Pages


Home » » Watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wanaokabiliwa na kesi namba 1/2014 ya uhujumu uchumi wameanza utetezi wao

Watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wanaokabiliwa na kesi namba 1/2014 ya uhujumu uchumi wameanza utetezi wao

Chimbuko Letu | 14:12 | 0 comments


Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wanaokabiliwa na kesi namba 1/2014 ya uhujumu uchumi wameanza utetezi wao mbele ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa  wa Mbeya Rashid Chaungu.

Watumishi hao ni pamoja na Martin Bakalaza ambaye ni Mhasibu wa Halmashauri,Upendo Atu Sanga Mkurugenzi wa Halmashauri,Afidh Mgagi Mweka Hazina wa Halmashauri,Abiud Fungamtama Afisa Elimu Vifaa na Marther Mgata Afisa Elimu Taaluma ambao kwa pamoja  wanatuhumiwa kwa makosa manane ya kujipatia shilingi 4,750,000/= kwa kutumia madaraka yao vibaya.

Mbele ya Mahakama Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU Nimrod Mafwele aliiambia Mahakama kuwa kwa pamoja wakitumia madaraka ambapo walijipatia kiasi hicho cha fedha kwa kutumia nyaraka mbalimbali mnamo Novemba 6 mwaka 2012 kwa madai ya kuendeshea semina ya wasimamizi wa mtihani wa kidato cha pili na gharama za mafuta kwa ajili ya kusambazia mitihani katika Wilaya ya Mbeya.

Walioanza kujitetea wakiongozwa na Wakili Nguli wa kujitegemea Mika Thadayo Mbise ni Martin Bakalaza,Upendo Sanga na Afidh Mgagi ambapo Mshitakiwa wa kwanza Martin Bakalaza ameiambia Mahakama kuwa yeye alipata maagizo kutoka kwa Viongozi wake kuwa akope pesa kwa ajili ya kufanikisha mitihani kwa kuwa pesa za mitihani zilichelewa kufika kwa wakati.

Bakalaza ameiambia Mahakama kuwa baada ya agizo hilo alikopa pesa taslimu shilingi 4,750,000/=kutoka kwa Mlipa Fedha Sevelina Mwaifwani na kulipa chakula na mafuta kisha kukabidhiwa stakabadhi za malipo katika maeneo husika.

Alipoulizwa na Wakili wa TAKUKURU kwamba taratibu zote zilifuatwa Bakalaza alidai kuwa taratibu zilifuatwa na pesa alizirejesha kwa Sevelina kama alivyokopa awali.

Mshitakiwa wa Pili Upendo Sanga ameiambia Mahakama kuwa yeye kama Mkurugenzi alitoa kibali kwa Bakalaza ili kuazima fedha hizo ili kufanikisha shughuli ya kitaifa hivyo alitimiza wajibu wake ili kutokwamisha zoezi la mitihani kwani fedha za mitihani zitumwa kwenye akaunti ya  shughuli za maendeleo.

Mweka Hazina Afidh Mgagi aliwasilisha utetezi wake mbele ya Mahakama kuwa kama Mweka Hazina aliruhusu fedha hizo zikopwe kokote ili kufanikisha mitihani ya kidato cha pili baada ya kupokea fedha za mitihani katika akaunti tofauti hivyo kama taratibu za fedha zingefuatwa mitihani isingeweza kufanyika hivyo Bakalaza alikuwa sahihi kukopa pesa hizo na alirejesha kwa njia ya masurufu.

Mgagi akiongozwa na Wakili Mbise aliomba Mahakama ipokee vielelezo vya Benki pamoja na Vibali vya kuomba fedha kutoka ofisi ya fedha kama ushahidi na utetezi wake Mahakamani jambo ambalo lilipingwa na Mwendesha Mahitaka Nimrod Mafwele.

Jambo hilo lilizua mabishano ya kisheria kuwa vielelezo vipokelewe au la hali iliyopelekea Mafwele kuomba kuahirisha kesi wakati Afidh akijitetea ambapo Hakimu alipinga hali iliyomfanya Hakimu Chaungu kuahirisha kesi kwa muda ili Mafwele atafakari uamuzi wake.

Mahakama iliendelea kusikiliza utetezi wa Afidh na baadae kupokea vielelezo hivyo kama uetezi wake na pande zote ziliridhia vitumike kama utetezi wake katika kesi hiyo.

Kwa pamoja Watuhumiwa wote watatu waliiomba Mahakama iwaondolee mashitaka yanayowakabili kwa kuwa walikuwa wanatimiza wajibu wao na kwamba hawajamsababishia hasara mwajiri wao kama mashitaka yanavyodai.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 26 mwaka huo wakati Abiud Fungamtama na Marther Mgata watapowasilisha utetezi wao mbele ya Mahakama na dhamana kwa washitakiwa inaendelea.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger