Mganga maarufu wa jadi aliyefamika kwa jina la Shija Ndula
Jinan’gai(35)mkazi wa Mapogolo Kata ya Madibira Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya
ameachana na kazi hiyo na kuamua kusalimisha matunguli yake katika Kanisa la
Nyumba ya Maombi(House of Prayer Shield of faith) Pambogo Kata ya Iyela jijini
Mbeya.
Shija Ndula mwenye familia ya Mke na watoto wanne ambaye sasa
anafahamika kwa jina la Mussa Shija amesema ameitumikia kazi hiyo takribani
miaka saba kabla ya kuamua kuachana na kazi hiyo na kujiunga na Kanisa linaloongozwa na
Mchungaji Isaya Laiser chini ya Kiongozi wake Mkuu Nabii Mulilege Mkombo
maarufu(Mzee wa Yesu) kutokana na kutopata mafanikio katika uganga wa kienyeji.
Akiongea kwa ujasiri mganga huyo amesema kuwa kazi aliyokuwa
akiifanya kwa muda wote huo hakupata mafanikio yoyote licha ya kutoza fedha
nyingi kwa wateja wake kuanzia shilingi laki moja hadi milioni mbili ambazo
alizitumia kwa anasa tu.
Hata hivyo mke wa mganga huyo Debora Mwandu(30) amesema kuwa
yeye anamshukuru Mungu kwa maisha mapya ndani ya Yesu kwani mganga ambaye ni
mume wake aliacha kazi yake ya ufundi wa kushona nguo akidai hapati faida
yoyote na kujiingiza kwenye uganga akidai kuwa mizimu imemwambia huko ndiko
kwenye mafanikio.
Pamoja na kufanya kazi hiyo kwa miaka saba hakuwahi kununua
uwanja wa kujenga nyumba wala kuweka akiba benki huku mambo yao yakienda mrama
kutokana na mapato najisi ambapo wateja wake wengi walikuwa ni wahalifu
wakiwemo majambazi ambao walikuwa wakiomba dawa ili wafanikiwe katika uhalifu.
Baadhi ya wateja walikuwa wanandoa,wanasiasa na
wafanyabiashara ambao walikuwa wakihitaji dawa kwa ajili kuboresha biashara zao
lakini alijua kuwa huo ulikuwa ni utapeli ambao ulikuwa unamkosanisha na Mungu.
Hata hivyo katika kazi hiyo mganga huyo alikutana na
changamoto kutoka kwa walimu wake ambao walidai kuwa ili kuongeza umaarufu ni
vema kutumia viungo vya bindamu hali iliyomkosesha amani kutokana na mauaji ya
banadamu jambo ambalo amepingana nalo na kuamua kumwishia Yesu.
Vitendo hivyo pia viliendana na matumizi ya wanyama pori
ambazo ni nyara za Serikali kama mafuta
ya Simba au ngozi za wanyama hali ambayo aliona ni hatari kwa maisha yake kwani
wakati wowote angeweza kukumbana na mkono wa sheria.
Mganga huyo ametoa wito kwa waganga wa kienyeji kuachana na
kazi hiyo kwani haina tija kwa jamii pia huleta uchonganishi kwa jamii na
kusababisha mauaji yasiyo ya lazima kwa
jamii isiyo na hatia wakiwamo walemavu wa ngozi.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kwamba hivi sasa waganga hao
wamenda mbali zaidi kwa kudai kujihusisha na mtandao wa free mason kwa kudai
kuwaondolea umaskini watu huku wakiwatoza fedha nyingi na wananchi wengi
hutapeliwa kwa matumaini ya kupata utajiri.
Kwa upande wake Mchungaji Laiser wa Kanisa la nyumba ya
maombi amesema ujio wa mganga huyo ni kufuatia mfungo wa mwezi mzima ukiokuwepo
kanisani kwake hivi karibuni,aidha amesema Kanisa lina mpango wa kumnunulia
cherehani ili aendelee kushona aweze
kujikimu kimaisha.
Mussa Shija alimaliza kwa kutoa wito kwa waganga wa kienyeji
kuachana na mila potofu za uchonganishi kwa jamii ili kuleta amani katika
jamii,Mkoa na Taifa kwa ujumla.