Picha ya pamoja
BARAZA la Ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra ccc) limetakiwa kubuni njia mbadala itakayosaidia kuondoa changamoto ya usafiri kwa wanafunzi pindi wanapoenda na kutoka mashuleni.
Mwito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Michael Kadeghe, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, wakati akizindua Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri wa nchi kavu na majini Mkoa wa Mbeya, katika hafla iliyofanyika jana katika ukumbi wa Haoteli ya Mtenda Sunset iliyopo Soweto Jijini hapa.
Kadeghe alisema hivi sasa kuna changamoto ya usafiri kwa wanafunzi nchi nzima hali inayosababisha wanafunzi kuhangaika kutafuta usafiri wa kuwarudishwa makwao kutokana na asilimia kubwa kutoka mbali na shule ziliko hivyo kuwaletea usumbufu na kushundwa kuelewa vizuri masomo yao.
Alisema kama baraza litaishauri vizuri Serikali kuona inasaidia vipi katika kutatua changamoto hiyo ili kuwa na usafiri maalumu kwa wanafunzi wa shule za kawaida ili kuwawezesha kuondokana na usumbufu unaojitokeza na kusababisha Wanafunzi kurubuniwa na baadhi ya madereva wanaowapa lifti.
Alisema hivi sasa wanafunzi wanarubuniwa sana na baadhi ya madereva ambao siyo waaminifu ambapo huwapa msaada wa usafiri kutokana na wanafunzi hao kusimamisha kila gari kutokana na magari mengi ya abiria kuwakataa wanafunzi kwa madai kuwa wanapata hasara kwa kuwajaza kwenye gari moja.
Aidha alitoa wito kwa baraza hilo kushirikiana bega kwa began a Serikali pamoja na taasisi zingine ili kutatua kero mbali mbali za wananchi kuhusiana na usafiri ambapo aliongeza kuwa magari mengi ni chakavu na bado yanaendelea kutoa huduma pamoja na mwendo kasi unaosababishwa na baadhi ya abiria kumchochea Dereva kuongeza mwendo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Taifa, Oscar Kikoyo alisema katika kuondoa baadhi ya wanafunzi hususani wa kike kurubuniwa na madereva kutokana na kupewa misaada katika magari yao Baraza limeanza kuunda Vilabu vya Mabaraza katika mashule kwa lengo la kutoa elimu.
Aliongeza kuwa kazi ya Baraza siyo kukamata magari yanayofanya kinyume na taratibu za usalama barabarani bali kazi yao ni kushauri na kutoa elimu kwa wasafiri juu ya haki zao ili serikali kupitia vyombo vyake iweze kuchukua hatua.
Alisema Mkoa wa Mbeya ni wa Saba kuzindua Baraza hilo ambapo baada ya kuzinduliwa rasmi wataanza kazi kwa kuwasilisha na kupokea maoni ya watumiaji wa usafiri, kupokea na kusambaza maoni na taarifa juu ya haki za watumiaji wa sekta ya usafiri, kushauriana na wadau kuhusu upatikanaji wa huduma bora na kuunda kamati za kushauriana nazo.
Baraza la Mkoa wa Mbeya lilizinduliwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Michael Kadeghe na kuwakabidhi vitambulisho wajumbe Watano wanaounda baraza hilo ambao ni Saidi Madudu ambaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti, Katibu Brandy Nelson na wajumbe wakiwa ni Jimmy Ambilikile, Rosta Kihwani na Oswald Ngulangwa.
Naye katibu wa Baraza hilo Mkoa wa Mbeya, Brandy Nelson ametoa wito kwa wadau wa usafiri Mkoa wa Mbeya kutoa ushirikiano na baraza ili liweze kufikia malengo waliyowekewa kwa kuwasaidia kutoa taarifa na maoni juu ya namna ya uboreshaji wa sekta ya Usafiri Mkoani Mbeya.
|
0 comments:
Post a Comment