Pages


Home » » Waziri Nape Nnauye amesema sekta ya habari nchini inakabiliwa na changamoto kubwa.

Waziri Nape Nnauye amesema sekta ya habari nchini inakabiliwa na changamoto kubwa.

Chimbuko Letu | 09:00 | 0 comments
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Nape Nnauye akizungumza na wadau wa Habari,Michezo na sanaa Mkoa wa Mbeya (hawapo pichani)katika ukumbi wa Mikutano wa Mkapa jijini Mbeya April 2 ,2016 .(Picha Keneth Ngelesi)


Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema sekta ya habari nchini inakabiliwa na changamoto kubwa kwa waandishi wake kushindwa kufanya utafiti na kwenda kufanya kazi kwenye matukio.

Waziri Nape aliyasema hayo  alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama cha Waandishi wa habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI) alipotembelea makao makuu ya chama hicho jijini Mbeya.

Alisema changamoto ya waandishi kushindwa kwenda kupata habari kwenye matukio na kutokufanya utafiti wa kutosha hupelekea habari nyingi kupikwa na kukosa weledi pamoja na kutokuwa na manufaa kwa jamii.

“Habari nyingi huandikwa kutoka habari maelezo basi lakini mwandishi akifanya utafiti na kwenda field kutasaidia kuja na habari nzuri yenye manufaa kwa jamii” alisema Nape.


Waziri Nape alisema changamoto hiyo inaweza kuondolewa endapo mswada wa sheria ya habari uliorekebishwa utapitishwa bungeni baada ya kupitiwa upya. 

Alisema uboreshaji wa mswada wa sheria ya huduma ya vyombo vya habari unaondoa kipengele cha sheria kandamizi  ya kufungia magazeti hukosesha ajira kwa watu wengi badala ya kumwajibisha mhusika mwenyewe ili afanye kazi kwa weledi.

Waziri Nape alipongeza ubunifu uliofanywa na waandishi wa habari kwa kuunda Chama ambacho kitasaidia kuwainua waandishi wa habari ili kuandika habari zenye weledi na faida kwa jamii.

“Niwapongeze TAJATI kwa kuanzisha chama hiki, hiyo ni ndoto yangu mimi kuona sisi waandishi tunafanya kazi mbele zaidi ya kuandika ni jambo zuri kwa mwandishi kuspesholaizi kitu kimoja” alisema Nape.

Alisema kupitia TAJATI itasaidia kuwepo kwa uwajibikaji kwa Serikali kuhusiana na maswala ya utalii na uwekezaji kwani kila kitakachoandikwa kimekuwa kimefanyiwa utafiti ambapo pia sekta hizo zitaimarika vizuri.

Aidha alitoa wito kwa uongozi wa Tajati kuhakikisha Chama hicho kinafungua matawi katika mikoa mingine ili kukifanya kubeba taswira ya kitaifa zaidi kuliko kuwepo katika Mkoa mmoja.

Awali akimkaribisha Waziri, Mwenyekiti wa TAJATI Ulimboka Mwakilili alisema chama kina mikakati mikubwa ya kujitangaza mikoani ambapo kwa kuanzia tayari mikoa mitano ya Kanda ya Nyanda za juu kusini imepata wawakilishi.

Alisema baada ya usajili wanachama kama timu wameshafanya kazi ya kutambua vivutio vya utalii na kutembelea viwanda vinavyofanya kazi na vilivyokufa ili kujua sababu iliyopelekea kushindwa kuendelea kuzalisha.

“Nikupongeze Waziri kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa serikali kufika ofisini kwetu, hii ni ofisi ya kitaifa ambayo inaunga mkono hoja yako ya kutaka makao makuu kuondoka jijini Dar es Salaamnasi tumefanya hivyo, pia tayari tumeanza kufuatilia viwanda ili kuendana na sera ya serikali ya awamu ya tano kuwa na uchumi wa viwanda” alisema Mwakilili.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger