Home » » Wananchi mkoani Songwe wametakiwa kuzitumia fursa ili kujipatia maendeleo.

Wananchi mkoani Songwe wametakiwa kuzitumia fursa ili kujipatia maendeleo.

Chimbuko Letu | 08:40 | 0 comments
 Luteni Mstaafu Chiku Galawa Mkuu Mpya wa Mkoa wa Songwe (Mkoa Mpya).
Wananchi mkoani Songwe wametakiwa kuzitumia fursa zinazotokana na changamoto zinazowakabili kwa  kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia maendeleo na kutimiza wajibu katika majukumu yao ya kila siku.


Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe (zamani Mbeya) Luteni Mstaafu Chiku Galawa wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro iliyofanyika katika makao makuu ya Mkoa wa Songwe yaliyopo Vwawa wilayani Mbozi.


Galawa alisema uwepo wa changamoto mbali mbali katika mkoa huo ndiyo iwe chachu kwa wananchi kutumia fursa hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili waweze kuziondoa kwa pamoja na kuufanya mkoa huo kusonga mbele kimaendeleo licha ya kuwa Mkoa mchanga.


“Pamoja na Mkoa wetu kuwa mchanga napenda kuwaambia kuwa tuzitumie changamoto zilizopo kama fursa ya kupata maendeleo na kinachotakiwa ni kila mmoja wetu kuwajibika katika nafasi yake kwani kwa kufanya hivyo wengine watakuja kujifunza Songwe ingawa ni Mkoa Mchanga” alisema Galawa.


Aliongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa kufanya kazi kwa mshikamano ili kuenzi umoja na utulivu kwa kila mtu kutii sheria bila shuruti kwa kuepuka kudai haki kwa vurugu kwani athari zake ni kubwa na kuzolotesha shughuli za uzalishaji mali kutokana na kupunguza rasilimali watu, muda na uharibifu wa mali za umma.


Awali akizungumza katika makabidhiano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mstaafu, Abbasi Kandoro alisema ni vema Mkuu wa Mkoa wa Songwe akajikita katika kutatua changamoto za Wananchi kwani wengi wao ni wachapa kazi ambao hawasubiri kutumwa kwenye shughuli za uzalishaji mali hususani kilimo.


Alisema awali Mkoa wa Mbeya ulikuwa mkubwa jambo lililochangia Changamoto nyingi kushindwa kutatuliwa kwa wakati lakini sasa Mkoa wa Mbeya unabaki na kilomita za mraba 34606 huku Mkoa mpya wa Songwe ukibaki na kilomita za mraba 29011 ukiwa na Wilaya 4, Halmashauri 5, Tarafa 12, Kata 74, vijiji 307 na mitaa 71.


Alisema Wananchi wa Songwe wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uvunjifu wa amani unaotokana na kudai haki pasipo kufuata sheria jambo linalopelekea kuchoma barabara na kuharibu mali hali inayojitokeza zaidi Tunduma, Vwawa na Mlowo.


Alisema tatizo linguine ambao Mkuu wa Mkoa anapaswa kuliangalia kwa ukaribu akishirikiana na viongozi wa mila nadini ni pamoja na  mauaji ya kishirikina pamoja na kujichukulia sheria mkononi hali inayosababishwa na imani za kishirikina, ulevi, wivu wa kimapenzi na ujambazi.


Wakati huo huo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Nyasebwa Chimagu alisema baada ya makabidhiano ya ofisi kazi inapaswa kuanza moja kwa moja ambapo baadhi ya watumishi walipewa uhamisho wa muda ili kuendelea na kazai katika Mkoa mpya wa Songwe.


Nyasebwa aliwataja watumishi hao kuwa ni pamoja na Dereva wa Mkuu wa Mkoa Samson Lyimo, Karani wa Mkuu wa Mkoa, Jesca Ndaga, Katibu wa Mkuu wa Mkoa, Devotha Chacha na Kaimu Katibu tawala Msaidizi(Utawala) ambaye alikuwa Katibu tawala Wilaya ya Kyela.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger