Pages


ABOMOLEWA NYUMBA NA KUCHOMEWA VYOMBO VYA NDANI AKIDHANIWA MSHIRIKINA ILEMI JIJINI MBEYA

Kamanga na Matukio | 02:30 | 0 comments
Wananchi wenye hasira kali wakibomoa nyumba ya mama Atupele Kalile akidhaniwa kuwa mchawi maeneo ya ilemi Mbeya
Kazi ya kubomoa nyumba ya mama huyo inaendelea
Wengine wameshaingia ndani na kuanza kutoa vyombo nje tayari kwa kuvichoma
Mtoto wa mama Atupele akijaribu kuokoa vitu vya mama yake visichomwe moto na wanakijiji
Vyombo vinazidi kutolewa ndani ilivichomwe moto
Tayari wameshaanza kuchoma moto vyombo vya mama Atupele
Mwingine anaendelea kubomoa nyumba ya mama Atupele
Wamefyeka shamba lake lote la mahindi
Wengine wanapongezana kwa kazi waliofanya
Kushoto mama Atupele Kalile anaedhaniwa kuwa ni mshirikina akiwa na mtoto wake




MWANAMKE mmoja aliyejulikana kwa jina la Atupele Kalile (60) mkazi wa Mtaa wa Masewe Kata ya Ilemi Jijini Mbeya amenusurika kifo baada ya wananchi wa Mtaa huo kutaka kumpiga kisha kubomoa nyumba yake wakimtuhumu kwa ushirikina.
  
Wananchi hao kumtuhumu Mwanamke huyo kuhusika na upotevu wa motto mwenye umriwa miaka mitatu(3) (Judith Chengula) aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha Februai 22, Mwaka huu.
  
Kwa mujibu wa wakazi hao walisema Mtoto huyo alipotea majira ya saa 11 jioni baada ya kupoteana na dada yake  Anitha Mgaya wakiwa wametokea kanisani ambapo hadi sasa mototo huyo hakuweza kupatikana licha ya juhudi kubwa za wakazi hao kumtafuta bila Jitihada.
  
Walisema katika vikao kadhaa vilivyoitishwa mtaani hapo kwa ajili ya kutafuta mbinu za kupatikana kwa mtotolakini Mwanamke huyo hakuonesha ushirikiano jambo ambalo lilizua hofu miongoni mwa wakazi hao hali iliyopelekea kuhisiwa kuhusika na tukio hilo.
  
Walisema katika kikao kilichofanyika Machi 23 Mwaka huu majira ya Asubuhi mtaani hapo wananchi hao waliendelea kusisitiza kuwa Mwanamke huyo achukuliwe hatua kwa kuwa ndiye anayehusika na upotevu wa motto ambapo iliamriwa kwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi.
  
Walisema baada ya kufika nyumbani kwake na kufanya upekuzi walikuta vitu vinavyohisiwa kuwa vinahusika na ushirikina ambavyo ni vitovu vya watoto wachanga watatu ambapo Mwanamke huyo baada ya kuulizwa alishindwa kutolea ufafanuzi hali iliyosababisha wananchi kupandwa na hasira na kuanza kumpiga.
  
Kutokana na tukio hilo Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa huo Nedy Mwamlima alimnusuru Mwanamke huyo katika kipigo kutoka kwa wananchi kwa kumpeleka katika kituo kikuu cha Polisi kwa usalama zaidi.
  
Baada ya mtuhumiwa huyo kunusuriwa na kukimbizwa katika kituo cha Polisi wananchi hao hawakupoza jazba zao ambapo waliamua kuteketeza nyumba ya mtuhumiwa ikiwa ni pamoja na kufyeka mazao yaliyokuwa yamepandwa jirani na nyumba yake.
Hata hivyo hasira za wananchi hao hazikuishia hapo bali walimsakama Mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina la Agnes Sika ambaye ni mke wa Mchungaji wa kanisa la Pentecost Groly  kwa madai kuwa ni rafiki wa mtuhumiwa na amekuwa akimfichia siri.
  
Jeshi la Polisi liliwahi kufika eneo laTukio na kumnusuru Agnes asipatwe na madhara ikiwa ni pamoja na kutochomewa nyumba yake ambayo tayari wananchi hao walionekana kuikimbilia kwa ajili ya kutaka kuibomoa.
  
Aidha Jeshi la polisi linaendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano zaidi pamoja na upelezi ambapo Baba mzazi wa Mtoto anayesadikiwa kupotea katika Mazingira ya kutatanisha akisema anamwachia Mungu  baada ya juhudi za kumtafuta kushindikana.

picha na E. Kamanga

Uongozi wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey Jijini Mbeya walalamikiwa kutosikiliza kero na kutolea ufafanuzi,

Kamanga na Matukio | 02:22 | 0 comments
Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey Jijini Mbeya.
 Na Venance Matinya, Mbeya.
Wanafunzi wanaosoma Chuo cha Uuguzi cha Aggrey kilichopo Sido Mwanjelwa Jijini Mbeya wameulalamikia uongozi wa Chuo hicho kwa kutosikiliza kero zao pamoja na kutotoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti wanafunzi hao wanaosomea fani za madawa(Clinical Medicine), meno (Dental), Maabara(Laboratory) na uuguzi(nursing) walisema baadhi ya kero ambazo hazitolewi majibu ya kueleweka ni pamoja na kusajili baadhi ya wanafunzi wasiokuwa na sifa.
Walisema baadhi ya wanafunzi waliosajiliwa katika chuo hicho ni ambao wana alama moja ya D ya ufaulu katika somo la Baiolojia katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha nne  wa taifa hali inayozua wasiwasi juu ya uwezo wa Wauguzi watakatolewa Chuoni hapo bila kuzingatia ufaulu wa masomo mengine kama Kemia na Fizikia.
Waliongeza kuwa mbali na hilo pia Chuo hicho hakina usaji wa kueleweka ambapo wao wanaoneshwa namba mbili ambazo zinasomoka 116 na 117 ambazo zimetolewa na Msajili wa Vyuo(Nacte) hali ambayo  wanadai kuwa itawasumbua katika mitihani yao ya mwisho.
Wanafunzi hao wa Mwaka wa Pili wapatao 120 walienda mbali zaidi kwa kudai kuwa  hata wanapoenda kwenye mafunzo ya Vitendo(Field) hupewa kazi ambazo hawajawahi kuzisoma katika mtaala hivyo kubaki wababaishaji na watazamaji tu bila kujua namna ya kufanya ambapo pia walidai kuwa hata wakiwa kwenye mazoezi hayo hakuna Mwalimu anayepita kufuatilia mwenendo wake.
Walisema katika utaratibu wa kufanya mazoezi ya vitendo wanafunzi walipaswa kupewa fedha za kujikimu ambazo ni Shilingi 150,000/= kwa kila mtu lakini tangu waanze Chuo hicho hawajawahi kupewa fedha hizo ambapo wakidai kwenye uongozi wanashindwa kupewa majibu ya kueleweka.
Kutokana na madai hayo wanafunzi hao wamejaribu kufanya mgomo na maandamano takribani mara mbili ili kushinikiza uongozi kuwapatia majibu ya kueleweka lakini juhudi zao zimekuwa zikigonga ukuta kutokana na jeshi la Polisi kuwahi eneo la tukio na kutuliza jitihada zao na kuendelea kutoa ahadi kuwa watarekebisha.
Februari 28, Mwaka huu, wanachuo hao walijaribu kufanya maandamano kushinikiza uongozi wa Chuo hicho kutolea ufafanuzi madai yote ya wanachuo ambapo uongozi huo uliwaahidi kurekebisha matatizo yote yaliyojitokeza lakini hali hiyo haikufanyika hadi yalipotokea maandamano mengine yaliyozimwa na jeshi la polisi.
Katika maandamano ya hivi karibuni wanafunzi hao walikuja na hoja mpya ambayo walidai kuwa tangu wanafunzi wa mwaka wa kwanza waanze masomo hawajapelekwa kwenye mafunzo ya vitendo kwa zaidi ya mwaka mmoja wakati ilitakiwa kabla yakufunga mwaka wawe wamesoma.
Akijibu tuhuma hizo Meneja wa Chuo hicho Kamugisha alisema Suala la usajili kuwa namba mbili linatokana na Wizara kutoangalia vizuri mtiririko wa usajili ambapo walitoa namba ya mbele na baadaye kujikuta namba moja imerukwa ambayo ni 117 badala ya 116 hivyo kusababisha utata huo.
Alisema kutokana na hilo waliamua kulifuatilia ambapo Wizara  yenyewe ilibaini kufanya makosa ambapo waliamua kuiondoa namba 117 na kuitaka Aggrey kutumia namba 116 ambayo hawajaifuta katika baadhi ya matangazo yao na kuongeza kuwa katika kuwaridhisha wanafunzi waliamua kutuma wanafunzi Wizarani ambao walileta majibu kwa wenzao.
Kuhusu kusajili wanafunzi wasio na sifa bado Meneja huyo alisema tatizo liko  Wizarani ambao wamekuwa wakibadilisha mitaala kila mara ambapo mara ya kwanza walitoa sifa kuwa anayetakiwa kujiunga na masomo ya uuguzi ni lazima awe na ufaulu wa alama ya D katika Somo la Baiolojia.
Aliongeza kuwa  mtindo huo umekuwa ukileta sintofahamu kwa wanafunzi ambao hawajaambiwa utaratibu huo hivyo kusababisha kudai maelezo ambayo baada ya kuambiwa wamekuwa wakisahau na kujikuta wakiendelea kuibua matatizo mengine.
Alienda mbali zaidi kuwa chanzo cha migogoro hiyo ni kutokana na baadhi ya wakufunzi kutuhumiwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi hali iliyosababisha uongozi wa Chuo kuwafukuza kazi jambo ambalo lilileta mvurugano chuoni hapo.
Aliongeza kuwa baada ya kutokea hali hiyo uongozi wa chuo ulilazimika kuwarudisha Wakufunzi hao kuendelea kufundisha licha ya kuonesha utovu wa nidhamu kazini  ambapo uongozi wa chuo umeshindwa kuchukua hatua yoyote.
Hata hivyo kufuatia uwepo wa kashfa hizo chuoni hapo baadhi ya wananchi na wadau wa Elimu wameitupia lawama chuo hicho kwa madai kuwa wanazalisha wauguzi wasiokuwa na sifa huku wakitolea mfano kwa sakata la daktari aliyewahi kumfanyia upasuaji wa Kichwa badala ya mguu.
Waliiomba Serikali kuingilia kati utaratibu wa chuo hicho ikiwa ni pamoja na kukagua sifa za wanafunzi waliojiunga na chuo hicho na wakufunzi waliopo hapo kama wanastahili kuendelea na kazi au kusimamishwa.
Walisema wanachojaribu kukitengeneza ni hatari kwa taifa na vizazi vijavyo kutokana na hatua wanazoenda nazo ambapo wanafunzi wanashindwa kufanya mazoezi ya vitendo na wakienda kufanya mazoezi hayo hushindwa kuendana na mazoezi kwa kile wanachodai kutofundishwa darasani.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii umebaini kuwa wanafunzi hao wanalipa ada ya Shilingi Milioni 1 na Laki mbili (1,200,000/=) kwa mwaka kiwango ambacho ni kikubwa kulingana na hali ya uchumi wa Watanzania wengi ilivyo sasa.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Chuo hicho Neema Mwambusi alipopigiwa kuhusiana na tuhuma za chuo hicho aliishia kujibu kuwa matatizo hayo yapo lakini yanapaswa kumalizwa kiubinadamu bila ya kuhofia uchumi wa wazazi na  kizazi kinachozalishwa kutokana na elimu inayotolewa chuoni hapo.

Aoa Mwanafunzi wa kidato cha pili kwa Ng’ombe 45.

Kamanga na Matukio | 02:21 | 0 comments
·       Aoa Mwanafunzi wa  kidato cha pili kwa Ng’ombe 45.
·       Atishia kuua wanaomfuatilia.
·       Mwanafunzi arudishwa kwa wazazi wake kukwepa mkono wa Sheria.
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mtu mmoja mkazi wa Kijiji cha Mpona Kata ya Totowe Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya anatuhumiwa kumwachisha masomo mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Totowe    kwa kumuoa  kisha kumpa ujauzito.
 
Mwananchi huyo aliyefahamika kwa jina la Shigala Mwachanya anatuhumiwa kutenda kosa hilo kwa kumpa ujauzito mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Ngolo Jiguma(19) ambaye amesitisha masomo yake kutokana na ujauzito alionayo ambapowazai walipatana kulipana Ng’ombe 45 kama fidia ambapo tayari Ng’ombe 20 wameshatolewa.
 
Aidha kutokana na Mwanafunzi huyo kutambua kuwa  Wazazi wake wametenda kosa ameamlia kuto hudhulia kliniki katika kituo cha afya cha Malangali na badala yake amekuwa akienda katika Zahanati ya Totowe ili kukwepa kukutwa na vyombo vya sheria.
 
Uongozi wa  Kijiji hicho umeanza kulifuatilia sakata hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Shule aliyokuwa akisomaMwanafunzi huyo Frank Mwakisyala ambapo juhudi hizo zinaonekana kugonga ukuta kutokana na kutishiwa kuawa na mtuhumiwa.
 
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Yaledi Mwanguku aliwaambia waandishi wa Habari kuwa suala hilo lipo juu ya uwezo wake hivyo alilazimika kulipeleka suala hilo kwenye uongozi wa kata kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
 
Diwani wa Viti Maalumu kata hiyoChristina Kibwana ambaye alionekana kulipokea suala hilo na kuanza kulifuatilia pia alidai kuwa alipokea ujumbe mfupi wa maandishi ukimtaka ahame kijijini hapo lasivyo aache kulifuatilia sakata hilo na asipoachaangeuawa.
 
Diwani huyo alisema ujumbe huo wenye maneno ya kutishia yalikutwa kwenye barua nje kidogo nje ya nyumba yake ambapo aliongeza kuwa baada ya kuona hali hiyo aliamua kutoa taarifa katika kituo  kidogo cha Polisi cha Galula Wilayani Chunya.
 
Diwani huyo aliendelea kulalamika kuwa baada ya kutoa taarifa katika kituo hicho hakuna dalili wala hatua zozote zilizochukuliwa ambapo alisema kuna dalili za Rushwa ambayo inasemekana kuwa Polisi walipewa Rushwa ya Shilingi Milioni Moja na Nusu(1500,000/=).
 
Alisema kutokana na kutoonekana kwa hatua zozote aliamua kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Chunya ambapo walimkamata mtuhumiwa huyo kisha kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Chunya.
 
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Totowe kupitia Chama cha Mapinduzi, Godian Wangala  alithibitisha kutokea kwa matukio yote hayo na kuongeza kuwa amesikitishwa na kitendo cha Mwananchi huyo pamoja na wazazi kwa kumwachisha masomo na kumsababishia Mwanafunzi kumnyima haki ya kupata elimu.
 
Alisema Elimu ni haki ya msingi ambayo ingeweza kumkomboa kifikra na Serikali kufikia malengo yake ya kutoa elimu kwa wote kwa kuhimiza ujenzi wa shule za kata na kuongeza kuwa Mwanafunzi huyo amekuwa akiyumbishwa kutokana na kukatishwa mahudhurio ya Kliniki.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani  amekiri kupokea taarifa hizo na kuahidi kulifanyia kazi kwa ukaribu zaidi na kuhakikisha wahusika watachukuliwa hatua zinazostahili.

WANANCHI WA KATA YA MAGAMBA WILAYANI CHUNYA WAIKATAA TAARIFA YA MAPATO NA MATUMIZI YA KATA YAO

Kamanga na Matukio | 02:26 | 0 comments

Kapala  Chakupewa Makelele Diwani wa kata ya Magamba Chunya na pia ndiye mwenyekiti wa ccm na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya chunya ndiye taarifa yake ya mapato na matumizi imekataliwa na wananchi wake
Kaimu mtendaji wa kata ya Magamba Festo Pandisha akijaribu kuwafafanulia vizuri taarifa hiyo ya mapato na matumizi 
Wananchi wakiwa makini kuwasikiliza viongozi wao wakiwasomea mapato na matumizi ya kijiji chao
Mwenyekiti naona hapo unapindisha mahesbu kuwa mkweli kama pesa mmetafuna tupe jibu la uhakika
Waheshimiwa hapo mbele naona mnatuyumbisha leo tunataka kujua ukweli wa pesa zetu
Naombeni mkajipange upya hatukubali hayo mahesabu
Kila mwananchi alinyoosha kidole kwa meza kuuu kupinga taarifa hiyo
Huku kikao kikiendelea vinywaji moto na baridi viliendelea kuuzwa katika mkutano huo ambao umefanyika kilabuni 
Mambo yanaendelea kikaoni hapo hivi kweli kikao kufanyikia kirabuni ni sawa? maana hatuna uhakika kila litakaloongewa hapo likaungwa mkono maana wengi watakuwa tayari wamelewa

WANANCHI wa kata ya Magamba Wilaya ya Chunya Mkoani hapa wameikataa taarifa ya mapato na matumizi iliyosomwa na Diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
  
Mwenyekiti huyo Kapala Chakupewa,alipatwa na mkasa huo hivi karibuni alipokuwa akiwasomea wananchi mapato na matumizi ya kata hiyo kutokana na utaratibu wa Serikali unaotaka wananchi kujua matumizi ya fedha walizochanga kwa ajili ya matumizi ya shughuli za maendeleo.
  
Taarifa iliyokataliwa na wananchi hiyo ilikuwa ni taarifa ya miezi sita(6) iliyokuwa inahusu mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo kutokana na mchango wa wakazi hao ulioanza kuchangishwa tangu mwaka 2007 na kufikia jumla ya Shilingi Milioni 7.
  
Sababu za wananchi hao kukataa taarifa hiyo ni kutokana na kile walichodai kuwa fedha hizo hazijafanya kazi yoyote ambapo Mwenyekiti huyo alisoma kama fedha hizo zimetumika hali iliyosababisha wananchi hao kuhoji eneo walilotumia fedha hizo ambapo baadaye Mwenyekiti huyo alibatilisha kauli yake kuwa hazijatumika.
  
Aidha wananchi hao wameendelea kuhoji kuwa ni kwa nini fedha za umma zitunzwe mikononi mwa watu binafsi badala ya kutunza katika taasisi za fedha pamoja na kutoanza kwa ujenzi huo kwa zaidi ya miaka Mitano tangu waanze kuchangishwa fedha hizo.
  
Hata hivyo kutokana na kutoridhika na mwenendo wa matumizi ya fedha hizo wananchi hao kwa ujumla wao waliamua kuwa ujenzi wa kituo cha afya usitishwe na fedha zilizochangwa zirejeshwe kwa kila kijiji kulingana na michango yao.
  
Akijibu tuhuma hizo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Magamba, Mwenyekiti huyo Kapala Chakupewa, amesema sababu za kutoanza kwa ujenzi huo kwa wakati   ni  kutokana na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kutotoa Gari la kusombea mawe kama walivyokuwa wameahidi awali.
  
Amesema baada ya kuomba gari kwa mkurugenzi aliambiwa gari hilo ni bovu hivyo halitaweza kufanya kazi ya kusomba mawe ndiyo maana ikamlazimu kuahirisha zoezi la ujenzi wa kituo cha afya hadi gari litakapopatikana lenye uwezo wa kufanya kazi.
  
Pia Mwenyekiti huyo amekiri kuwa Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Festo Pandisha kuwa anadaiwa zaidi ya Shilingi Laki nne (400,000/=) ambazo alichangisha kutoka kwa wananchi kwa ajili ya ujenzi wa Shule lakini Mtendaji huyo alisema hajui zilipo licha ya kukiri kuzipokea kutoka kwa wananchi.
  
Aidha pia Mtendaji huyo aliahidi kuzirejesha fedha hizo kwa kununua saruji yenye thamani ya Shilingi laki nne kwa ajili ya ujenzi wa shule lakini hajafanya hivyo hadi siku taarifa ya fedha inasomwa hadi wananchi kuikataa.
  
Kutokana na kauli za Mwenyekiti huyo kuonekana kumtetea Mtendaji na kudidimiza maendeleo ya kata, Wananchi wameamua taarifa hiyo ikaandaliwe upya ili isomwe wiki ijayo na fedha zote zirudishwe kwa ajili ya matumizi mengine ambayo wananchi wenyewe wataamua.
  
Wamesema endapo fedha hizo na taarifa hazitaandaliwa upya na kwa usahihi basi watapeleka malalamiko yao kwenye ngazi za kisheria ili hatua zingine ziweze kuchukua  mkondo wake ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti na Mtendaji kuwajibishwa kwa ubadhilifu na uzembe.
  
Hata hivyo kutokana na mienendo hiyo uchunguzi uchunguzi wa Mbeya yetu umebaini kuwa usimamizi mbovu wa michango ya fedha za wananchi unatokana na   vijiji vinavyounda kata hiyo kutokuwa na Watendaji hali inayosababisha watu binafsi kukamishwa nyadhifa hizo na kuchangisha michango kisha kutokomea nayo.
  
Kata hiyo inayoundwa na vijiji vtatu ambavyo ni Kijiji cha Magamba, Songambele na Nahalyongo vyote  vikiwa vinasimamiwana makaimu Maofisa watendaji kutokana na kutokuwa na Maofisa wa moja kwa moja waliojariwa na Serikali kushika nafasi hizo.

Aidha kutokana na kukosekana kwa maendeleo katika baadhi ya vijiji  umetokana na usimamizi mbovu wa fedha zinazochangwa na wananchi wenye hali ngumu ya maisha licha ya wakazi hao kupenda kufanya shughuli za maendeleo.

Pia baadhi ya wahusika na wasimamizi wa miradi ndani ya vijiji wameshindwa kufafanua na kuelezea namna ya kukomesha hali hiyo inayorudisha nyuma juhudi za wananchi.

Picha na E. kamanga

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger