·
Ataka watoto wa kike wapewe kipaumbele katika
elimu
·
Ni wale wanao walaghai wanafunzi
Mke wa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Tunu
Pinda, amewakemea baadhi ya wanaume wanaotumia matatizo waliyonayo wanafunzi wa
kike na kuwalaghai ili watimize haja zao kwa kuwarubuni kuwahudumia huku
akiitaka jamii ya Watanzania kuwapa watoto wa kike kipaumbele katika elimu.
Mama pinda ameyasema hayo katika uzinduzi wa mradi wa
Msichana kwanza uliofanyika mkoani Mtwara huku akitanabaisha kuwa watoto wengi
wa kike wanashindwa kuhudhuria masomo pale wanapokuwa kwenye hedhi.
Alisema, hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wasichana
wanaotoka kwenye familia zinazoishi katika hali duni hukosa haki ya kimsingi ya
kuweza kumudu usafi wao na kushindwa kuhudhuria masomo yao huku akiwakemea
wanaume “Mafataki” wanaowalaghai mabinti kwa kuwahaidi kuwahudumia.
“Baadhi ya wasichana, kwa kukosa mahitaji muhimu zikiwemo
pedi, wamejiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na ’mafataki’ ambao huwaahidi
kushugulikia mahitaji yao. Hali hii haikubaliki”
“Tatizo la hedhi limekuwa likiwasumbua mabinti wetu hasa
walioko katika maeneo ya vijijini na wengine walioko katika mazingira duni,
alisema Mama pinda.
Mradi huo ambao umeandaliwa na TMARC na USAID kwa ufadhili
wa Vodacom Foundation umelenga kuwakomboa wasichana wanaokosa kuhudhuria masomo
mashuleni wakati wakiwa kwenye hedhi
umelenga kuwa endelevu na wa gharama nafuu kwa kuwawezesha wasicha zaidi ya 10,535
waliopo ndani na nje ya shule kwa kuanzia mikoa ya Lindi na Mtwara.
Pamoja na kuishukuru Vodacom, T -MARC na USAID, Mama Pinda
ameongeza kuwa ni vyema sasa jamii ikaliona tatizo hilo na kulipa kipaumbele
haina haja ya kufumbia macho tatizo hili ili kuwawezesha watoto wa kike
kutimiza malengo yao na ndoto zao huku akitoa wito kwa viongozi wa serikali
hasa katika ngazi za mikoa kuhakikisha mradi huo unafanikiwa na kuwa endelevu
kwa kutoa ushirikiano unaofaa kwa wahusika na kuhakikisha waalimu wanahusishwa
kwa ukaribu zaidi.
Nae Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Jamii (Vodacom
Foundation), Yessaya Mwakifulefule, alisema kuwa “Tunaamini kwamba mradi huu
utabadilisha tabia na hivyo kupunguza tabia hatarishi za ngono miongoni mwa
vijana sambamba na kujikinga na kuanza kushiriki ngono mapema kama njia ya
kupunguza mimba kwa wasicha wadogo mashuleni, kuepusha maambukizi ya magonjwa
yanayoambukiza kama vile UKIMWI na pia kupunguza utoro mashuleni.”
Aidha, Mwakifulefule alisema kuwa baada ya kipindi cha miaka
miwili, mradi huo unapaswa kutoa mafunzo ya jinsi ya kujitunza na kufanya usafi
na hivyo kuwapatia manufaa endelevu na stahiki kwa jamii katika mikoa hiyo ya
Lindi na Mtwara.
“Tunaamini kwamba mradi huu utafika mbali katika suala zima
la usafi kwa wasichana mashuleni sambamba na kudumisha heshima yao binafsi,”
alisema Mwakifulefule, akiongeza kuwa, “Vodacom Foundation imewekeza kiasi cha
shilingi milioni 160.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa T - MARC Diana kisaka, alisema
kuwa mradi huo wa majaribio wa miaka miwili unalenga kuwafikia mabinti wote
wanaoishi katika mazingira duni.
“Lengo la mradi huu ni kuwasaidia wasichana hawa ambao
wamekuwa hawaudhurii masomo kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama za mataulo
maalum kwa ajili kuwasitiri wakati wanapokuwa kwenye hedhi kitu ambacho
kimechangia kufanya vibaya mashuleni. Hivyo, tunaamini kwa kuanzisha mradi huu
utawasaidia kuboresha mahudhurio yao mashuleni sambamba na matokeo yao kuwa
mazuri,” alisema Kisaka.
0 comments:
Post a Comment