Pages


HITILAFU YA UMEME YASABABISHA VIFO VYA MWANAMKE MMOJA NA WANAWE WAWILI.

Kamanga na Matukio | 03:04 | 0 comments
 Sehemu ya masalia ya vyombo na samani zilizoteketea kwa moto kufuatia hitilafu ya umeme iliyopelekea mama mmoja na wanawe wawili nao kutoketea katika Mtaa wa Mapelele,Kata ya Ilemi Jijini Mbeya.
Nyumba iliyoteketea kwa moto baada ya hitilafu ya umeme.(Picha zote na Ezekiel Kamanga)
*******
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Mwanamke mmoja mkazi  wa mtaa wa Mapelele kata ya Ilemi Jijini Mbeya amefariki dunia akiwa amelala chumbani  na wanawe wawili baada ya moto mkubwa kuzuka uliosababishwa na hitilafu ya umeme majira ya saa 4.55 usiku agosti 16 mwaka huu wakati familia hiyo ikiwa imelala chumbani .

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Bw. Barakiel Masaki aliwataja marehemu hao kuwa ni pamoja na Bi.Pendo Paul (23) mkazi wa Ilemi, na watoto wake wawili ambao ni Tekla Paul(4),Aman Paul mwaka mmoja ambao wote walikuwa wamelala chumba kimoja wakati moto unatokea.

Alisema kuwa wakati moto huo unatokea mume wa mwanamke huyo aitwaye Paul Mlelwa alikuwa safarini Jijini Mwanza kikazi kwa muda wa wiki moja sasa toka aondoke na kwamba familia hiyo imehamia katika nyumba hiyo  ya kupanga  mwezi mmoja uliopita.

Akizungumzia tukio hilo barozi wa mtaa huo Bw.Pius Mwampenjele alisema alipata taarifa za ajali ya moto huo ndipo alipoomba msaada kwa majirani ili kuweza kusaidia kuzima moto ambao tayari ulikuwa umeshateketeza vyumba viwili  na familia ya Bw. Paulo ambayo ilikuwa na mke na watoto wawilli waliokuwa wamelala chumbani walishafariki dunia.

Hata hivyo Mwenyekiti wa mtaa wa Mapelele Bw.Christopher Mwakibete alisema kwamba tukio hilo  ni la pili katika mtaa wake kwa muda wa wiki moja  kufutia tukio la kwanza kutokea agosti 14 mwaka huu ambapo watu wawili ambao ni mke na mume walifariki dunia kwa moto uliosababishwqa na hitilafu ya umeme ambayo ilikuwa ni majira hayohayo.

Alisema kuwa matatizo ya umeme katika mtaa wake yamelipotiwa mara nyingi kwa diwani wa kata ya Ilemi na ofisi za Tanesco Mkoa lakini hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa  zaidi ya kutelekeza nguzo za umeme kwa muda mrefu bila utekelezaji .

Aidha ameongeza kuwa uwezo Transifoma umekuwai mdogo kutokana  na wingi wa wateja na mara nyingi umeme umekuwa mdogo na wakati mwingine kuzima kabisa hali ambayo inahatarisha usalama wa wananchi wa eneo hilo.

BREAKING NEWS!! MOTO WATEKETEZA NYUMBA,WATATU WADHANIWA KUFARIKI, TAKUKURU WAMPIGA MWANAMKE

Kamanga na Matukio | 06:05 | 0 comments
*Ajali ya Moto yateketeza nyumba na watu watatu wahofiwa kufariki Ilemi Jijini Mbeya usiku wa kuamkia leo.

*Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa Wilayani Mbarali,Mkoani Mbeya wanadaiwa kumpiga mwanamke wa Kijiji cha Udindilwa,Kata ya Ruiwa baada ya kukataa kupokea hati ya wito ya mumewe na mwanamke huyo kufungua kesi mahakamani yenye nambari RUJ/IR/1058/2012.

*Majambazi yenye silaha yavamia Kijiji cha Isunda,Kata ya Kamsamba,Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Kwa habari zaidi endelea kutembelea Mtandao huu.

WAYA UMEME WATUMIKA KAMA ADHABU KWA WATUHUMIWA - MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:55 | 0 comments
 Sehemu ya Mwili wa Bwana Ibarahim Hassan Matipa, mkazi wa Kijiji cha Kongoro Mswiswi,Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ukiwa umejeruhiwa baada ya kupigwa kwa waya wa umeme na Askari wa Jeshi la Polisi PC Wiston, kwa kosa la kudaiwa kuiba pesa shilingi Milioni 4 mali ya Bwana  Lenard Mwampyate.
 Bwana Ibrahim Hassan anayedaiwa kushirikiana na wenzake sita kuiba pesa shilingi milioni 4,na kupigwa kwa kutumia waya wa umeme.
*****
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbarali.
Jeshi la polisi wilayani Mbarali mkoani Mbeya limeingia katika kashfa ya kutesa na kuzulu miili ya maabusu wanaokamatwa wakiwa salama na kufikishwa katika vituo vyao.

Hali hiyo imebainika baada ya mwananchi Ibrahim Hassan Matipa na wenzake kukamatwa Julai 30, 2012 kwa tuhuma za wizi wa Shilingi Milioni Nne mali ya Leonard Mwampyate alizodai kuwa alizihifadhi katika kiti cha gari yake aina ya Noah yenye nambari T 554 BQB ambayo ilikuwa imekodishwa kwenye harusi ikiendeshwa na mjomba wake Goliath Mwangonji kwa ajili ya harusi.

Akizungumza na mwandishi wetu Bwana Matipa alisema kuwa baada ya kukamatwa walipelekwa katika kituo cha Polisi cha Mswisi wilayani humo na kuanza kuteswa huku wakipigwa na waya za umeme katika miili yao.

Alisema kuwa wakati wanapigwa na askari waliyemtambua kwa jina la PC Wiston, walikuwa wakilazimishwa wakubali kuwa walihusika na tukio hilo la wizi na wao baada ya kuendelea kukataa ndipo wakaendelea kusulubiwa na askari huyo.

Aliwataja wenzake sita ambao nao walipata kipigo kutoka kwa askari huyo kuwa ni Ismail Omary na Rashid Mussa,wengine ni Bagaza Abubakari,Bwana Harusi Omary Mbago,Rashid Musa,Ally Mwangonji ambaye ni dereva na Saidi Silapola.
 
Kwa mujibu wa Askari huyo PC Wiston,amesema pesa hizo zimelipwa shilingi milioni 3 kati ya milioni 4 zinazodaiwa kuibwa na ndipo watuhumiwa wakaachiwa huru bila kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Haki za Binadamu mkoani hapa Bwana Said Madudu,amelaani vikali kitendo kilichofanywa na askari huyo na kwamba taarifa za tukio hilo zimeshafikishwa kwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Diwan Athuman alimuagiza Mkuu wa Upelelezi wa mkoa(RCO) kulishughulikia suala hilo kutokana na yeye kuwa nje kiofisi.

CHADEMA WAENDELEA KUJIZOLEA WANACHAMA WAPYA.

Kamanga na Matukio | 03:40 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbarali.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA),kimeendelea kujizolea wanachama wapya baada ya kufanya mkutano wa hadhara Agosti 8 mwaka huu katika Kijiji cha Kongoro Mswisi,Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.

Mkutano huo ulifunguliwa na Mwenyekiti wa chama hicho wilaya Bwana Peter Mwashite wakiwa na nia ya kutoa shukrani kwa wananchi wa kijiji hicho waliokipigia kura chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 wa kuchangua Rais,Wabunge na Madiwani,licha ya kura kutotosha kukiwezesha chama hicho kuibuka na ushindi.

Aidha,katika mkutano huo viongozi kadhaa wa chama hicho walipanda jukwaani na kunadi sera za chama akiwemo aliyewahi kugombea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Mbarali Bwana Gidawaya Kazamoyo,Diwani wa viti maalumu Lucy Ngonde,Diwani wa Kata ya Kiwira,Wilaya ya Rungwe Bwana Julius Laurent Mwakalibule,Mwenyekiti wa Vijana mkoa Bwana Julius Kasambala na Bi.Agatha John ambaye ni mwenyekiti wa wanawake Wilaya ya Mbeya Mjini.

Katika mkutano huo kadi za wanachama zaidi ya 74 kutokea Chama Cha Mapinduzi(CCM) walijiunga na chama cha CHADEMA.

Akihutubia mkutano huo Diwani wa Viti Maalumu wa wilaya ya Mbarali Bi, Lucy Ngonde,amesema kuwa zaidi ya bilioni 1.4 pesa za Halmashauri ya wilaya hiyo zimefujwa ba kusababisha miradi ya maendeleo kukwama na kwamba pesa hizo ni tofauti ya shilingi milioni 87 zimefujwa na Mweka Hazina wa halmashauri hiyo.

Wakat huohuo amemtaka Mkurugenzi wa wilaya hiyo kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya chaguzi za vitongoji,ambapo imebainika kuwa baadhi ya vijiji vina makaimu wenyeviti kikiwemo Kijiji cha Mswiswi,kitongoji cha Uswafwani hakina mwenyekiti kwa takribani mwezi mmoja mpaka sasa,Majengo Mapya miaka miwili,Mshikamano miaka mitatu na Maendeleo miaka miwili,hali inayopelekea kuzorota kwa maendeleo wilayani humo.

AUAWA KWA TUHUMA ZA UBAKAJI - MBOZI.

Kamanga na Matukio | 03:37 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja anayedaiwa kuwa ni mkazi wa Nambala,Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya ameuawa na kisha kuchomwa moto na kuteketea mwili mzima kwa kile kinachodaiwa kuwa marehemu huyo amekuwa akijihusisha na vitendo vya ubakaji.

Tukio hilo limetokea majira ya saa mbili asubuhi katika Kijiji cha Masangula,Kata ya Nyimbili,wilayani humo siku ya jana Agosti 9 mwaka huu,ambapo marehem.

Marehemu anakadiliwa kuwa na umri kati ya miaka 25 mpaka 30,ambapo wakazi wa kijiji hicho wamedai kuwa marehemu amekuwa akijihusisha na vitendo hivyo vya ubakaji kijijini hapo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana Asalile Mbembela,ambaye amesema tukio hilo ni la mara ya kwanza kutokea kijijini hapo.

Aidha,Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bwana Elinga Kalinga,alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mbozi,hata hivyo hakuna mtu hata mmoja aliyejitokeza kuhusiana na tukio la ubakwaji.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa Diwani Athuman,amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kutoa wito kwa wananchi kutojichukulia sheria mkononi,hali inayopelekea kusababisha mauaji.

Hata hivyo amesema pindi wanapomkamata mhalifu au mtuhumiwa wamfikishe kwenye vyombo vya sheria ili kuchukua mkondo wake  na kwamba wananchi wanapaswa kuwa waadilifu kwa kufuata imani zao ambapo zitasaidia kupunguza uhalifu mkoani hapa.

SHUKRANI ZETU ZA DHATI - BOMBA FM REDIO 104.0MHz MBEYA TANZANIA

Kamanga na Matukio | 05:07 | 0 comments

Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa kila Mdau wetu/Msikilizaji wetu wa Kituo cha Redio cha kurushia matangazo BOMBA FM 104.0MHz MBEYA - TANZANIA kwa ushirikiano wenu,hii ni zawadi kwa wadau wote popote pale mlipo.

BOMBA FM REDIO imeibuka mshindi wa nafasi ya pili,huku TBC wakiibuka kama mshindi wa nafasi ya kwanza na MBEYA PRESS CLUB wakiwa katika nafasi ya tatu kwa Vyombo vya Habari vya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika kipengele cha MATANGAZO YA MOJA KWA MOJA katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji yaani Nanenane yaliyofanyika kikanda katika Viwanja vya John B.Mwakangale vilivyopo Jijini Mbeya.

Shukrani nyingine pia ziende kwa Viongozi wa mbalimbali wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wakiwemo Wakuu wa Mikoa,Wabunge,Wakuu wa Wilaya,Uongozi wa TASO,Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA),Taasisi mbalimbali,Vyombo Vya Habari na wafanyakazi wa vyombo hivyo pamoja na viongozi wengine wa Sekta mbalimbali,bila kuwasahau Wafanyabiashara na Wadau wote waliohudhuria maadhimisho hayo..

 *******
Imetolewa na Utawala kupitia Kitengo Cha Promotion.
Bomba FM 104.0MHz
Elimisha & Burudisha!!
+255 755 790 000
+255 656 117 664 
Barua pepe:- bombafm104@yahoo.com

ANGALIA MATUKIO MBALIMBALI YA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKUKUU YA WAKULIMA NA WAFUGAJI(NANENANE ) - MBEYA

Kamanga na Matukio | 05:00 | 0 comments
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abas Kandoro wa kwanza kulia,akifuatiwa na Mgeni Rasmi Dr  Christina Shengoma,ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakifuatilia kwa umaniki matukio mbalimbali katika Kilele cha Maadhimisho ya sikukuu ya wakulima na wafugaji Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ndani ya Viwanja vya John B. Mwakangale jana. Kauli mbiu ya siku ya Wakulima na wafugaji “Nane Nane” kwa mwaka huu ni "KILIMO KWANZA ZALISHA KISAYANSI NA KITEKNOLOJIA ILI KUKIDHI MAHITAJI YA ONGEZEKO LA IDADI YA WATU"
 Haya ni Mambo yale ya nyama choma ndani ya Viwanja vya John B. Mwakangale nane nane.
 Mdau akiwa anaweka sawa kitu cha nyama choma.


 Ndani ya banda la Chuo cha Mbeya Institute of Science and Technology(Mist),katika Viwanja vya John B. Mwakangale.

 Ni Jengo la Mamlaka ya maji hapa 
Mgeni  Rasmi Dr Ishengoma,Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Baadhi ya wananchi kutoka taasisi mbalimbali wakiwa katika maandamano katika maonesho ya sikukuu ya wakulima na wafugaji nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika Viwanja vya John B. Mwakangale mkoani Mbeya.
Baadhi ya wananchi kutoka taasisi mbalimbali katika maonesho ya sikukuu ya wakulima na wafugaji nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika Viwanja vya John B. Mwakangale mkoani Mbeya.
 Wananchi na wadau kutoka taasisi mbalimbali wakitazama maandamano katika maonesho ya sikukuu ya wakulima na wafugaji nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika Viwanja vya John B. Mwakangale mkoani Mbeya.ndamano hayo ya maonesho
 Kauli mbiu ya siku ya Wakulima na wafugaji “Nane Nane” kwa mwaka huu ni "KILIMO KWANZA ZALISHA KISAYANSI NA KITEKNOLOJIA ILI KUKIDHI MAHITAJI YA ONGEZEKO LA IDADI YA WATU"
 Pembejeo kibao zinapita hapa.
 Mgeni Rasmi Dr Christina Shengoma akihutubia wakulima pamoja na wananchi wote wa mikoa inayounda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni pamoja na Iringa,Mbeya,Rukwa,Katavi na Njomba katika sikukuu ya wakulima na wafugaji nanenane.
 Burudani ya Ngoma za asili enzi na jifunze utamaduni wa kabila lako,ili kuendelea kuudumisha utamaduni wa mtanzania.

 Akina mama wakiwa wamevalia mavazi ya Chama tawala yaani Chama Cha Mapinduzi(CCM) nao hawakuwa nyuma ili mradi ni mkereketwa na unapendezewa na sera zake..
 Lile Gari linalotumia Mtungi wa Gesi kutoka MIST ndilo linapita sasa 

 Mwandishi wa habari na mpiga picha wa Kituo cha Televisheni cha ITV Ndugu Festo  akiwa anachukua kwa makini Ngoma za asili katika maonesho ya nane nane.
Picha zote zimepigwa na Ndugu Joseph Mwaisango(Mbeya Yetu Blog.)

TAWI LA CHADEMA LONDON LAZINDULIWA NA VIONGOZI WA MPITO WACHAGULIWA.

Kamanga na Matukio | 04:53 | 0 comments
Viongozi na wanachama wa tawi la CHADEMA London katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa Tawi lao.
---
Siku ya Jumanne  tarehe 7 August 2012, tawi la CHADEMA London lilizinduliwa rasmi. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa kamnda Godbless Lema ambaye pia alijitolea kuwa mlezi wa tawi hilo. 

Pamoja na uzinduzi huo uchaguzi wa viongozi mpito ulifanyika na wanachama wapya walijitokeza na kujiandikisha.

Kwa habari zaidi zihusianzo na tawi la CHADEMA London wasiliana na Katibu Mwenezi Kamanda Chris Chagula au Mwenyekiti wa tawi Kamanda Chris Lukosi.
Kamanda Godbless Lema akiongea machache wakati wa uzinduzi wa tawi la CHADEMA jijini London nchini UK. Katika mambo aliyo yaongea ni pamoja na kujitoela kuwa mlezi wa twai la London na kwa kuanzia alikabidhii pesa taslimu dola za kimarekani 200 kwaajili ya kusaidia shughuli za chama.
Mwenyekiti wa tawi la CHADEMA London kamanda Chris Lukosi akimwaga sera zake wakati wa uzinduzi huo.
 Kamanda Dr. Alex ambaye ni mweka hazina akimwaga sera zake.

Mwenyekiti wa CHADEMA London kamanda Chris Lukosi akimtambulisha bwana Magabe ambaye ndo moja wapo wa watu walio wezesha tawi la CHADEMA kufunguliwa nchini UK.
 Makamu mwenyekiti Liberatus akichukua minutes.
 Katibu wa vijana Emmanuel Lunyama akimwaga sera.

 Mwenyekiti akionyesha uzalendo wa chama chake.
 Jessica Maduhu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake  CHADEMA tawi la London akimwaga sera zake na kushukuru kwa kuchaguliwa.
 Magareth katibu wa Baraza la wanawake la CHADEMA tawi la London akiongea machache.

ULEVI WA KUPINDUKIA WAMSABABISHIA MWALIMU KULALA MSALANI.

Kamanga na Matukio | 04:50 | 0 comments
*Ni katika sherehe za Nanenane,wasamaria wema wamwokoa.
Habari na Ezekiel Kamanga,Chunya.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida kwa kioo cha jamii,Mwalimu Timotheo Samaitu wa Shule ya Msingi Magamba,Kata ya Magamba,Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya,alipoiacha familia yake majira ya saa sita mchana Agosti 8 mwaka huu kisha kulala katika Choo kibovu kwa kile kinachodaiwa na ulevi wa kupindukia.

Mwalimu huyo alitoa kali ya mwaka aple alipoenda kulala katika Kilabu cha Pombe za kienyeji,majira ya mchana na kuamua kuuchapa usingizi fofofo mpaka pale alipoamshwa na watu wasamaria wema.

Watu hao ni pamoja na Kasimu Lupa,Safari Hemson,Mashaka Ilonje na Rafael Andson kwa pamoja walimbeba mwalimu huyo kutoka katika choo cha kilabu hadi nyumbani kwake huku mwalimu huyo akiwa hajitambui.

Mwalimu Samaitu,ambaye pia ni Mwalimu Mkuu msaidizi imedaiwa kuwa amekuwa na tabia ya ulevi wa kupindukia,hali inayodhalilisha taaluma nzima ya Ualimu nchini.

Aidha,taarifa hizo zilifikishwa kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Fabian John,ambaye amethibitisha taarifa hizi,pia Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtakuja Bwana Bahati Athuman Mtwale kwa upande wake amewashukuru wananchi waliotoa masaada wa kuokoa maisha ya mwalimu huyo kutokana na ubovu wa choo hicho.

MWENYEKITI WA KIJIJI AJIUZURU.

Kamanga na Matukio | 04:49 | 0 comments
*Ni baada ya tuhuma za ubadhilifu wa shilingi 180,000/=H
*Akiri kuzilipa mkutanoni pesa anazodaiwa.
*Mjumbe wa Halmashauri ajimegea shilingi 424,400/=

Habari kamili na Ezekiel Kamanga,Mbarali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Azimio Mswisi,Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Bwana Luka Mwanyangwa amelazimika kujiuzuru pamoja na Halmashauri ya kijiji hicho baada ya kukiri kufuja pesa za kijiji hicho jumla ya shilingi 180000,zilizokuwa zimetolewa na mradi wa TASAF kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho.

Mjumbe wa Halmashauri hiyo Bwana Daud Ngwale,anahusishwa kufanya ubadhilifu wa shilingi 424,400 ambapo inadaiwa kuzichukua fedha hizo katika akaunti ya kijiji na kuamua kuzitafuna badala ya kuzielekezea katika mradi uliokusudiwa.

Aidha,katika mkutano uliofanyika kijijini hapo Agosti 4 mwaka huu ulipobainika ufujaji huo na uliazimia viongozi hao kurejshewa pesa hizo mara moja vinginevyo wangefungwa kamba na kupelekwa Polisi ambapo Mwenyekiti Bwana Mwanyangwa alizilipa papo hapo shilingi 180,000 na kutangaza kujiuzuru uongozi huku mwenzake Bwana Ngwale akipewa muda hadi 1gosti 9 mwaka huu awe amezirejesha pesa hizo.

Hata hivyo Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bwana Tito Gerald Joha,amekiri kupokea pesa kutoka kwa mwenyekiti huyo wa kijiji na kujiuzuru kwake anatarajia kutoa muhtasari wa mkutano huo na kuwasilisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwa maamuzi zaidi.

Wakati huo huo,mbali na ubadhilifu huo,halmashauri hiyo imetumia zaidi ya shilingi 200,000 kwa ajili ya kuendesha kesi ya Bwna Robert Mwaigwisa,ambapo rai imetolewa kwa wote waliofanikiwa kwa wananchi kutojichukulia hatua  ya kisheria.

Habari ambazo zilikuwa zikiendelea nje ya mkutano huo zinadai kuwa mwenyekiti alishinikizwa kujiuzuru licha ya Bwana Mwanyangwa,kueleza ya kuwa yeye bado ni mwenyekiti halali wa kijiji hicho.

MTOTO AHOFIWA KUFA MAJI - RUNGWE

Kamanga na Matukio | 06:04 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Rungwe Mbeya.
Mtoto anayefahamika kwa jina la Allan Mwakalasya(17),mkazi wa Kijiji cha Mpandapanda,Kata ya Kiwira,Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya amehofiwa kufa maji baada ya kwenda kuogelea katika maporomoko ya Mto Kiwira.

Tukio hilo limetokea Julai 6 mwaka huu majira ya saa 6 mchana, marehemu akiwa na mwenzake walienda kuogelea katika maporomoko ya mto huo,ndipo alipopiga mbizi mara tatu na mara nne aliingia akiwa ametanguliza kichwa alichukua dakika tano kuibuka na kunyosha mikono juu na kuzama moja kwa moja na mpaka sasa hajapatikana.

Baada ya tukio hilo watoto wenzake walichukua jukumu la kwenda kutoa taarifa kwa mama yake mzazi Bi. Emma Kosiyo(43) na mjomba wake Bwana Albert Mwakajila(60),ambao walienda eneo la tukio na kumtafuta Allan bila mafanikio na kuamua kutoa taarifa katika Ofisi ya kijiji ambapo ilipigwa Mbiu na wananchi kukusanyika eneo hilo la tukio huku wataalamu wa uzamiaji majini wakimtafuta bila mafanikio.

Takribani siku wananchi wameendelea na zoezi hilo na wakati huo wanatarajia kuonana na Viongozi wa kimila ili kusaidia kuendelea kuutafuta mwili wa Allan.

Hata hivyo taarifa hizo zimetolewa katika Kituo cha Polisi cha Kiwira,na Askari wa kituo hicho wameendelea kushirikiana na wananchi kuutafuta mwili huo.

WATU WAWILI WAJERUHIWA NA SIMBA - MBOZI.

Kamanga na Matukio | 06:03 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Watu wawili waishio Kijiji cha Shasya,Kata ya Halungu,Wilaya ya Mbozi Mkoania Mbeya wamenusurika kifo baada ya kujeruhiwa vibaya na mnyama anayedhaniwa kuwa simba kijijini hapo.

Akizungumzia tukio hilo Diwani wa Kata ya Halungu mheshimiwa Samson Simkoko,amewataja waliojeruhiwa ambao wamefahamika kwa jina moja ni pamoja na Nzowa na Simkoko,tukio lililotokea katika msitu wa Shasya wakiwa katika shunguli ya kuwinda Nguruwe Pori mnamo Agosti 6 mwaka huu.

Katika sakata hilo Simba huyo alianza kuwashambulia na katika mapambano hayo watu hao wamejeruhiwa vibaya,licha ya kujikongoja hadi kijijini na kuomba msaada na kukimbizwa katika Hospitali ya Mbozi Mission,ambapo hali zao zimetajwa kuendelea vema.

Aidha Diwani Simkoko alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Halungu,na majeruhi kupewa PF3 kwa ajili ya matibabu na kisha alitoa taarifa katika Ofisi ya Maliasili,Wilaya ya Mbozi na sasa wanafanya msako mkali kwa kushirikiana na wananchi kumsana Simba huyo.

MRISHO NGASSA ATAMBULISHWA RASMI SIMBA - AFANYA MAZOEZI KWA MARA YA KWANZA NDANI YA UZI MWEKUNDU

Kamanga na Matukio | 02:40 | 0 comments

Mchuma mpya aliopewa Ngassa baada ya kusajiliwa na Simba.
Mrisho Ngassa akiingia mazoezini.
Mashabiki wa Simba wakiwa wanampokea mchezaji wao mpya Mrisho Ngassa.
Ngassa ndani uzi mwekundu akiwa na Uhuru Suleiman.
Ngassa akipambana na Amri Kiemba.
Na jezi yake ile ile namba 16.
Wanasimba wakiwa juu ya mawe ya ufukwe wa COCO wakiwaangalia wachezaji wao wakifanya mazoezi.
Hapa Ngassa akiwa amezingirwa na mashabiki wa Simba baada ya kufika makao makuu ya klabu hiyo kutambulishwa
Mrisho Ngassa akiwa na uzi wake mpya baada ya kutambulishwa makao makuu ya Simba
Ujumbe kwa uongozi wa Yanga.
Picha zote zimepigwa na Salehe Ally wa GPL

Katibu Wa Halmashauri Kuu ya Taifa, CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye:Orodha Ya Mh, Tundu Lissu inalenga Kupotosha Tuhuma za Rushwa Zinazowakabili Baadhi ya Wabunge.

Kamanga na Matukio | 05:34 | 0 comments
  KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa, CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akiwa katika pozi mbalimbali alipozungumza na waandishi wa habari, leo, Julai 30, 2012, katika ukumbi wa Sekretarieti,. Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.Picha na Bashir Nkoromo
---
 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinalaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wana siasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.

    Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.

    "Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni  mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na kuongeza;

   "Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii".

    Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.

   "Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti", alisena Nape.

    Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.

    "Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.

     Nape alisema  CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara hiyo.

     "Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.
 
     Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.

    "Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.
 
Kwa hisani ya  LUKAZA BLOG.

WATU 9 WAKAMATWA KUFUATIA VURUGU KATIKA MGOMO WA WALIMU MJI MDOGO WA TUNDUMA - MBEYA

Kamanga na Matukio | 05:32 | 0 comments
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya Diwani Athumani,akizungumza suala la kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha walimu pamoja na walimu wamekamatwa kutokana na tuhuma za kuhamasisha wezao kugoma jambo ambalo ni kinyume cha sheria katika Mji mdogo wa Tunduma Mkoani Mbeya.
*******
Habari na Ezekiel Kamanga, Tunduma.
Watu 9 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya,wakiwemo viongozi wa Chama cha walimu na walimu wenyewe kufuatia vurugu zilizosababisha hasara zaidi ya shilingi milioni 100 wakati wa mgomo wa walimu ulioanza juzi.

Kitendo cha walimu hao kugoma kuingia madarasani kufundisha kwa kushirikiana na wanafunzi walifanya maandamano ya amani ya kudai haki ya masilahi ikiwemo mishahara na tukio linadaiwa kutumiwa vibaya na wahalifu kwani walitumia nafasi hiyo kufanya uhalifu kwa kuiba mali za watu.

Wahalifu hao walichoma ofisi za Halmashauri ya Mbozi ndani ya Mji mdogo wa Tunduma  na kuiba mali zilizokuwemo kama  kompyuta 5 za ofisi, pikipiki yenye namba STK 6264, kumbukumbu na nyaraka mbalimbali.

Wahalifu hao  walivunja milango ya ofisi zote, kuvunja vioo vya magari ya kubebea taka aina FAW  SM 8726, na kuiba betri mbili za gari hilo  na gari dogo aina ya Nissan lenye namba SM 2858 mali ya mamlaka hiyo.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani , aliwataja watuhumiwa hao wanaodaiwa kuhusika na uhalifu  na kusababisha hasara ya shilingi  milioni 117, 515,000  kuwa ni Mexon Mbilinyi(27) mkazi wa Mtaa wa Maporomoko, Akida Kondo(25) mkazi wa Mtaa wa Chapwa, Chalres Rupia(29) mkazi wa Mwaka,Athumani Mgala(39) mkazi wa migombani.

 Wengine ni Stela Garbert(20) mkazi wa Mtaa wa Migombani,Atiliyo Benard(28) mkazi wa Mkurungu nchini Zambia, Nikodemus Exavely(17), Mashaka Amoni(17) wote ni wakazi wa Mtaa wa Kaloleni - Tunduma na James Kabuje(29) mkazi wa Mtaa wa Mabatini - Tunduma.

Diwani, alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuhusika na uhalibifu wa ofisi ya halmashauri ya mji mdogo wa tunduma ikiwa na kuiba mali yenye thamani zaidi ya milioni 100 na kwamba wote kwa pamoja wamefikishwa mahakamani leo.

Akizungumzia suala la kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha walimu pamoja na walimu  alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na tuhuma za kuhamasisha wezao kugoma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Aliwataja wahusika hao kuwa ni Mwalimu wa Patro Mangula na ni Katibu wa chama cha walimu wilaya ya Kyela ambapo inadaiwa kuwa kiongozi huyo alikuwa akishirikiana na watu wengine kupita mashuleni kuhamasisha walimu waliokuwa wanaendelea na kazi ya kufundisha wajiunge na mgomo.

Wengine ni Mwalimu Emanuel Kyejo wa shule ya msingi Mbebe Wilaya ya Ileje na mjumbe wa chama cha walimu wilaya ya Ileje, Anyakingwe Lwinga na mjumbe wa chama cha walimu ambapo wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuhamasisha walimu kugoma.

Aidha, katika uhalifu wa Tunduma, Kamanada Diwani alisema kuwa polisi Mkoani Mbeya kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuokoa Mabati 168, Printa moja na mita mbili za maji, Bendera moja ya Taifa na photocopy mashine.

Pia, Kamanda Diwani alitumia nafasi hiyo kutoa ufafanuzi kwa nini askari wake walitumia  Bomu  na risasi katika vurugu hizo ambapo alisema kuwa Bomu hilo lilitumiwa kulitawanyisha kundi kubwa la watu lililokuwa linazidi kuelekea kwenye ofisi za serikali pamoja na Taasisi za kibenki  na kwamba hakuna madhara yaliyojitokeza.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakiipotosha jamii kuwa askari walitumia bomu kuwatawanya wanafunzi na ndio sababu za wananchi kuanzisha vurugu jambo hilo si kweli kwani bomu lilitumiwa baada ya kundi la wahuni lililokuwa likivamia ofisi na kuiba mali zilizomo ndani,”alisema.

Alisema,  wakati kundi hilo linafanya vurugu tayari wanafunzi walikuwa wamerejea kwenye makao yao lakini kundi hilo la wahuni ndio lilikuwa likizidi kujikusanya na kuendelea kufanya uhalifu huo huku baadhi wakiwa wanaelekea kwenye eneo la Benki.

“Baada ya walinzi wa Benki kuona kundi hilo linaikaribia benki askari walipiga risasi mbili juu ili kuwatawanya na kwamba zoezi hilo lilisaidia kuwarudisha watu hao waliokuwa na lengo la kufanya uhalifu katika benki hiyo ,”alisema

Aidha,  Diwani aliitaka jamii kuondoa mawazo potofu kwamba huenda vurugu hizo zimechangiwa na baadhi ya wanasiasa jambo ambalo si kweli kwani jeshi la polisi linaamini kuwa kundi hilo la uhalifu halina itikadi yoyote ya siasa.

“Polisi inawashikilia watu hao kwa tuhuma za uhalifu na ninaamini watu hawa ni wahalifu hivyo watafikishwa mahakani kwa makosa ya uhalifu tu na wala hakuna siasa,”alisema

 Hata hivyo aliwataka walimu pamoja na viongozi wa chama cha walimu kuacha kuwahamasisha wezao kufanya mgomo kwani wao tayari walitangaza kugoma na wamegoma hivyo kupita mashuleni na kuwakuta wezao wanafundisha na kuwalazimisha kugoma ni uvunjifu wa amani hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa zidi yao.

Kwa upande wao wanafunzi wakiiongea katika mkutano wa hadhara na wamewaomba walimu kurejea kazini kwani wanaathirika kimasomo kufuatia mgomo wao hali wakiwa wanajiandaa kufanya mitihani kwa darasa la nne,saba,kidato cha pili na nne.

Naye,Diwani wa Kata ya Tunduma kupitia tiketi ya CHADEMA  mheshimwa Frank Mwakajoka,amesema hujuma zilizofanywa na vibaka hao hali hiyo haitavumiliwa na kuwataka wakazi wa mji huo kuwa walinzi wa mali za umma,kwa kitendo hicho kimefanywa na watu ambao si wakazi wa Tunduma,hali inayopelekea wakazi kuathirika.

Ameongeza kwa kusema wale wote waliohusika na uhalifu huo kurudisha vifaa vilivyoibwa ili huduma ziendelee kama kawaida,ambapo baadhi ya bidhaa zimeanza kurudishwa  na kukabidhiwa Jeshi la Polisi.
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger