Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Vitendo vya ukatili dhidi ya
watoto vimeendelea kushika kasi katika baadhi ya maeneo hususani vijijini,
licha ya Serikali na asasi mbali mbali kulipigia kelele ambapo hivi karibuni
Baba mmoja aliamua kuuza nyumba ikiwa na watoto ndani na kutokomea
kusikojulikana na kuwaacha wasijue la kufanya.
Mkasa huo wa ajabu ulitokea
katika kijiji cha Hatwelo, Kata ya Ijombe Mbeya Vijijini ambapo Mkazi huyo
aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Yuta alipouza nyumba yake na kutokomea yeye na
mkewe na kuwaacha watoto wawili wenye umri kati ya miaka 9 na 11 wakikosa
mahala pa kuishi.
Akizungumzia sakata hilo
kijijini hapo, Mwanaharakati wa haki za Binadamu, Yasin Yuta, alisema majirani
waligundua baada ya kusikia kelele za mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la
Erasto Emmanuel (11) aliyekuwa amefungiwa ndani na kukaa kwa siku saba.
Alisema baada ya kumfungulia
mtoto huyo ndipo ilipobainika kuwa nyumba hiyo ilikuwa imeshauzwa huku mtoto
akiwa ndani na ndipo mnunuzi alipofunga na kufuli bila kujua kama kuna mtoto
ndani huku watoto wengine wakiwa kwa ndugu zao ambao pia hawakuelezwa kama
nyumba imeuzwa.
Nyumba hiyo iliuzwa kwa Dati
Nsagaje kwa gharama ya shilingi 750,000/= ikiwa ni nyumba mbili pamoja na
kiwanja ambapo mnunuzi huyo alilipa kianzio cha shilingi laki nne biashara
iliyofanyika tangu April 26 mwaka huu na
kiasi kilichobaki wakiwa wameahidiana kulipana Mwezi Mei 15, Mwaka huu.
Wahanga wa tukio hilo ambao ni
watoto walisema hawakuwa na taarifa zozote za kuuzwa kwa nyumba wanayokaa ambapo
walisikia kuwa baba yao ameenda Sumbawanga kumfuata mke wake ambaye inasemekana aliolewa na
mwanaume mwingine.
“ Nilikuwa nimelala ndani ambapo nilipoamka asubuhi nilikuta
mlango umefungwa kwa nje hata hivyo nilivumilia hadi njaa ilipoanza kuniuma baada
ya siku tano nikaanza kupiga kelele ndipomajirani walipokuja kunifungulia na
kuniambia nyumba imeuzwa” alisema mtoto Erasto Emmanuel.
Mtoto mwingine aliyetelekezwa
ambaye siku ya tukio alikuwa ameenda kulala kwa bibi yake Groli Emmanuel (9)
ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Hatwelo alisema siku akiwa anaondoka
aliagwa na baba yake ambaye alimwachia shilingi 3000 lakini hakumwambia kama
nyumba imeuzwa.
Kutokana na kitendo hicho
kutokubalika, baadhi ya Majirani baadhi ya majirani walisema ni kitendo cha
kinyama na hakipaswi kufumbiwa macho ambapo waliamua kuchanga fedha ili
kuikomboa nyumba ili irudi mikononi mwa watoto.
Majirani hao walifanikiwa
kuchanga shilingi 410,000/= alizokuwa amedai mnunuaji ili aweze kurejesha
nyumba ikiwa ni fedha alizokuwa ametoa awali hivyo kukubaliana kuicha nyumba
hiyo ambayo kwa mujibu wa majirani na baadhi ya ndugu wamesema itakuwa ni mali
ya watoto.
Hata hivyo katika hali
isiyokuwa ya kawaida na kuonesha kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi wa
Serikali ya Kijiji ambao walishiriki moja kwa moja zoezi hilo huku wakiwa
wamesaini kama mashahidi na kugonga mhuri wa Serikali ya Kijiji walipoulizwa
kuhusiana na sakata hilo hawakuwa na majibu ya kuridhisha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha
Hawelo, Ibrahimu Mponzi, alisema kitendo alichokifanya muuzaji ni cha kawaida
kwa sababu ameuza mali yake mwenyewe na kwamba wao kama majirani na serikali ya
kijiji hawawezi kuhoji atakako waacha watoto kwa sababu ni mipangilio ya maisha
ya kila mtu.
Mbali na mwenyekiti wa Kijiji
kuwa shahidi wa upande wa mnunuaji akiwa sambamba na watu wengine wanne akiwepo
Mkewe ambaye pia ni Balozi wa nyumba kumi pia waliosaini wengine ni ndugu wa
mnunuaji ili hali muuzaji akiwa hana shahidi hata mmoja.
Aidha juhudi za majirani
kuikomboa nyumba hiyo na kuwa mali ya watoto zilifanikiwa ambapo mnunuzi
Datistani Mwanshinga alibatilisha ununuzi wa nyumba hiyo Mei 9, Mwaka huu baada
ya kukiri kurejeshewa fedha zake.