ni kwanini basi mtuhumiwa wa mauaji ya Mwangosi hakuweza kuchukuliwa hatua za haraka, na kwanini hatua ilichukuliwa baada ya wananhabari hapa nchini kufanya maandamano ya kulaani vikali mauaji hayo.Pia kunamasawali ambayo nadhani kila mtu huenda akawa anajiuliza kuhusu kifo hicho na haki je itaweza kutendeka kwasababu siku ya ambayo mtuhumiwa anafikishwa mahakamani alipelekwa huku akiwa  kwenye gari la kifahari, la Land Cruiser, polisi kuzuia kabisa, mtuhumiwa huyo, asipigwe picha na paparazi. 

Vile vile, kitendo cha Kamuhanda kutoshtakiwa na kuendelea na kazi, wakati inafahamika wazi kuwa yeye, ndiye aliyesimamia hiyo operesheni ya mauaji ya Mwangosi unafikiri inaleta picha gani kwa watanzia ambao hivi wanaouelewa mkubwa wa waya yanayoendelea hapa nchini?

Hata hivyo kutokana na tukio hilo waandishi mbalimbali mkoani Iringa wamekuwa wakiwinda na baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa ni askari na kutishiwa kuuawa hali iliyowalazimu baadhi yao kuamua kuandika ushahidi wao kwa maandishi na kuuweka pia katika sauti ushahidi utakao saidia mahakama kutenda haki wakati wa kutoa hukumu ya kesi hiyo.

Pamoja na hayo bado kuna wasiwasi mkubwa wa haki kutendeka baada ya hivi karibuni KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari, marehemu Daudi Mwangosi, kutukana na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwa mkoani Iringa kuibiwa Ipad iliyokuwa na nyaraka muhimu za uchunguzi wa tukio hilo.

Baadhi ya wajumbe hao waliibiwa fedha na vifaa vya kazi vyenye thamani ya mamilioni ya fedha kwenye hoteli waliyofikia, muda mfupi baada ya kuwasili mjini hapa.

Wajumbe walioibiwa katika tukio hilo ni pamoja na Theophil Makunga ambaye ameibiwa ipad, kamera na fedha taslimu zaidi ya sh milioni moja.

Mwingine ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji Stephen Ihema ambaye naye ameibiwa zaidi ya sh milioni moja na mjumbe mwingine ameibiwa sh 150,000.

Pamoja na hayo kamati hiyo ilionekana kuwa na hofu kubwa kutokana na mazingira ya wizi na jinsi walivyoibiwa katika hoteli hiyo ya Ruaha International.

Inaelezwa kwamba baada ya kuwasili na kupumzika kidogo katika vyumba vyao, walipanga kwenda kupata chakula cha jioni.

Wakiwa nje wakisuburi chakula, mtu mmoja ambaye hajanaswa na polisi, kwa kutumia funguo maalumu alifungua kwenye vyumba vya wajumbe hao na kuiba fedha na vifaa hivyo.

Wadadisi wa mambo ya siasa wanahoji kuwa ni kwa vipi mwizi huyo aliweza kufungua vyumba hivyo tu na kuacha vingine.

Hoja ya msingi inayoweka njia panda wajumbe wa kamati hiyo ni juu ya usalama, kwamba mwizi huyo ameweza kuingia kwenye vyumba vyao bila kukamatwa, ni kwa vipi wanaweza kuwa na uhakika wa usalama wao?

Mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo aliliambia gazeti moja la kila siku kuwa ni mara ya kwanza kwa wizi wa aina hiyo kutokea hotelini hapo.

“Nina muda mrefu hapa hotelini, sijaona wizi wa aina hii. Nadhani mwizi huyo aliwafuatilia sana wajumbe na alijipanga,” alisema mfanyakazi huyo.

Hata hivyo hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo na polisi wanaendelea na uchunguzi.
Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu.

Wajumbe hao wamepewa hadidu rejea yenye maswali sita ambayo ni kujua chanzo cha kifo cha Mwangosi, iwapo kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa na kama kweli kuna orodha ya waandishi watatu wa kushughulikiwa mkoani Iringa.

Swali lingine ni kama nguvu zilizotumika zilistahili, kama kuna utaratibu wa vyama vya siasa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa polisi na kujua uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa ukoje.

Katika hatua nyinyine, hofu ya kutaka kumtorosha askari, Pasificus Cleophace Simon, anayetuhumiwa kwa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Mbinu za kutaka kumtorosha askari huyo, namba G2573, zinadaiwa kufanywa na baadhi ya askari wenzake wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Polisi wanaodai kutoridhishwa na hatua ya kupandishwa kizimbani kwa askari huyo pekee.

Mkakati wa askari waliozuia kwa kuwasukuma waandishi wa habari wasimpige picha mtuhumiwa, huku akijifunika kitambaa usoni inatajwa kuwa moja ya mbinu iliyopangwa ili mtuhumiwa asijulikane machoni kwa watu.

Siku moja baada ya askari huyo kupandishwa kizimbani, kulikuwa na mazungumzo ya baadhi ya askari wa FFU waliokuwa katika ukumbi wa baa moja uliopo ndani ya jengo la Iringa Net jirani na Benki ya Posta wakielezea mpango huo.

Askari hao wanne, waliokuwa wamevalia kiraia, katika mazungumzo yao walitoboa siri kubwa ya kumnusuru askari mwenzao kwa kumtorosha nje ya nchi, vinginevyo kesi hiyo itamuelemea.
Walisema kuwa wamejaribu kwa kila njia kufikiria jinsi ya kumnasua mwenzao, mwisho wakakubaliana afikishwe mahakamani ili asomewe mashitaka yake kama kawaida, huku wakifanya mpango wa kumkimbiza nje ya nchi halafu baada ya kufanikisha wataiambia mahakama mtuhumiwa ametoroka.

Wakati hayo yakizungumzwa ndani ya baa hiyo, mmoja wao alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, asingekubali askari huyo afikishwe mahakamani na kuendelea kusota mahabusu, kwani wangekuwa tayari kulipuana ili kuhakikisha mkuu huyo wa Jeshi la Polisi na viongozi wengine wa Polisi, wanakuwa miongoni mwa watuhumiwa.

“IGP Mwema alitumia busara kufanya hivyo vinginevyo kule ndani kusingekalika. Ungekuwa ni uonezi mkubwa kama mwenzetu atiwe gerezani wakati alikuwa akitii amri yao wenyewe.

“Inabidi ifanyike haraka iwezekanavyo ili hata Kamanda Kamuhanda aondoke maana wananchi wameshapata hasira, usione wamekaa kimya ipo siku lolote linaweza kutokea,” alisema mmoja wao.
Tuliongea na Mwema siku mbili ikaonekana Kamuhanda hawezi kukwepa kesi hiyo. Hivyo tumepanga kumkimbizia nje ya nchi,” alisema mmoja wa askari polisi mkoani humo.

“Hii kesi ina watu wengi na isingekuwa hii mbinu inayotaka kutumika kumtorosha mtuhumiwa, Kamuhanda na wengine wasingepona kwa sababu yule kijana hatakubali kutumikia jela peke yake wakati haukuwa uamuzi wake.

“Tulipanga kwamba wakati mtuhumiwa anafikishwa mahakamani askari watakaomsindikiza wahakikishe wanamlinda kwa kila njia ili asipigwe picha akajulikana sana, kwani akijulikana hata huko atakakopelekwa anaweza kukamatwa tena. Si uliona jinsi askari walivyofanya mahakamani kuzuia asipigwe picha?” kilisema chanzo chetu cha habari.

Ilielezwa kuwa tayari mtuhumiwa huyo ametengenezewa cheti kingine cha kuzaliwa chenye jina la Kacian Alphonce Mapila, huku akielezwa kuwa ni Mhehe tofauti na kabila lake (Mhaya).

Kwa maelezo hayo kila mtu anaweza kuwa na fikra tofauti kuhusu ukweli wa kesi hiyo na kuona namna ambavyo jeshi limekuwa likitumia kila njia kulindana ili kukwepa aibu ya chombo hicho muhimu cha kusimamia usalama wa raia na mali zake baada ya wao kuwa chanzo cha kupoteza maisha ya raia na uhalibifu wa mali za mwananchi.

Kwa kesi hiyo huenda watu wakawa na mawazo hasi kwa wanahabari kuwa wanataka kulikandamiza jeshi la polisi kwa kuwa mwenzao kauwa lakini vipi kuhusu vifo vingine vya raia vinavyotokana na kupigwa na polisi, Mbeya mwanafunzi wa shule ya sekondari Iyunga aliuawa mikononi mwa polisi, kwenye vurugu za Mwanjelwa tumeona watu zaidi ya 6 wakijeruhiwa kwa kupigwa risasi na polisi, vurugu za Tunduma raia mmoja aliuawa naye ambapo baadaye ilitoelewa taarifa kuwa alikuwa akijaribu kuiba benki jambo ambalo si kweli na hivi karibuni mwanachama wa CHADEMA aliuawa mkoani Morogoro.

Kutokana na hayo je haki itaweza kutendeka kweli?Vipi kuhusu maamuzi yanayotolewa na viongozi, wanahabari na raia usalama wao uko wapi kunapotekea mikutano ya kisiasa, na kwanini viongozi wa kuu wa wameshindwa kuzungumzia hilo?
Kwa maoni 0714-558777.

KUSHUKA KWA UWAJIBIKAJI NA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI WA IDARA MBALIMBALI

Kamanga na Matukio | 05:32 | 0 comments
Na Gabriel Mbwille, Mbeya.
Imedaiwa kushuka kwa uwajibikaji na utendaji kazi wa watumishi wa idara mbalimbali hapa nchini vikiwemo vyombo vya habari kukosa maadili kunatokana na mfumo mbovu wa elimu ya hapa nchini.

Hayo yalisemwa na waandishi wa habari mkoani Mbeya wakati wa mafunzo ya uandishi wa habari kwa njia za mtandao ambayo yameandaliwa na umoja wa klabu za wa andishi wa nchini  (UTPC) yaliyofanyika katika ukumbi wa hospitali ya mkoa Mbeya.

Walisema kuwa hivi sasa kumekuwa na tabia ya ajira kutolewa kwa kuangalia kigezo cha elimu pekee pasipo kuangalia ujuzi na uzoefu wa mfanyakazi kikazi na kimazingira haliinayopelekea kuajiliwa kwa watu waio na ufahamu wowote wa kile wanachokifanyia kazi.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo Saidi Benjamini alisema hivi sasa ni jambo la kawaida kwa mtu kuajiliwa mara baada ya kumaliza mafunzo pasipo kupewa elimu ya mazingira ya kazi hali inayopelekea idadi kubwa ya watumishi wa Serikali kudanga takwimu kwa jamii na taifa.

Naye mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Hawa Mathias alisema kutokana na teknolojia kukua baadhi ya watumishi wamekuwa wakitumia takwimu na tafiti kutoa elimu kwa wananchi pasipo kuangalia uhalisia wa eneo husika na kwamba tabia hiyo imekuwa ikichangia kwa sehemu kubwa elimu inayotolewa ndani ya jamii kutofanikiwa kwa sehemu kubwa kutokana na kutoendana na uhalisia wa eneo husika.

Naye mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoani Mbeya Christopher Nyenyembe alisema kuwa utafiti kabla ya kuandika habari ni moja ya taratibu za kazi kwa mwandishi bora na kuwataka waandishi wa habari kufanya tafiti kwakina ndani ya jamii kabla ya kuiandika habari badala ya kutumia tafiti zilizopo kwenye mitandao kwa sababu tafiti nyingine zimekuwa haziendani na uhalisia wa mazingira ya kazi.
 
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Maggid Mjengwa alisema tabia ya Serikali kuangalia zaidi vyeti vya elimu ndiyo matokea ya sasa kwa wanafunzi kuhitimu elimu yao ya msingi pasipo kujua kusoma wala kuandika.

Aidha tabia ya kuaingiza siasa na maarifa imekuwa ikichangia kwa sehemu kubwa kukwamisha maendeleo ya elimu hapa nchini ambapo hivi karibuni tumeona Taifa limeamua kuacha mfumo wa mwanafunzi kuonesha nini amejifunza kwa kipindi chote na tumeingia kwenye mfumo wa mwanafunzi kukisia majibu.

"Hivi karibuni Tanzania imengia kwenye mfumo wa usahihishaji wa mitihani ya darasa la saba kwa njia ya mtandao ambapo wanafunzi watakuwa wakiweka vivuli kwenye majibu sahihi badala ya wanafunzi hao kuonesha uwezo walionao kutokana na yale waliyofundishwa ambapo hii inahatarisha zaidi kwa taifa kuwa na wanafunzi wasio na uelewa na elimu kwa sababu ya kuandika majibu yao kwa njia ya kukisia pia huenda ikawa ni njia kubwa ya wanafunzi kupewa majibu ya mtihani kuliko hata tatizo la awali lililojitokeza"alisema Mjengwa

BREAKING NEWS:- FUATILIA PICHA ZA MATUKIO YA WATOTO WALIOZALIWA WAKIWA NA MAUMBILE YA NG'OMBE NA BINADAMU NA WAKUNGA WAKIJARIBU KUOKOA MAISHA YA WANANCHI WA VIJIJINI..

Kamanga na Matukio | 01:05 | 0 comments
*Usikose kutembelea mtandao huu.

AMPA MIMBA MWANAE WA KUMZAA - MZAZI

Kamanga na Matukio | 00:56 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
 Mkazi wa Mtaa wa Mbete,Kata ya Isanga Jijini Mbeya Bwana Yussuf Hamad(39),anatuhumiwa kumpa mimba binti yake wa kumzaa(15) jina lake limehifadhiwa.

Hayo yamethibitishwa na Mama mzazi wa binti huyo Bi, Regina Simon(35) baada ya kupata taarifa Mei 11 mwaka huu kuwa binti yake ana ujauzito wa miezi minne,na kuamua kutoa taarifa kwa Balozi  wa mtaa huo Bwana Steven Ovaova ambaye naye alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji Bwana Angelo Sanga.

Viongozi hao wa mtaa walimuita  mtuhumiwa na ili kupata ukweli wa tukio hilo,lakini mtuhumiwa alikanusha ingawa binti yake alithibitisha kutendewa ukatili huo na kwamba alikuwa akitishiwa kwa mapanga kila alipokuwa akifanya naye tendo la ndoa.

Baada ya uongozi kupata maelezo kutoka kwa binti huyo na mzazi kukataa waliamua kuipeleka kesi hiyo Polisi,ambapo walitoa PF3 iliyomwezesha binti huyo kupelekwa kwa daktari ambaye alithibitisha kuwa binti huyo ana ujauzito.

Hata hivyo hivi sasa binti huyo amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya akisubiri kujifungua ingawa umri mdogo wa binti huyo amekuwa chini ya uangalizi wa karibu wa daktari hospitalini hapo.

Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani Septemba 25 mwaka huu katika mahakama kuu jijini hapa,ili kujibu tuhuma zinazomkabili kesi inayotarajiwa kusikilizwa na hakimu wa mahakama hiyo mheshimiwa Majige.

AFARIKI AKIVUA SAMAKI

Kamanga na Matukio | 00:33 | 0 comments
Na Ezekiel Kamanga,Chunya.
Mwananchi mmoja aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Kidava,amefariki dunia akivua samaki katika Kitongoji cha Kambipotea,Kijiji cha Iyovyo,Kata ya Totowe Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.

Tukio hilo limetokea Septemba 19 mwaka huu majira ya saa 2 asubuhi,marehemu akiwa na Mtumbwi alipokwenda kuvua samaki na mauti hayo yamemkuta alipokuwa akivuta nyavu alizotega samaki,lakini nyavu hizo zilikwama kwenye mwamba ndipo marehemu alichupa kupiga mbizi ndani ya maji ili kujaribu kuzinasua nyavu hizo.

Aidha katika juhudi hizo za kunasua nyavu hizo marehemu alikosa hewa na dakika tatu baadae alipoteza maisha kutokana na kunasa katika nyavu hizo alizokuwa akijaribu kuzinasua.

Baada ya kushindwa kuibuka baadhi ya wavuvi waliokuwa karibu baada ya kuona marehemu haibuki baada ya kuzama walifuatilia eneo la tukio na kuanza kuvuta nyavu hizo hadi ufukweni mwa ziwa na kumkuta marehemu kapoteza maisha.

Wavuvi hao baada ya kuutoa mwili wa marehemu katika maji walitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kambipotea Bwana Richard Mbuya,ambapo alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na yeye kuitaarifu Polisi.

Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kuruhusu mwili huo kuchukuliwa kwa ajili ya maziko,kutokana na marehemu kutokuwa na ndugu hivyo Serikali ya kijiji ilichukua jukumu la mzishi,

Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa marehemu kabla ya kifo chake imedaiwa alitokea katika Kijiji cha Nzihi,barabara ya kuelekea Kidamali Mkoani Iringa.

KAMBA YA KUFUNGIA NG'OMBE YATUMIKA KUFUNGIA USUKANI WA BASI LA ABIRIA.

Kamanga na Matukio | 05:41 | 0 comments
 Sehemu ya chini ya usukani ukiwa umefungwa kwa kamba (ambayu hutumika kufungia ng'ombe) na mti kama uonavyo pichani,katika basi la abiria linalomilikiwa na Kampuni la Mwasha ambalo husafirisha abiria kutoka Sumbawanga/Mbeya na Mbeya/Sumbawanga. Hii imegunduliwa baada ya ajali iliyotokea hivi karibuni katika eneo la Senjele,Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya,baada ya basi hilo kupinduka ambapo zaidi ya abiria 50 walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Ifisi Wilaya ya Mbeya Vijijini.
 Baadhi ya mashuhuda wa ajali ya basi linalomilikiwa na Kampuni la Mwasha ambalo husafirisha abiria kutoka Sumbawanga/Mbeya na Mbeya/Sumbawanga. Hii imegunduliwa baada ya ajali iliyotokea hivi karibuni katika eneo la Senjele,Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya.
 Mmoja wa majeruhi akiwa amelazwa,akisubiri kupewa matibabu katika Hospitali ya Ifisi kufuatia ajali ya basi hilo lilolopinduka na kujeruhi abiria 50.
  Mmoja wa majeruhi akiwa mapumzikoni baada ya kupewa matibabu katika Hospitali ya Ifisi kufuatia ajali ya basi hilo lilolopinduka na kujeruhi abiria 50.
 Wauguzi wa Hospitali ya Ifisi wakikokota kitanda kilichobeba majeruhi wa ajali ya basi.
 Majeruhi akipatiwa matibabu.
Muuguzi Mkuu Sikitu Mbilinyi wa Hospitali ya Ifisi,akitoa taarifa ya majeruhi waliopokelewa katika Hospitali hiyo ya Ifisi,kufuatia ajali ya Kampuni la Mwasha ambalo husafirisha abiria kutoka Sumbawanga/Mbeya na Mbeya/Sumbawanga. Hii imegunduliwa baada ya ajali iliyotokea hivi karibuni katika eneo la Senjele,Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya,baada ya basi hilo kupinduka ambapo zaidi ya abiria 50 walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Ifisi Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Hata hivyo imedaiwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na basi hilo kubeba mizigo mizito na kujaza abiria kupita kiasi na usukani wake kufungwa kamba ya katani na mti.(Picha zote na Ezekiel Kamanga,Senjele)

MWANAMKE AJIFUNGUA KIUMBE KINACHOFANANA NA NG'OMBE

Kamanga na Matukio | 05:28 | 0 comments
*Kichwa cha ng'ombe.
*Kiwiliwili cha binadamu.

Na Ezekiel Kamanga,Chunya.
Mwanamke mmoja ambaye amefahamika kwa jina la Shija Paulo(35),mkazi wa Kijiji cha Magaga,Kata ya Mbuyuni Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya amejifungua kiumbe kinachofanana na ng'ombe chenye jinsi ya kiume.

Tukio hilo limetokea Septemba 16 mwaka huu majira ya saa 11 alfajiri,mwanamke huyo alipokuwa amepelekwa katika Zahanati ya Mbuyuni kwa ajili ya kujifungua akiwa na mumewake Bwana Mwigulu Yangula(Makeni) lakini kabla ya kufika zahanati mwanamke huyo alipatwa na uchungu ndipo alipoomba msaada kwa Mkunga wa jadi aliyekuwa karibu Bi. Agripina Fredrick Sikanyika(Namwinje).

Mkunga huyo alimpokea mwanamke huyo na kujifungua salama huku kiumbe hicho kikiwa na kichwa na domo mithili ya ndama(mtoto wa ng'ombe) chenye dalili ya kuota mapembe na manyoya meusi hadi eneo la kifuani ambapo kutoka hapo kifuani mpaka miguuni alikuwa na umbile la binadamu na jinsi ya kiume  licha ya kutimiza miezi tisha ya kuzaliwa na uzito wa wastani.

Hali hiyo ilimtisha sana Mkunga Bi. Sikanyika na kuitwa Bwana Yangula kushuhudia kiumbe hicho naye alistaajabu kwa yale yaliyotokea.

Hata hivyo kiumbe hicho kilidumu kwa muda wa masaa  matatu na kufariki dunia na katika uchunguzi wa mwandishi wa habari hii amebaini kuwa hiyo ilikuwa ni mimba ya nane kwa mwanamke huyo na kila mimba hupata watoto ambao si riziki.

Tukio hilo pia lilishuhudiwa na mhudumu wa Kituo cha Afya,kitongoji cha Magaga Bwana Josephat Alisen Ismail,ambaye naye amesema ameshangazwa na tukio hilo na kusema hajawahi kukutana na jambo hilo katika taaluma hiyo ya utabibu.

Wakati wa tukio hilo Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Michael Sanziwa hakuwepo na alipopigiwa simu aliruhusu kiumbe hicho kichukuliwe na mzazi ambapo maziko yake yalifanyika kandokando ya nyumba ya Bwana Yangula.

Katika tukio hilo watu wengine wamelihusisha na imani za kishirikina na wataalamu wa viumbe wamesema kuwa mara nyingi viumbe hivyo huwa haviishi muda mrefu,lakini hali ya mama aliyejifungua inaendelea vema baada ya kujifungua.

MWANAFUNZI AANGUKA NA MTI NA KUPOTEZA MAISHA.

Kamanga na Matukio | 05:27 | 0 comments
*Kichwa chake chapasuka na utumbo watoka nje.

 Habari na Ezekiel Kamanga,Sumbawanga Vijijini.
Mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kilangawana,Kijiji cha Maleza,Kata ya Kapeta,Wilaya ya Sumbawanga Vijijini Mkoani Rukwa aitwaye Imani Nzala(12),amefariki dunia baada ya kudondokewa na mti ulikokuwa ukikatwa na Babu yake Bwana Nzala kwa ajili ya kuchomea tanuli la tofali.

Katika ajali hiyo ya kusikitisha iliyotokea Septemba 16 mwaka huu majira ya saa tano,mtoto huyo alipasuka kichwa na utumbo wake kutoka nje hali iliyopelekea kukimbizwa hadi Kituo cha Afya cha Kilangawana.

Licha ya marehemu kukimbizwa katika kituo hicho akiwa bado hajafariki,Muuguzi wa kituo hicho aliomba Imani awaishwe hadi Kituo cha Afya cha Kamsamba,ambako huko kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa waliomba asafirishwe hadi Hospitali ya Wilaya ya Mbozi,lakini kabla ya gari la wagonjwa kufika mwanafunzi huyo alifarikia dunia.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kamsamba Bwana Michael Kajemi,amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba kifo cha mwanafunzi huyo kimetokana na kuvuja damu nyingi katika mwili wake.

Mazishi ya kuupumzisha mwili wa marehemu Imani,kwenye nyumba yake ya milele yamefanyika Septemba 17 mwaka huu kijijini kwao.

NOTI ZA SHILINGI 500 NA 2000 ZA HARIBIWA KWA AJILI YA KUTENGENEZA POMBE AU KUVUTIA SIGARA.

Kamanga na Matukio | 05:26 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Sumbawanga Vijijini.
Taifa linaweza kuingia katika hatari ya kudidimia kwa uchumi kufuatia watu wasiokuwa na mapenzi na taifa hili kuziharibu noti za shilingi 500 na 2000 kwa kuondoa mstari(ufito) unaong'aa na unaohalalisha pesa hizo na kisha kuutumia katika pombe za kienyeji au bia ili kuongeza kileo wakidai kuwa husaidia kuokoa pesa kwani hulewa kwa muda mfupi.

Mbali na hivyo mstari huo(ufito) pia huzichanganya na sigara au tumbaku ambapo hudai hulewa haraka,hivyo kufanya uadimu wa noti hizo katika maeneo ya Kijiji cha Maleza,Kata ya Kipeta,Wilaya ya Sumbawanga Vijijini.

Athari hiyo pia imevikumba vijiji vya Kilangawana na Kamsamba hali ambayo imefanya kuwepo kwa ugumu wa upatikanaji wa fedha hizo.

Hata hivyo wananchi kadhaa ambao hawakupenda majina yao kutajwa,wamethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kuitaka Serikali na Benki Kuu kuchukua hatua za haraka ili kukomesha vitendo hivyo.

Katika hali ya kuhalalisha noti hizo zilizoharibiwa wahalifu hao hutumia gundi kwa kutumia uzi wa mifuko ya mbolea ili ziendelee kutumika na hivyo kuzalisha noti bandia.

Wakati huohuo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema wanapopokea noti hizo na pia kuwafichua wahalifu hao.

WANUSURIKA KIFO:- WANAFUNZI 23 WA SHULE YA MSINGI KAPUNGA WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUOKOTA MIKATE INAYOSADIKIWA KUWA NA SUMU.

Kamanga na Matukio | 05:12 | 0 comments
*Ni katika shamba la Kapunga Rice Project.
*Wazazi wacharuka na kuanza kujenga shule mpya mahali alipobomoa mwekezaji.
*Zaidi ya shilingi milioni 2.5 zachangwa papo hapo.

Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Wanafunzi 23 wa Shule ya Msingi Kapunga,Kijiji cha Mapogolo,Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wamenusurika kifo baada ya kula mikate inayosadikiwa kuwa na sumu mnamo mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Ramadhani Nyoni na mzazi mmoja wapo wa watoto waliokumbwa na janga hilo la kusikitisha na kuhatarisha uhai.

Mzazi huyo ambaye hakupenda jina lake kutaja amesema yeye ilimlazimu kununua lita 20 za maziwa,kisha kuwanywesha watoto hao na kuokoa maisha yao ambapo hali zao zimetajwa kuendelea vema.

 Wakazi wa kijiji hicho wakionekana kukerwa na kitendo hicho iliwalazimu kuitisha mkutano wa hadhara na kuazimia kujenga shule mpya ili kuwaondoa watoto katika shule iliyopo katika shamba la mwekezaji.

 Mbali ya wananchi kukerwa na vitendo vya kikatili vya mwekezaji huyo,pia Walimu wamefurahia uamuzi wa wanakijiji kuamua kujenga shule mpya katika himaya ya kijiji ili kuondoa adha ya kutembea umbali wa kilometa 52 kwenda na kurudi kutoka Chimala,ambako ndipo walipopanga kutokana na uhaba wa nyumba kijijini hapo na zilizopo shambani kwa mwekezaji walimu hao hufukuzwa mara kwa mara.

Aidha wazazi hao waliachanga jumla ya shilingi 2,500,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi,ambapo Afisa Elimu kitengo cha Ujenzi amesema atawakabidhi ramani ya shule,uongozi wa kijiji,ili kuondoa adha ya wakazi zaidi ya 12,000 wanaoishi eneo hilo ambapo shughuli za maendeleo zimedumazwa na mwekezaji huyo ikiwemo kuhodhi miundombinu kama barabara,umeme na maji.

Licha ya miundo mbinu yote kupita kijijini hapo lakini wananchi hawanufaiki nayo bali kuambulia kipigo na kufunguliwa kesi mahakamani pasipo sababu maalumu.

Hata hivyo wananchi hao wamesema hawakuona sababu yoyote ya msingi kuweza kutoa taarifa katika Jeshi la polisi,kutokana na mwekezaji kujaza mafuta magari pindi magari ya jeshi hilo yanapoenda kijijini hapo.

Wananchi hao walienda mbali zaidi kwa kusema kuwa baadhi ya mifugo ya wananchi imekuwa ikiuawa mara kwa mara na mwekezaji huyo,lakini hakuna hatua zozote ambazo zimekuwa zikichukuliwa likiwemo tukio la wananchi kugongwa na gari la mwekezaji ambapo alimfukuza na kisha kumgonga mwananchi huyo,ambaye kwa sasa amepata ulemavu na mwekezaji kutochukuliwa hatua zozote tangu mwezi Julai mwaka jana.

Pia mwekezaji huyo mapema mwezi Januari mwaka huu alichoma mpunga wa wakulima kwa kunyunyizia dawa kupitia ndege ya umwagiliaji na kusababisha zaidi ya wananchi 150 kuathiriwa na sumu hiyo ya mimea na kuwasababishia hasara kubwa,ambapo njaa inatazamiwa kuwakabili wananchi hao.

TAMAA:- ADUNDWA MAKABURINI BAADA YA KUTAFUNA PESA ZA JENEZA

Kamanga na Matukio | 05:11 | 0 comments
**Marehemu azikwa bila jeneza.
**Fundi aliyepewa pesa atorokea Mbeya.
**Watumishi wa Mungu washuhudia kichapo.
Habari na Ezekiel Kamanga.,
Bwana Marco Sikalunga Mkazi wa Kijiji cha Chilangawana,Sumbawanga Vijijini mpakani na Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya amenusurika kufikwa na mauti paacha ya kupokea kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali,baada ya kupewa jukumu la kuchangisha fedha shilingi 50,000 kwa ajili ya kuchonga jeneza.

Bwana Sikalunga alidai kuwa fedha hizo zilizochangishwa alimkabidhi fundi anayefahamika kwa jina la Senga na kwamba utakapofika muda wa saa za kuzika ataleta jeneza hilo.

Lakini katika mshangao mnamo Septemba 13 mwaka huu ulitokea msiba kijijini hapo,ambapo alifariki Suzana Upepo,na kijana huyo alipotakiwa kupeleka jeneza alidai anaenda kuchukua kwa fundi na alipofika nyumbani kwa fundi huyo hakufanikiwa kumkuta.

Kufuatia sakata hilo wananchi waliamua kuuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuzika bila jeneza,wakiwa njiani wananchi hao wakiwa na hasira kali walimpiga Bwana Sikalunga mbele ya Mchungaji Ladislaus Kamanga na Gidion .A. Simponda(Mwandete).
Hata hivyo Bwana Senga ambaye ni fundi aliyepewa jukumu la kutengeneza jeneza hilo anadaiwa kutorokea Mkoani Mbeya na kiasi hicho cha fedha cha shilingi 50,000.
Wakati huo huo wananchi hao wanatarajia kumchukulia hatua za kisheria Bwana Sikalunga.

MWENYEKITI WA KIJIJI AKATA MITI YA SHULE BILA RIDHAA YA KAMATI

Kamanga na Matukio | 05:06 | 0 comments
*Kamati yacharuka yamtaka alipe fidia.
*Vijana watishia kikao cha ndani.
*Diwani akanusha kumbeba mwenyekiti.

Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Motomoto Bwana Kassimu Mwagala,amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuitwa na Kamati ya Shule ya msingi Motomoto alipotakiwa kutolea maelezo suala la kukata miti saba ya shule hiyo kutokana na shinikizo la vijana kutaka kuongeza uwanja wa shule pasipo ridhaa ya kamati hiyo.

Akiongea kwa masikitiko Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi Lydia Mdoe,amesema kitendo hicho kilichofanywa na mwenyekiti huyo nicha dharau,hivyo kuwafanya waishi kwa hofu shuleni hapo licha ya dhamana waliyopewa na Serikali ya kulinda mali za shule na mazingira yetu.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo Bwana Yusuph Tosha amesema ukataji wa miti hiyo uliofnya na Mwenyekiti wa kijiji ni kuifanya kamati yake kuonekana haifanyi kazi na ni kuingilia majukumu.

Hali hiyo ilizua taflani katika kikao ambapo Bwana Mwagala kwa kujihami aliandamana na kundi la vijana,ambao walifanya fujo katika mkutano na baadae Diwani wa Kata ya Ruiwa mheshimiwa Alex Mdimilage aliagiza kuwa vijana wote waitwe Ofisi ya kata watoe maelezo ni kwani walivamia mkutano usiowaruhusu.

Hata hivyo kutokana na kukera na kitendo cha Mwenyekiti wa kamati hiyo ilimtaka kulipa jumla ya shilingi 210,000 ili iwe onyo kwake,ambapo ametakiwa kuomba radhi,kamati hiyona kutakiwa kuzilipia kabla ya Oktoba 12 mwaha huu.
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger