Mkuu wa Wilaya ya Kalonga, Nchini Malawi Rosemary Kalonga na Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dk Thea Ntara.
Na Ezekiel Kamanga.
Watu 17 wakazi wa Kijiji cha Lusungo Kata ya Lusungo Wilaya
ya Kyela Mkoani Mbeya wamekamatwa kwa kutokuwa na vyoo na uchafu wa mazingira
hivyo kuzorotesha juhudi za kupambana na ugonjwa wa kipindupindu Wilayani humo.
Ugonjwa huo umedumu kwa kipindi cha miezi mitatu sasa na Kata
ya Lusungo na Ndobo ndizo pekee bado zina wagonjwa wa kipindupindu hali
iliyomfanya Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dakta Thea Ntara kupiga kambi Kata ya
Lusungo ili kufanya ukaguzi wa vyoo na usafi wa mazingira.
Hata hivyo juhudi za Mkuu wa Wilaya zinakwamishwa na Diwani
wa Kata ya Lusungo Veronica Kanyanyila na Mwenyekiti wa Kijiji Zawadi Lugano
Mwangojola ambao wamekuwa wakidai ugonjwa huo umesababishwa na imani za
kishirikina na si uchafu au ukosefu wa vyoo.
Katika oparesheni hiyo maalumu iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya
aliyeambatana na Maafisa wa Afya pia iliyakumba maeneo mbalimbali kama Kata ya
Ikama na Kijiji cha Tenende ambapo alilazimika kuvunja Kilabu cha pombe Kata ya
Ikama baada ya kuwakuta wakazi wa eneo hilo wakinywa pombe za kienyeji katika
mazingira machafu.
Mbali ya ukaguzi huo pia Mkuu wa Wilaya alishuhudia baadhi ya
wananchi wakinywa pombe ya moshi na pombe zilizopigwa marufuku kutoka nchi
jirani na kulazimika kuwakamata wahusika ambao wamefikishwa kituo kikuu cha
Polisi Wilaya ambapo pindi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Dakta Thea aliteketeza sindano zinazodhaniwa kutumika kwa
ajili ya kujidunga wakati wa matumizi ya madawa ya kulevya katika Kata ya Ikama
na ametoa agizo la kuwasaka wauzaji wa madawa hayo na wanaouza pombe
zilizopigwa marufuku kutoka nchi jirani.
Kwa upande wake Afisa Afya Geophrey Baroshi amesema kuwa
zoezi hilo ni endelevu na watahakikisha kila kaya ina choo na kuwa na mazingira
safi kwa muda wote ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huo Wilayani Kyela na kwamba
waliokamatwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mtendaji wa Kijiji cha Lusungo Fadhili Sade amesema kuwa
wamefanya ukaguzi katika kaya 681 za kijiji hicho na zote hazina vyoo hali
inayofanya mapambano ya kipindupindu kuwa magumu mno kwani wengi wao wamekuwa
wakiamini ugonjwa huo unatokana na ushirikina.
Aidha Mtendaji wa Kata ya Lusungo Stephen John amesema
wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa Diwani wa Kata na Mwenyekiti wa kijiji
kuwa aache kutangaza kuwa Kata hiyo inakabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu
kwani ndiyo kunachochea kuongezeka kwa ugonjwa huo ambao unatokana na ushikina
na si uchafu au ukosefu wa vyoo.
0 comments:
Post a Comment