Pages


Home » » BABA AUZA NYUMBA MTOTO AKIWEMO NDANI NA KUTOKOMEA KUSIKOJULIKANA.

BABA AUZA NYUMBA MTOTO AKIWEMO NDANI NA KUTOKOMEA KUSIKOJULIKANA.

Kamanga na Matukio | 04:56 | 0 comments
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimeendelea kushika kasi katika baadhi ya maeneo hususani vijijini, licha ya Serikali na asasi mbali mbali kulipigia kelele ambapo hivi karibuni Baba mmoja aliamua kuuza nyumba ikiwa na watoto ndani na kutokomea kusikojulikana na kuwaacha wasijue la kufanya.


Mkasa huo wa ajabu ulitokea katika kijiji cha Hatwelo, Kata ya Ijombe Mbeya Vijijini ambapo Mkazi huyo aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Yuta alipouza nyumba yake na kutokomea yeye na mkewe na kuwaacha watoto wawili wenye umri kati ya miaka 9 na 11 wakikosa mahala pa kuishi.


Akizungumzia sakata hilo kijijini hapo, Mwanaharakati wa haki za Binadamu, Yasin Yuta, alisema majirani waligundua baada ya kusikia kelele za mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Erasto Emmanuel (11) aliyekuwa amefungiwa ndani na kukaa kwa siku saba.


Alisema baada ya kumfungulia mtoto huyo ndipo ilipobainika kuwa nyumba hiyo ilikuwa imeshauzwa huku mtoto akiwa ndani na ndipo mnunuzi alipofunga na kufuli bila kujua kama kuna mtoto ndani huku watoto wengine wakiwa kwa ndugu zao ambao pia hawakuelezwa kama nyumba imeuzwa.


Nyumba hiyo iliuzwa kwa Dati Nsagaje kwa gharama ya shilingi 750,000/= ikiwa ni nyumba mbili pamoja na kiwanja ambapo mnunuzi huyo alilipa kianzio cha shilingi laki nne biashara iliyofanyika tangu April 26 mwaka huu  na kiasi kilichobaki wakiwa wameahidiana kulipana Mwezi Mei 15, Mwaka huu.


Wahanga wa tukio hilo ambao ni watoto walisema hawakuwa na taarifa zozote za kuuzwa kwa nyumba wanayokaa ambapo walisikia kuwa baba yao ameenda Sumbawanga kumfuata  mke wake ambaye inasemekana aliolewa na mwanaume mwingine.


“ Nilikuwa nimelala  ndani ambapo nilipoamka asubuhi nilikuta mlango umefungwa kwa nje hata hivyo nilivumilia hadi njaa ilipoanza kuniuma baada ya siku tano nikaanza kupiga kelele ndipomajirani walipokuja kunifungulia na kuniambia nyumba imeuzwa” alisema mtoto Erasto Emmanuel.  


Mtoto mwingine aliyetelekezwa ambaye siku ya tukio alikuwa ameenda kulala kwa bibi yake Groli Emmanuel (9) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Hatwelo alisema siku akiwa anaondoka aliagwa na baba yake ambaye alimwachia shilingi 3000 lakini hakumwambia kama nyumba imeuzwa.


Kutokana na kitendo hicho kutokubalika, baadhi ya Majirani baadhi ya majirani walisema ni kitendo cha kinyama na hakipaswi kufumbiwa macho ambapo waliamua kuchanga fedha ili kuikomboa nyumba ili irudi mikononi mwa watoto.


Majirani hao walifanikiwa kuchanga shilingi 410,000/= alizokuwa amedai mnunuaji ili aweze kurejesha nyumba ikiwa ni fedha alizokuwa ametoa awali hivyo kukubaliana kuicha nyumba hiyo ambayo kwa mujibu wa majirani na baadhi ya ndugu wamesema itakuwa ni mali ya watoto.


Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida na kuonesha kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kijiji ambao walishiriki moja kwa moja zoezi hilo huku wakiwa wamesaini kama mashahidi na kugonga mhuri wa Serikali ya Kijiji walipoulizwa kuhusiana na sakata hilo hawakuwa na majibu ya kuridhisha.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Hawelo, Ibrahimu Mponzi, alisema kitendo alichokifanya muuzaji ni cha kawaida kwa sababu ameuza mali yake mwenyewe na kwamba wao kama majirani na serikali ya kijiji hawawezi kuhoji atakako waacha watoto kwa sababu ni mipangilio ya maisha ya kila mtu.


Mbali na mwenyekiti wa Kijiji kuwa shahidi wa upande wa mnunuaji akiwa sambamba na watu wengine wanne akiwepo Mkewe ambaye pia ni Balozi wa nyumba kumi pia waliosaini wengine ni ndugu wa mnunuaji ili hali muuzaji akiwa hana shahidi hata mmoja.


Aidha juhudi za majirani kuikomboa nyumba hiyo na kuwa mali ya watoto zilifanikiwa ambapo mnunuzi Datistani Mwanshinga alibatilisha ununuzi wa nyumba hiyo Mei 9, Mwaka huu baada ya kukiri kurejeshewa fedha zake.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger