Pages


WANANCHI WAMUOMBA MKUU WA MKOA KUTATUA MGOGORO WA KUTENGULIWA MWENYEKITI WA KIJIJI - MBEYA

Kamanga na Matukio | 05:43 | 0 comments
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abass Kandoro akihimiza jambo wakati akiongea na waandishi wa habari ofini kwake.
*******
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbarali.
Wananchi wa Kijiji cha Ijumbi, Kata ya Ruiwa Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, wamemuomba Mkuu wa Mkoa Bwana Abbas Kandoro kuingilia kati mgogoro baina ya pande mbili zinazopingana Diwani na Afisa Mtendaji wa Kata wakidaiwa kumuengua Mwenyekiti wa kijiji hicho kwa kutumia madaraka yao.

Kauli hiyo imetolewa na wananchi wa Kata hiyo kawa nyakati tofauti wakati wakiongea na mtandao huu kijijini hapo, ambapo inadaiwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana John Kalikumoyo ameenguliwa uongozi  kutokana na ubadhilifu pia kuitisha mikutano ya hadhara bila kibali na kuzuia wananchi katika shughuli za maendeleo.

Wananchi hao wamepinga madai hayo na kuwa ni njama za mtendaji Kata Bwana Jordan Masweve na Diwani mheshimiwa Alex Mdimilage, kwani ya kudhoofisha juhudi za mwenyekiti huyo kwa kuzuia mianya ya upatikanaji wa pesa kinyume na utaratibu wa makusanyo ya pesa za serikali.

Imedaiwa kuwa Viongozi hao wa kata waliitisha mkutano wa halmashauri ya Kijiji Aprili 17 mwaka huu, wakimtuhumu Bwana Kalikumoyo kwamba ameuza ng'ombe aliyekamatwa kijijini hapo na kujipatia fedha jumala ya shilingi milioni 1,080,000 na makosa hayo yanafanya kupoteza sifa za kuwa kiongozi.

Aidha viongozi hao walimtaarifu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na yeye kuandika barua Aprili 18 mwaka huu, kutengua uongozi wa uenyekiti wa kijiji na kumkaimisha Afisa Mtendaji wa Kijiji.

Katika sakata hilo wananchi wa kijiji hicho wamemuomba Mkuu wa Mkoa Bwana Kandoro, kwenda haraka iwezekanavyo kijijini hapo ili kuleta suluhu kwani wananchi hao wamedai kuwa viongozi hao wa kata Bwana Masweve na Mdimilage ndio wabadhilifu.

Hata hivyo miongoni mwa vitendo vinavyolalamikiwa na wanachi kwa viongozi hao ni pamoja na kujipatia zaidi ya shilingi milioni 24 kutoka kwa wafugaji ambazo hazijaingia katika mfuko wa kijiji, ba kwamba suala hili Mkuu wa mkoa anapaswa kuunda tume ya kuchunguza kwani hawapo tayari kuchangia shughuli za maendeleo kama vile ujenzi wa shule za sekondari, zahanati na maji.

Wakati huo huo wamesema sababu yao ya kutka kususia kuchangia shughuli za maendeleo ni kutokana na viongozi hao kukataa kusoma bajeti ya mapato na matumizi ya kijiji, na badala yake kuwataka viongozi wa Vijiji kusoma taarifa hizo, hali inayowapelekea kuwa na swali kuwa Serikali ya kata haina mapato na matumizi?.

Baadhi ya vijiji vinavyohusishwa kutumiwa na Viongozi hao wa kata ni Motomoto, Malamba, Mahango, Igalako na Udindilwa vyote vilivyopo katika Kata ya Ruiwa.

TUME YA MGOGORO WA ARDHI BAINA YA MWEKEZAJI WA KAPUNGA NA KIJIJI CHA MAPOGORO YAANZA KAZI.

Kamanga na Matukio | 05:42 | 0 comments
Mfugaji Bwana Mungo Makubi (27) kushoto na Singu Mwakami (23) wakimtazama ng'ombe aliyeuawa kwa kugongwa na gari aina ya Toyota Landcruiser lenye nambari ya usajili T 566 BQH. iliyokuwa ikiendeshwa na mwekezaji wa Kapunga Rice Project wilayani Mbarali aitwaye Bwana Gerry Baquzein baada ya kuwakosa wafugaji hao baada ya kujistiri nyuma ya mti na kisha hasira za mwekezaji kuishia kwa kumgonga ng'ombe huyo mwenye thamani ya shilingi laki 6 za kitanzania na kisha kufa papo hapo. (Picha na Maktaba yetu).
*******
Habari Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Tume iliyoteuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Abbas Kandoro, imeanza kazi ya kupima eneo la mipaka ili kujua uhalali wa pande hizo mbili zinazopingana kwa muda wa miaka sita sasa, ambapo kijiji hicho kimeshindwa kufanya shuguli za kimaendeleo kutokana na mwekezaji huyo (Kapunga Rice Project) kuwanyanyasa wananchi hao.

 Wakati tume hiyo ikiwa imeaanza kazi rasmi Aprili 19 mwaka huu, imeshuhudia mwekezaji huyo akibandika matangazo ya kuwataka wananchi wasipite maeneo kadhaa na kwamba atakamata mifugo, baiskeli, pikipiki, magari na waenda kwa miguu na kuwatoza faini watakapokiuka agizo hilo.

Amesema faini hizo zinaanzi shilingi 20,000 hadi 100,000 hali ambayo imepingwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Ramadhan Nyoni pamoja na Halmashauri ya kijiji hicho na kuitaka tume hiyo ione yenyewe ukatili unaofanywa na mwekezaji huyo.

Aidha ni takribani miaka 6 mwekezaji huyo hajaweza kuendeleza kijiji hicho na kuhodhi shule, zahanati, miundo mbinu ya maji na umeme na hivyo kijiji hicho kuwa kama kisiwa na kuwafanya wananchi hao kuishi kama watumwa katika ardhi yao.

Baadhi ya wajumbe walioteuliwa katika Tume hiyo ya uchunguzi ni pamoja na Mwenyekiti Bi Frola Luvanda (Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda), Sospeter Kajuna (Afisa mipango Mkoa), Geofrey Mwaijobele (Afisa Mipango Wilaya ya Mbarali), Omary Mataka (Mpima Ardhi) na Enock Kyando (Afisa Mipango Mkoa).

Wengine ni Saimon Mlimandago na Clemence Mero ambapo tume hiyo itafanya kazi mpaka May 14 mwaka huu katika upimaji wa awali imeoneshwa na wananchi mipaka asili kabla ya kijiji hicho kulikabidhi Shirika na NAFCO ambalo lilipewa ardhi hiyo bure kwa ombi rasmi la Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, 1989 na kuanza rasmi mradi wa umwagiliaji 1993.

Hata hivyo uongozi wa Kijiji umeitaka tume hiyo kutenda haki ili kwani eneo waliloikabidhi NAFCO kipindi hicho ni hekari 5,500 badala ya 7,370 zinazodaiwa hivi sasa na mwekezaji kuwa ndizo alizouziwa ambapo hakunaukweli wowote na kijiji hicho kuonekana kipo ndani ya eneo la mwekezaji.

Wakati huo huo baadhi ya kare wanazozipata ni pamoja na kukamatwa mifugo na kuuawa, kuzuia kupitisha mazao kijijini hapo na mwekezaji huyo kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo na kuwakodisha wananchi, kwa hiyo serikali iangalie upya kwani mwekezaji huyo hainufaishi Kijiji wala taifa.

CCM YAZIDI KUMEGUKA MKOANI MBEYA,

Kamanga na Matukio | 05:43 | 1comments
Mbunge wa Jimbo la Mbozi Magharibi Mheshimiwa David Silinde ambaye naye akiwaasa wananchi kuwa watulivu ili kumsikiliza Makamu wa Rais na kusahau yaliyotokea, ambaye anakuja kwa shughuli za Kiserikali na sio kisiasa na kama kuna tatizo lolote basi ni muda muafaka wa kumuuliza Makamu wa Rais ili kutafutiwa ufumbuzi.(Picha na Maktaba yetu).
*******
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbozi.
Wiki moja baada ya mfululizo  wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Jijini Mbeya kuachia nyadhifa zao kupitia Chama Cha Mapinduzi  (CCM) na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wimbi hilo sasa limebeba sura mpya kwa kuhamia Wilaya ya Mbozi.

 Katika hali isiyo ya kawaida Aprili 25 mwaka huu mchumi wa CCM wilaya hiyo Bi Happiness Kwilabya aliachia wadhifa huo na kujiunga na CHADEMA, akifuatana na wanachama 18 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Kata hiyo maarufu kama uwanja wa malori wilayani hapo.

Wanachama hao walipokelewa na Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya hiyo Bwana Joseph Mwachembe maarufu kama China, ambaye pia Katibu wa Mbunge wa Mbozi Magharibi Mheshimiwa David Silinde.

Akiongea katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi ambao umevuta hisia za watu wengi ambapo Bi Happiness amesema sababu kutoka CCM na kuhamia CHADEMA ni kutokana na mipango mingi inayopangwa si ya utekelezaji na badala yake wamekuwa wakijinufaisha wao binafsi na kuwafanya wananchi kuishi katika hali ya umaskini.

Aidha amezungumzia kero mbalimbali kuwa miradi mingi aliyokuwa akiibuni na kushauri kama mchumi imekuwa ikikwamishwa  na baadhi ya viongozi, ambao wapo kwa maslahi yao binafsi na si chama wala taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amesema hajashawishiwa na mtu yeyote kukihama chama tawala na kwamba amehamia chama kingine ili kuhakikisha anapigania haki na maslahi ya watanzania.

Kwa takribani mwezi mmoja hivi sasa CCM imepoteza zaidi ya wenyeviti wa mitaa wapatao watano, ambao wameamia CHADEMA na mwingine aliposimamishwa kugombea wadhifa huo aliibuka na ushindi wa kishindo katika Mtaa wa Nonde Bwana Ezekiel King, ambaye pia alishawahi kuwa golikipa wa Tukuyu Stars na Mapinduzi Stars ya Mbeya, mtaa anaoishi Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Bwana Athanas Kapunga.

WIMBI LA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI KWA WANANCHI LASHIKA KASI MKOANI MBEYA

Kamanga na Matukio | 05:41 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Wimbi la kujichukulia sheria mkononi kwa wananchi pindi akamatwapo mhalifu limezidi kushika kasi mkoani Mbeya, baada ya wananchi wanaojiita wenye hasira kali kufanya mauaji, pasipo kumfikisha katika vyombo vya dola kuchukuliwa hatua za kisheria.

Tukio hilo limetokea Aprili 24 mwaka huu katika Mtaa wa Airpot Ilembo, Kata ya Iyela Jijini Mbeya ambapo majira ya saa 12 kamili asubuhi, wananchi hao walimuua Simon Samson (34) kwa kutumia vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo chake papohapo.

Baada ya mauaji hao wananchi hao waliuchukua mwili wa marehemu na kuutupia katika korongo lililopo mtaa wa Iyela .

Aidha wananchi hao wamemtuhumu marehemu kuwa ni mwizi katika mtaa huo, ingawa hakukutwa na kitu chochote wakati wa tukio hilo.

Mpaka hivi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na mauaji hayo hali mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Jijini hapa.

Wakati huo huo mtu asiyefahamika jina wala makazi ameokotwa akiwa amefariki na mwili wake kutupwa kando kando ya mto Mita karibu na makaburi ya Sabasaba  jijini hapa na mpaka sasa mwili hakujaweza kutambuliwa.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya Barakiel Masaki amethibitisha kutokea kwa matukio yote mawili na kwamba uchunguzi unafanyika ili kuweza kubaini watuhumiwa.

MWENYEKITI WA MTAA AJIUZULU NA KUHAMIA CHADEMA

Kamanga na Matukio | 05:24 | 0 comments

 Picha ya kwanza Mwenyekiti wa mtaa wa Ilolo Kati Ngambi Ngambi (Kushoto), akifuatiwa na Samson Kibole (katikati) wakiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbeya Bwana John Mwambigija na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilemi Joseph James Mbela, walipokuwa wakipokelewa rasmi kutokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuachia nyadhifa zao katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Ilolo Kati. Picha ya Pili Diwani wa Kata ya Mwakibete (CHADEMA) Bwana Lucas Mwampiki akionesha kadi zilizopokelewa kwa wanachama wa CCM ambao wamejiunga na CHADEMA.
Picha ya Tatu  Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbeya Bwana John Mwambigija na akimtambulisha rasmi aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilemi Joseph James Mbela, mara baada ya kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Picha ya Nne Ngambi K Ngambi akionesha rasmi kadi ya CCM na kumkabidhi Diwani wa Kata ya Sinde mheshimiwa Fanuel Kyanula (CHADEMA) mwenye shati ya rangi nyeusi.
*******
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Wimbi la Wenyeviti wa Mitaa kujuzulu kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuhamia CHADEMA limeingia katika sura mpya, baada ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo Kati Bwana Ngambi K Ngambi naye kujiuzulu.

Tukio hilo limetokea Aprili 24 mwaka huu katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa huo na kuhudhuriwa na baadhi ya madiwani wa CHADEMA jijini Mbeya wakiwemo madiwani wa Kata za Mwakibete, Forest, Sinde ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo.

Akifungua mkutano huo Diwani wa Kata ya Sinde Mheshimiwa Fanuel Kyanula, alitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Sinde ambapo kila mwananchi alikuwa akichangia shilingi 3,000 badala ya shilingi 10,000 za awali.

Aidha mchango huo umesaidia kumalizia kabisa ujenzi wa madarasa hayo, amewashukuru wananchi kwa kuitikia wito wa kuchangia mchango huo bila usumbufu na kipingamizi cochote.

Diwani Kyanula akielezea matumizi ya mchango huo umeweza kukidhi kazi ya upigaji wa sakafu na uwekaji wa nyaya za umeme, hatua hiyo ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri alitoa pongezi kwa na usimamizi mzuri hadi kufikia kukamilika kwa ujenzi huo.

Naye Diwani wa Kata ya Mwakibete Bwana Lucas Mwampiki amempongeza mwenyekiti huyo wa mtaa Bwana Ngambi na kwamba ni kiongozi mchapa kazi, hodari na hivyo wao kwa sasa wamempata Kamanda ambaye ataongoza mapambano dhidi ya ubadhilifu.

Kwa upande wake Bwana Gambi amesema kujiunga kwake CHADEMA ni hiari yake na wala hajalazimishwa na mtu bali ni kuchoshwa ba ukandamizaji ambavyo vilikuwa vikifanywa na CCM naye kwa kuwaonea huruma wananchi aliokuwa akiwaongoza.

Katika mkutano huo watu kadhaa walikabidha Kadi za CCM wakiwemo Rose Mwashilindi (50), Atusekelege Asumbisye (52), ambaye alikuwa balozi wa mtaa huo na Samson Mwakibole.

Katika hadhara hiyo Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbeya Bwana John Mwambigijaaliwapongeza waliohamia kwa hiari yao kujiunga na Chama hicho na kudai kina watu makini ndio maana kimekua kikipata mafanikio siku hadi siku na kutamba 2015 wataichukua dola.

Kuhama kwa Ngwambi aliyekuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Ilemi ni pigo kubwa kwa CCM kwa kipindi cha hivi karibuni kwani Mwenyekiti wa mtaa wa Ilemi Bwana James Joseph Mbela naye alihamia CHADEMA akidia amechoshwa na ufisadi uliokithiri ndani ya CCM.

HAKIMU AVUNJIWA NYUMBA NA KUIBIWA - MKOANI MBEYA

Kamanga na Matukio | 04:59 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mtu au watu wasiofahamika wamevunja na kuiba vitu kadhaa nyumbani kwa Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Mbeya Vijijini Sadiki Mbilu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya Barakiel Masaki, amesema wezi hao walivunja kitasa cha mlango wa nyumba ya hakimu huyo Aprili 23 mwaka huu majira ya 12:30 eneo la Sabasaba Jijini Mbeya.

Baadhi ya vitu vilivyoibiwa ni pamoja na TV flat screen inchi 32, Radio na deki yake aina ya Toshiba, DVD deki aina ya LG na King’amuzi cha Startimes vyote vikiwa na thamani ya shilingi 2,570,000/=.

Hata hivyo Kaimu Kamanda Masakai amemeongeza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini watu waliohusika na wizi.

Wimbi la wizi Mkoani Mbeya limeendelea kukua kwa kasi kubwa siku hadi siku ambapo baadhi ya wezi wamekuwa wakikamatwa na kupigwa na wengine kukuawa hata kwa kuchomwa moto.

AUAWA BAADA YA KUPIGWA NA MCHI WA KUTWANGIA.

Kamanga na Matukio | 04:57 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawatafuta watu watatu kwa kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Shinde Guda (33), huko Wilaya ya Chunya Mkoani hapa.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Barakiel Masaki amesema marehemu huyo ni makazi wa Kitongoji cha Shinyanga, Kijiji cha Mamba B, Kata ya Lupa, Wilaya ya Chunya ambapo Aprili 22 mwaka huu majira ya saa tatu usiku marehemu alikuwa kuwa kilabuni na aliuawa kwa kupigwa na mchi kisongoni na watu watatu na kufariki papo hapo.

 

Masaki amewataja watuhumiwa hao wa mauji kuwa ni pamoja na Mashaka Chelehani (29), Emmanuel Mwalupembe (20) na Mengu Mwalupembe (18) ambao wote ni wakazi wa Lupa wilayani humo.

 

Hata hivyo watuhumiwa wote kwa pamoja walitoroka kusikojulikana mara baada ya kutenda tukio hilo.

 

Kaimu Kamanda huyo Barakiel amesema msako mkali unafanywa ili kuwakamata watuhumiwa na kwamba chanzo cha mauaji hayo ni ulevi kwani mara kadhaa walionekana katika hali ya kulewa.

ZAIDI YA ABIRIA 40 WANUSURIKA KIFO MKOANI MBEYA, BAADA YA BASI LAO KUGONGWA NA KUPINDUKA.

Kamanga na Matukio | 05:34 | 0 comments
Mmoja wa majeruhi wa  kati ya 40 walionusurika kifo baada ya basi waliokuwa wakisafiri aina ya Coaster, lenye nambari za usajili T 374 AVR, kupinduka lilipogongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.
 Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Imezu wakikwa katika Hospitali ya Rufaa, wakisubiri kupatiwa matibabu, mara baada ya basi aina ya Coaster waliyokuwa wakisafirikia  enye nambari za usajili T 374 AVR, kupinduka lilipogongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.
  Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Imezu wakikwa katika Hospitali ya Rufaa, wakisubiri kupatiwa matibabu, mara baada ya basi aina ya Coaster waliyokuwa wakisafirikia  enye nambari za usajili T 374 AVR, kupinduka lilipogongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Basi aina ya Coaster waliokuwa wakisafiria abiria zaidi ya 40, lenye nambari za usajili T 374 AVR, likiwa limepinduka baada ya kugongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.
 Basi aina ya Coaster waliokuwa wakisafiria abiria zaidi ya 40, lenye nambari za usajili T 374 AVR, likiwa limepinduka baada ya kugongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG.
Basi la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG lililohusika katika ajali, baada ya kuligonga kwa nyuma basi aina ya Coaster enye nambari za usajili T 374 AVR ambapo zaidi ya abiria 40 kunusurika kifo. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.(Picha na Ezekiel Kamanga, Mbeya.)
*******
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Abiria zaidi ya 40 wamenusurika kifo baada ya basi waliokuwa wakisafiri aina ya Coaster, lenye nambari za usajili T 374 AVR, kupinduka lilipogongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa basi la El Saedy likiwa katika hali ya mwendokasi liliharibika mfumo wa breki kutoka eneo la Mlima Nyoka na kuligonga basi hilo dogo kwa nyuma katika mteremko wa Shule ya Sekondari Imezu, hali iliyopelekea basi hilo dogo kupinduka.

Baada ya Coaster kupinduka basi la El Saedy likiwa bado katika mwendokasi liliendelea na safari, kabla ya dereva kufanikiwa kulichepusha kabla halijavuka reli ya TAZARA katika Kijiji cha Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Aidha baadhi ya abiria katika basi hilo dogo walikuwemo wanafunzi 28, wa kike na kiume wakielekea shuleni majira ya saa moja asubuhi, Aprili 23 mwaka huu katika Shule ya Sekondari Imezu.

Mara baada ya ajali hiyo kutokea baadhi ya abiria walikuwemo katika basi hilo dogo walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Jijini Mbeya, ambapo kati yao wamelazwa ili kufanyiwa uchunguzi na wengine wakiruhusiwa kurudi nyumbani.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Mbeya Barakiel Masaki,hakupatikana kuelezea ajali hiyo ingawa dereva wa basi la El Saedy anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.

Wakati huo huo watroto watano waliokuwa wakioga katika mfereji wa Mwanjejele, uliopo Igurusi Wilaya ya Mbarali, Aprili 22 mwaka huu majira ya saa tisa alasiriwaliokota begi lililokuwa linaelea katika maji ya mfereji huo na kukuta maiti ya mtoto mchanga.

Maiti hiyo ikiwa imeharibika vibaya kutokana na kuoza ndipo walipolichukua begi hilo na kulikabidhi katika Kituo cha Polisi cha Igurusi.

Hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo, licha ya wimbi la kuuawa kwa watoto wachanga Mkoani Mbeya limekuwa tatizo hali inayosababisha vifo kwa watoto wasio na hatia.

MHESHIMIWA LOWASSA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI MKOANI MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:33 | 0 comments

Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Monduri Edward Ngoyai Lowassa, akizungumza na Waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa High Class uliopo Mji mdogo wa Tunduma, Wilaya ya Mpya ya Momba mkoani Mbeya, wakati wa Harambee ya kuchangia Ujenzi wa Kanisa la Kisasa la EAGT, ambapo alitoa jumla ya shilingi milioni 10 taslimu na kuahidi kuwapeleka waimbaji watatu nchi ya Israel kwa gharama zake.

SINDANO YA GANZI YAMSABABISHIA MAUTI MTOTO BAADA YA KUCHOMWA KATIKA ZAHANATI BINAFSI, MZAZI AILIPIA SHILINGI 20,000.

Kamanga na Matukio | 01:39 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Sindano ya ganzi yamsababishia mauti mtoto Tumaini Rataniel Mtajiha (5), mkazi wa Kijiji cha Hagomba Kata ya Itaka baada ya kuchomwa na daktari wa zahanati binafsi ya Sisika, inayomilikiwa na mwalimu mmoja katika Mtaa wa Ichenjezya, Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea Aprili 22 mwaka huu majira ya saa tano asubuhi baada ya mtoto huyo kufikishwa katika Zahanati binafsi, akiwa na jipu katika makalio ndipo Daktari alipompokea na kumtoza shilingi 20,000 baba mzazi wa marehemu Bwana Rataniel Mtajiha (45), ili apewe huduma.

Sababu ya kuchomwa sindano ya ganzi ni kutokana na mtoto huyo kuonaonekana ni mwoga hivyo achomwe sindano hiyo, na baada ya kuchomwa mtoto huyo alifariki papo hapo.

Baada ya tukio hilo Bwana Mtajiha alitoa taarifa Kituo cha Polisi Vwawa, ambapo walifika na kumchukua Daktari huyo (Jina linahifadhiwa), mwili wa mtoto na jalada lake pamoja na  sampuli ya dawa alizotumia hadi kwenye Hospitali ya Wilaya ili kufanyiwa uchunguzi majira ya saa 10:00 jioni.

Aidha, baada ya kutafakari kwa kina Hospitali hiyo ya wilaya, walitoa taarifa mkoani na kuagiza mwili ufanyiwe uchunguzi Aprili 23 mwaka huu, baada ya jopo la mkoani kuwasili wilayani Mbozi ili kufanya uchunguzi wa kina.

Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Mbeya hakuweza kupatikana kuthibitisha tukio hili, na hivi sasa Daktari wa Zahanati hiyo anashikiliwa na Kituo cha polisi Vwawa akisubiri uchunguzi kufanyika.

Wakati huo huo baba mzazi Bwana Mtajiha, amesema hakutegemea mwanae kufikwa na mauti kwani, muda wote alikuwa anacheza licha  ya kukabiliwa na jipu hilo.

NDAMA (NG’OMBE) WA AJABU AZALIWA WILAYANI MBOZI. ANA MIGUU 6, MIDOMO 4 NA MACHO MATATU

Kamanga na Matukio | 01:38 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
*Ana miguu sita, midomo minne na macho matatu

Ndama wa ajabu amezaliwa katika Kijiji cha Bara, Kata ya Bara Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya Aprili 19 mwaka huu.

Ndama huyo ambaye bado jinsia yake haijulikani ambapo mmiliki wake hakuwa tayari kutaja jina lake kwa masharti kwamba wazee wa kimila hawajampatia kibali cha kuzungumzia lolote kuhusiana na kiumbe hicho cha ajabu.

Aidha, ndama huyo ana jumla ya miguu sita, midomo minne na macho matatu lakini ana uwezo wa kunyonya kama kawaida.

Wazee wa kimila wa Kijiji hicho wamekuwa wakikutana mara kwa mara ili kupata mustakabali wa tukio la ajabu kijijini hapo.

Wakati wazee hao walikutana ndama huyo akiendelea vema na juhudi za kumtafuta Bwana mifugo wa Kata na Wilaya ya zinafanyika ili kujua sababu za ndama huyo kuzaliwa hivyo.
*****Endelea kutembelea mtandao huu na tutaelekea eneo la tukio kupata picha ya ndama huyo wa ajabu, mara ya kibali kutoka kwa wazee wa mila kukamilika******.

BENKI YA DAMU KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI YAKABILIWA NA UPUNGUFU MKUBWA WA DAMU - MBEYA

Kamanga na Matukio | 01:37 | 0 comments
Habari na Mwandishi maalumu, Mbeya.

Benki ya damu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inakabiliwa na upungufu mkubwa wa damu hali ambayo inahatarisha usalama wa maisha hasa kwa akina mama wajawazito na wagonjwa wanatokanao na ajali ambao wamekuwa wakihitaji damu kwa wingi.



Akiongea na mwandishi wetu ofisini kwake meneja wa benki kuu ya kuchangia damu kanda ya nyanda za juu kusini dokta Baliyima Lelo amesema kuwa benki hiyo inaupungufu wa chupa mia moja za damu salama.



Amesema benki hiyo huitaji chupa mia tatu kila siku za damu salama lakini kwa sasa benki hiyo ambayo husambaza damu katika hospitali zote za mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini imekuwa ikipata lita 200 za damu salama badala ya mia tatu.



Kutokana na tatizo hilo Dokta Lelo ameiomba jamii kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha kwa wagonjwa wenye uhitaji mkubwa wa damu hasa kwa akina mama wajawazito ambao mara nyingi wamekuwa wakionekana kuwa na upungufu wa damu mwilini.

WANAKIJIJI WATIMUA AFISA MTENDAJI WA KAJIJI WAMKAIMIASHA MWANAKIJIJI.

Kamanga na Matukio | 01:36 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Katika hali isiyo ya kawaida wakazi wa kijiji cha Matamba kata ya Isange wilayani Rungwe mkoani Mbeya wamemfukuza kazi afisa mtendaji wa kijiji hicho na kumpachika madaraka mwananchi wa kawaida kushika wadhifa huo.

Uamuzi huo umefikiwa jana wakati wa kikao cha kijiji kilichoketi kujadili hali ya maendeleo ya kijiji hicho ambapo, ilibainika kuwa afisa mtendaji alihusika na wizi wa shilingi milioni moja na laki sita, kujimilikisha saruji za wananchi zilinunuliwa kwa ajili wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya kata na kutumia vibaya madaraka.

Aidha wananchi hao walimchagua Fomen Mwandembo ambaye ni mwananchi wa kawaida kukaimu wadhifa huo hadi hapo Serikali itakapo mleta afisa mtendaji mwingine.

Mwenyekiti wa kijiji hicho John Mwakyoma amesema kuwa huamuzi huo hauwezi kupingwa kutokana na kwamba imekuwa ni tabia ya maafisa watendaji kujimilikisha mali za umma pasipo kuchukuliwa hatua zozote.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Isange Eliasi Mwasambili amesema kuwa baada ya tukio hilo walikubaliana kumwamisha kituo cha kazi afisa huyo badala ya kumfukuza.

Kwa mujibu wa sheria za nchi afisa mtendaji huajiliwa na hapatikani kwa njia ya uchaguzi, hivyo kitendo hicho ni kinyume na sheria na kanuni za utumishi wa umma.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana Mwakyoma amesema anayabariki maamuzi ya wananchi kwani mtendaji huyo wamemuonya mara nyingi lakini lakini amekuwa akikaidi na kudhoofisha nguvu za wananchi na maendeleo kwa ujumla kijijini hapo.

MHESHIMIWA LOWASA ATOA MILIONI 10 KUSAIDIA UJENZI WA KANISA LA EAGT

Kamanga na Matukio | 01:39 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Edward Ngoyai Lowassa ametoa shilingi milioni 10, kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la EAGT lililopo Mji mdogo wa Tunduma, Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya.

Fedha hizo zimetolewa jana katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa hilo, iliyofanyika katika viwanja vya Hoteli ya High Class mjini humo.

Lowasa alitumia zaidi ya dakika 28 pekee kuwepo kwenye viwanja hivyo ambapo amesema kuwa watanazania wanapaswa kuwa na wito wa kujenga nyumba za kuabudu kuliko kujenga zaidi nyumba za starehe zikiwemo Bar.

Amesema kuwa amefurahi kualikwa katika harambee hiyo na kwamba kwa sasa nchi ipo kwenye kipindi kigumu cha uchumi na masuala ya katiba mpya, hivyo amewaomba wakristo kupanga ratiba ya kuiombea nchi ili iendelee kuwa na amani na watanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa uliopo nchini.

Aidha, amesema jambo hilo ni muhimu kwa kila mtanzania akiliombea taifa, Tanzania haitaweza kutokea migogoro na vita za wenyewe kwa wenyewe kama ilivyo kwa mataifa mengine mfano Nigeria.

Baada ya hotuba yake hiyo fupi aliwaita wasaidizi wake jukwaani na kuwaagiza wampande na mfuko wa fedha na kisha akamkabidhi mfuko wa pesa taslimu shilingiu milioni 10, Askofu Keneth Kasanga wa kanisa hilo.

Kwa uapnde wake Askofu huyo alimshukuru Waziri mstaafu Lowasa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Monduli kuwa amejenga nyumba ya Mungu na hawezi kumuacha katika mambo yake yote na mahitaji pia.

Kanisa hilo lina zaidi ya waumini 750, walipanga kuwa na kiasi cha shilingi milioni 750 na siku hiyo zimekusanywa jumla ya shilingi milioni 17.9, huku fedha zilizoahidiwa ni shilingi milioni 15.
Kamanga na Matukio | 01:35 | 0 comments

MWANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE, APEWA MIMBA HALI ILIYOMSABABISHIA KUSHINDWA KUENDELEA NA MASOMO - MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:55 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Iwalanje, Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya Pendo Jacob (17), amepoteza masomo baada ya kupewa mimba na Bwana Shungu Ringston Ndasoni (28), mkazi wa Kijiji cha Hatwelo, Kata ya Iwalanje.

Mwanafunzi huyo amefukuzwa shule hivi karibuni kufuatia wazazi wakeBwana Jacob Mwakambanga (60), na Bi Lomia Jacob miaka (30) kuitwa na Mkuu wa shule na kuambiwa kuwa binti yao ana ujauzito na miezi minne, baada ya kupimwa katika Zahanati ya kijiji hicho na kutakiwa kupeleka barua kwa Afisa Mtendaji wa kijiji ili tararibu za kumkata kijana aliyempa mimba binti huyo akamatwe.

Wazazi baada ya kupewa barua hiyo walikwenda kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Rafael Mwandoje pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji Ibrahimu Mponzi, ambao walimuita mtuhumiwa na wazazi wake na kueeleza suala lililotokea ambapo wazazi wa binti walitolewa nje ya kikao na baadae wazazi wa mtuhumiwa wakaambiwa wamtoroshe mwanae kwasababu kesi hiyo ni mbaya.

Aidha, Bwana Yassin Yuta (32) ametishiwa na viongozi hao na kumzuia asiendelee kufuatilia mambo ya kijiji hicho, baada ya kuonekana mnamo Aprili 17 mwaka huu akiwa na waandishi wa habari baada ya kumshutumu kutoa siri za kijiji hicho kwa vyombo vya habari na kishi kumuoanya kucha mara moja vinginevyo wanamuua.

Kufuatia sakata hilo ukaitishwa mkutano wa hadhara, siku hiyo hiyo na kusimamiwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Mponzi na kutoa agizo kuwa Bwna Yassin asionekane katika kijiji hicho na kuwamuru wananchi wakimuona wachukue sheria mkononi au kuuawa.

Hata hivyo agizo hilo liliwashangaza baadhi ya wananchi wapenda amani kutokana na kiongozi aliyepewa dhamana kuchochochea uhalifu.

Kwa upande wake Bwana Yassin amesema ametishiwa kuuawa na Bwana Mohammed Mwangoka, Shungu Ringston(mtuhumiwa) na Ibrahim Mponzi(Mwenyekiti), ambapo ametoa taarifa katika Kituo cha Polisi Uyole na Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

MWENYEKITI WA KIJIJI AJITOA CCM NA KUHAMIA CHADEMA

Kamanga na Matukio | 05:54 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Ileje.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Itale, Kata ya Itale, Wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya Bwana Weston Mwamahonje, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameacha wadhifa wake na kuhamia Chama Cha Demokrasia na Mwaendeleo (CHADEMA).

Tukio hilo limetokea Aprili 19 mwaka huu majira ya asubuhi baada ya Mwenyekiti huyo kuamua kuishusha bendera ya CCM nakupandisha bendera ya CHADEMA na kuhudhuri na wanachama mbalimbali wa chama hiyo.

Bwana Mwamahonje alikabidhi kadi ya chama tawala kwa Katibu Kata wa CHADEMA.

MVUA KUBWA ILIYONYEESHA WILAYA YA CHUNYA YAVUNJA NYUMBA 16 NA KANISA MOJA.

Kamanga na Matukio | 05:53 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Chunya.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imevunja nyumba kumi na sita na kanisa moja katika Kata ya Matundasi, Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya, Aprili 18 mwaka huu majira ya saa 10 kamili jioni.

Kanisa liliezuliwa paa kutokana na upepo huo la Kanisa la Tanzania  Assemblies of God (TAG) linaloongozwa na Mchungaji Mwanjoka, ambapo ukuta wa upande mmoja wapo ulivunjika na kuanguka hali iliyowasababishia waumini wa tano kujeruhiwa na kisha kukimbizwa katika Hospitali ya wilaya hiyo baada ya kufunikwa na kiusi cha ukuta.

 Waumini hao walikuwa katika shughuli za Ujenzi ambapo upepo mkali ulianguka ukuta na kusababisha mmadhara kwao, amjeruhi hao ni pamoja na Mama Mwashiwawa, Mama Doke na watoto watatu ambao majina yao hayakufahamika mara moja.

Baadhi ya wananchi waliathiriwa na janga hilo wamehifadhiwa na ndugu zao hivyo basi msaada wa karibu unahitajika ili kuwanusuru adha hiyo, kwani wanaupungufu wa chakula na malazi.

Wakati huo huo majeruhi wawili waliojeruhiwa katika sakata la Afisa Mtendaji wa kata hiyo Bwana Joseph Nangale kuhusishwa na ujambazi mwanzoni mwa mwezio huu, ambapo Bahati Sibonike alipingwa risasi miguu yote na Diki Lengai alijeruhiwa miguu yote kwa kupingwa na marugu kufuatia majambazi hao kuvunja duka la Bwna Hamis Choga na kupora milioni 24,300,000.

Sababu za kujeruhiwa kwao ni kutokana na kutoka kwenda kumsaidia Bwana Choga, ambapo Nangale alimpiga Lengai kwa kutumia marungu, hali iliyompelekea kupooza baadhi ya viuongo vyake na Sibonike amekatwa mguu mmoja.

Hata hivyo Afisa Mtendaji huo amekamatwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu mashtaka yanayomkabili.

SUNGUSUNGU WAMTIA ULEMAMVU MWANANCHI

Kamanga na Matukio | 05:42 | 0 comments

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Daudi Mwashitete (40) Mkazi wa Kitongoji cha Lunyego Kata ya Itaka, Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya amepata ulemavu baada ya kupingwa na sungusungu wa kijiji hicho, akidaiwa kuwa ni mwizi wa baiskeli.

Majeruhi huyo alikamatwa na sungusungu hao Aprili 8 mwaka 2011 katika Kijiji hicho akiwa na baiskeli yake, akidaiwa kuonyesha risiti ya baiskeli hiyo na yeye kudai kuwa ipo nyumbani kwake ndipo sungusungu hao walipoanza kumpiga kwa marungu yaliyowekwa misumali kisha kumpiga miguu yote miwili hali iliyompelekea kuvunjika.

Baada ya ukatili huo walimuacha na wao kuondoka na baiskeli yake na zoezi hilo lilisimamiwa na Afisa mtendaji wa kijiji cha Hangomba Bwana Watson Maduguli, ambaye kwa sasa ni Afisa mtendaji wa kijiji cha Bara, Kata ya Bata.

Bwana Mwashitete amepelekwa hospitalini ambapo madaktari walidai akatwe miguu kutokana na kujeruhiwa vibaya miguu hiyo, lakini alikataa na kukimbili kwa Mganga wa Kienyeji ambapo ametibiwa na hivi sasa anaendelea vema.

Aidha taarifa za kujeruhiwa kwake ziliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Itaka na sungusungu hao hawajachukuliwa hatua zozote licha ya Mkuu wa polisi wilaya ya Mbozi kupata taarifa.

Hata hivyo sungusungu hao wameendelea kufanya vitendo vya kikatili katika Kijiji kingine cha Bara, huku Mtendaji wa kata hiyo akifumbia macho na uongozi wa wilaya kutomchukulia hatua zozote pamoja na sungusungu.

Miongozi mwa sungusungu wanaolalamikiwa na wananchi hao ni pamoja na Iman Mdolo, Michael Mkondya, Wicref Mtambo na Malaso.

MWALIMU ALIYEWATAKA WANAFUNZI KIMAPENZI AFUKUZWA KAZI.

Kamanga na Matukio | 05:03 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Samaritan iliyopo mji mdogo wa Mbalizi, Mkoani Mbeya Mwalimu Francis Kita, amefukuzwa kazi baada ya kuwataka kimapenzi wanafunzi watatu wa Kidato cha tatu.

Mwalimu huyo aliyewataka kimapenzi wanafunzi hao kwa nyakati tofauti  alikiri kupokea barua ya kufukuzwa kazi lakini amekanusha kutenda kosa hilo.

Imedaiwa kuwa mwalimu Kita kwa kutumia madaraka na dhamana aliyopewa, alikiuka maadili ya taaluma ya ualimu baada ya kuwataka kimapenzi wanafunzi hao wawili(majina yamehifadhiwa), badala ya kuwafundisha au kuwajenga katika misingi ya kujisomea na malezi.

Hata hivyo mwalimu huyo alitaka kuitekeleza dhamira hiyo katika Ofisi ya shule hiyo kwa vile shule hiyo ni ya bweni, iliyopo nje yanjiji maarufu kama mji wa Mbalizi, Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Baada ya wanafunzi hao kuona wanabugudhiwa waliamua kupeleka malalamiko yao kwa Mkuu wa shule Bi Faraja Mbwana, ambaye naye alitoa taarifa kwa Mkurugenzi wa shule hiyo Bwana Ben Mwasaka ambapo waliweka mtego wa kumnasa kirahisi mwalimu huyo ambaye anasoma pia Chuo Kikuu huria Jijini Mbeya.

Mwalimu huyo alipewa wadhifa huo hivi karibuni  na mara kwa mara amekuwa akilalamikiwa na baadhi ya wanafunzi ambao walidai kupewa adhabu pindi wanapokataa kwenda ofisini kwake.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Bi Mbwana amesema kuwa ni kweli Makamu wake mwalimu Kita amefukuzwa kazi hivi karibuni, ingawa alisema kuwa msemaji mkuu ni Mkurugenzi wa shule hiyo Bwana Mwasaka.

Aidha Bwana Mwasaka hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, kutokana na kuwa nje ya ofisi yake.

Uchunguzi umebaini kuwa Mkurugenzi huyo wa shule anampango wa kumburuza malimu huyo mahakamani kwa kitendo cha kuwadhalilisha watoto kuwalea kama mzazi.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Juma Kaponda amewapongeza watoto hao kwa ujasiri walioonesha na iwe mfano wa kuingwa ili kubaini vitendo viovu vinavyofanywa na walimu au watu waliopewa dhamana ya kuongoza.

Mbali na pongezi kwa wanafunzi hao pia ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuchukua hatua za haraka na makusudi, kutokana na uovu wanaofanyiwa watoto wa kike.

AFARIKI BAADA YA KUNG’ATWA NA NYOKA.

Kamanga na Matukio | 05:02 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Mkazi mmoja wa Narco, Kata ya Utengule Usangu Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Bi Gigwa Chelleh (16), amefariki dunia baada ya kung’atwa na nyoka mwenye sumu wakati akiwa shambani.

Tukio hilo limetokea Aprili 17 mwaka huu majira ya saa nane mchana, marehemu akiwa shambani baada ya kutumwa na mama yake Bi Digina Maleva kuchukua mboga kwa ajili ya kuwaandalia chakula nduguze waliokuwa machungoni.
Marehemu hakurejea mapema nyumbani hali iliyompelekea mama yake kuwauliza nduguze kuwa Gigwa mbona anachelewa kurudi, ndipo baadhi ya marafiki zake walipomjibu kuwa walimuacha marehemu akiendelea kuchuma mboga.
Baada ya kumfualia walimkuta marehemu amefariki huku mwili wake ukiwa umevimba na mguu wake wa kulia ukionesha kugongwa  na kitu kinachodhaniwa kuwa ni nyoka mwenye sumu kali na mwili ulikuwa umeharibiwa na sumu hiyo.
Aidha, mwili wa marehemu ulichukuliwa majira ya saa 11:30 jioni na kupelekwa katika Kituo cha Afya cha Igulusi, ambapo Daktari alibainisha kuwa marehemu amefariki baada ya kung’atwa na nyoka mwenye sumu.
Hata hivyo mazishi ya marehemu Gigwa yamefanyika Utengule Usangu Aprili 18 mwaka huu, na tunaiombea familia hiyo faraja katika kipindi hiki kigumu na roho ya marehemu ilale mahali pema peponi, Amina.
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger